UCHAMBUZI WA MJEMA: Kwa hili, Rais Ruto hajaitendea haki Tanzania, Kenya ituombe radhi

Katika siku za karibuni, mjadala unaoendelea katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ndani na nje ya nchi, umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kauli za Rais wa Kenya, William Ruto, aliyoitoa akigusia hali ya uchumi wa nchi jirani, ikiwamo Tanzania.

Kauli hiyo imeibua hisia na mjadala mpana, hasa ikitafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kuwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na shinikizo la kisiasa analokutana nalo ndani ya nchi yake.

Katika mazingira kama haya, kuna haja kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kulinda heshima ya taifa lao kwa hoja na takwimu sahihi, badala ya kukaa kimya pale nchi inapowasilishwa vibaya kimataifa. Hili si suala la jazba, bali ni wajibu wa kikatiba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 28(1) inaeleza wazi kuwa kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa nchi.

Maana ya kifungu hiki ni pana zaidi ya ulinzi wa mipaka ya kijiografia. Inajumuisha pia kulinda taswira ya taifa kimataifa dhidi ya taarifa au propaganda zinazoweza kupotosha ukweli. Hivyo, pale kauli zinapotolewa na viongozi wa mataifa mengine na kugusa hadhi ya nchi, ni wajibu wa wananchi na wataalamu kujibu kwa hoja, takwimu na staha.

Akizungumzia bei ya mafuta nchini Kenya, Rais Ruto alijibu hoja za wananchi wake waliokuwa wakihoji kwa nini bei hiyo ni ya juu kuliko katika baadhi ya nchi jirani, ikiwamo zile zisizo na bandari. Katika maelezo yake, alitaja nchi kadhaa za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuashiria kuwa tofauti ya viwango vya uchumi ndiyo sababu kuu ya tofauti hiyo ya bei.

Hata hivyo, hoja hiyo imezua mjadala, hasa pale alipodai kuwa Kenya ndiyo nchi pekee katika ukanda huo iliyo katika kundi la uchumi wa kati, huku nchi nyingine zikiainishwa kama zenye maendeleo duni.

Kauli hii inakinzana na takwimu za Benki ya Dunia, ambazo zinaonyesha kuwa Tanzania na Kenya zote zimeainishwa katika kundi la nchi zenye kipato cha chini cha kati (Lower Middle Income Countries).

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Kenya ilifikia hadhi hiyo mwaka 2014, huku Tanzania nayo ikifikia mwaka 2020. Hivyo, kwa mantiki ya viwango vya kimataifa, nchi hizi mbili ziko katika daraja moja la uchumi, ingawa zinaweza kutofautiana katika ukubwa wa Pato la Taifa (GDP) au kipato cha mtu mmoja mmoja.

Ni katika muktadha huu ndipo umuhimu wa mjadala wa kisayansi na takwimu sahihi unapojitokeza. Kauli za kisiasa, hasa zinapotolewa katika mazingira ya presha za ndani ya nchi, zinaweza kukosa uwiano wa kitaalamu na kuleta tafsiri potofu kwa hadhira pana.

Zaidi ya hilo, hoja ya kulinganisha bei ya mafuta inahitaji uchambuzi mpana unaozingatia vigezo mbalimbali, ikiwamo sera za kodi, gharama za usafirishaji, miundombinu, pamoja na mifumo ya udhibiti wa bei katika kila nchi. Bila kuzingatia vipengele hivi, ni rahisi kutoa hitimisho lisilo kamili.

Aidha, katika hotuba hiyo, Rais Ruto aligusia pia suala la miundombinu, hususan barabara, akieleza kuwa kuna tofauti kubwa kati ya Kenya na baadhi ya majirani zake. Hata hivyo, hoja kama hizi zinahitaji kuangaliwa kwa kina kwa kutumia takwimu huru na za kulinganishwa, badala ya kauli za jumla zinazoweza kuacha maswali mengi kuliko majibu.

Kwa upande wa Tanzania, kumekuwa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya barabara, reli na bandari katika miaka ya karibuni, hatua inayolenga kuimarisha uchumi na kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi. Hivyo, mjadala wa kulinganisha nchi unapaswa kuzingatia mwenendo wa muda mrefu badala ya picha ya wakati mmoja.

Kwa ujumla, mijadala ya kikanda ni muhimu katika kujenga uwajibikaji wa serikali kwa wananchi wake. Hata hivyo, ni vyema mijadala hiyo ikajengwa juu ya ukweli na takwimu sahihi, badala ya kauli zinazoweza kuchochea upotoshaji au kuathiri mahusiano ya kidiplomasia.

Kwa Watanzania, somo kubwa ni kujenga utamaduni wa kujibu hoja kwa weledi, utulivu na ushahidi. Kulinda heshima ya taifa si kwa kelele, bali kwa ukweli. Na katika enzi ya taarifa za haraka, ukweli huo unapaswa kuwasilishwa kwa umakini mkubwa zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo la Aprili 20, 2026, Rais Ruto, akizungumza katika ibada ya Kanisa la PAG Karen jijini Nairobi, alieleza kuwa kodi ya mafuta nchini Kenya inatumika kugharamia ujenzi wa barabara.

Katika hotuba hiyo, alinukuliwa akisema Kenya ina takribani kilometa 20,000 za barabara za lami zinazohudumiwa, huku kilometa 6,000 zikiwa katika hatua ya ujenzi.

Aidha, alidai kuwa ukijumlisha mtandao wa barabara za lami katika nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), haziifikii hata idadi hiyo ya kilometa 20,000.

Kauli hiyo imeibua mjadala mpana, hasa ikilinganishwa na takwimu zinazotolewa na mamlaka za kitaifa na taasisi huru za uchambuzi. Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alijitokeza hadharani Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu hali halisi ya miundombinu ya barabara nchini.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Tanzania ina jumla ya mtandao wa barabara uliotangazwa rasmi (gazetted) unaofikia kilometa 182,000. Kati ya hizo, kilometa zaidi ya 16,000 ni barabara za lami zinazopatikana mijini na vijijini. Aidha, kuna miradi ya barabara za lami yenye urefu wa kilometa 5,100 inayoendelea kujengwa katika hatua mbalimbali, pamoja na kilometa 3,700 ambazo tayari zimepangiwa makandarasi.

Takwimu hizi zinatoa taswira tofauti na ile iliyowasilishwa katika hotuba ya Rais Ruto na kuibua swali la msingi kuhusu umuhimu wa usahihi wa taarifa katika mijadala ya kikanda. Ni wazi kuwa kulinganisha nchi kunahitaji kutumia vigezo vinavyofanana na takwimu zilizoidhinishwa, badala ya kauli za jumla zisizo na rejea za kitaalamu.

Zaidi ya hapo, Waziri Ulega alibainisha kuwa Tanzania ilirithi chini ya kilometa 600 za barabara za lami wakati wa uhuru, na kwamba zaidi ya kilometa 15,000 zimejengwa na Watanzania wenyewe katika kipindi cha baada ya uhuru. Hii inaonyesha juhudi za muda mrefu za uwekezaji katika miundombinu, ambazo haziwezi kupuuzwa katika mjadala wa kulinganisha nchi.

Katika diplomasia ya kisasa, lugha na takwimu vina uzito mkubwa. Kauli zinazoweza kuonekana kama za kisiasa ndani ya nchi zinaweza kuwa na athari pana zaidi zinapotafsiriwa kimataifa. Ndiyo maana taasisi za uhakiki wa taarifa kama Africa Check zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa kuthibitisha takwimu kabla ya kuzitumia katika mijadala ya umma.

Aidha, suala la hadhi ya nchi ndani ya EAC linapaswa kuangaliwa kwa umakini. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania na Kenya zote zipo katika kundi la nchi zenye kipato cha chini cha kati. Hivyo, matumizi ya lugha inayoweza kudhoofisha hadhi ya mshirika mwingine hayajengi misingi ya ushirikiano wa kweli wa kikanda.

Mjadala huu pia unaangazia changamoto pana zaidi ya mawasiliano ya kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kauli zinazotolewa na viongozi zinaweza kuchochea hisia za kitaifa, lakini pia zinaweza kuathiri uhusiano wa kidiplomasia kama hazitazingatia ukweli na staha inayostahili.

Kwa upande wa Tanzania, hoja iliyotolewa na Waziri Ulega inalenga kuweka kumbukumbu sahihi kwa kutumia takwimu zinazoeleweka na kuthibitishwa. Hii ni hatua muhimu katika kujenga mjadala wa afya unaotegemea ukweli badala ya hisia.

Kwa ujumla, tukio hili linatoa funzo muhimu kwa ukanda wa Afrika Mashariki: kwamba ushirikiano wa kweli unahitaji uwazi, uaminifu na matumizi sahihi ya taarifa. Bila misingi hiyo, hata hoja zenye nia njema zinaweza kugeuka chanzo cha msuguano usio wa lazima.

Katika kulinda heshima ya taifa, Watanzania wanapaswa kuendelea kujibu hoja kwa utulivu na ushahidi. Huo ndiyo msingi wa diplomasia yenye nguvu si sauti kubwa, bali ukweli ulio thabiti.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900.