Sintofahamu yatanda uwanja wa dabi Mei 3

MEI 3, 2026, Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), itachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Wakati ratiba ikisema hivyo, kumekuwa na hali ya sintofahamu ya matumizi ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufuatia kauli ya meneja wa uwanja huo, Gabriel Maswele aliposema kuna maboresho yanaendelea, lakini suala la uwezekano wa kuutumia, hana majibu.

Dabi hiyo ya Kariakoo katika duru la pili la Ligi Kuu Bara, Simba itakuwa mwenyeji baada ya ile ya kwanza iliyochezwa Machi Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kumalizika bila ya kufungana.

Simba msimu huu imekuwa ikiutumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam kwa mechi zake za nyumbani katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB, lakini uwanja huo umeon-ekana hauwezi kutumika kwa dabi hiyo.

Hatua hiyo inailazimu Simba ambayo ni mwenyeji kuchagua uwanja mwingine ambao umekidhi vigezo vilivyowekwa na kuthibitishwa na Bodi.

Kanuni ya 9 (2) za Ligi Kuu toleo la 2025, inasema: “Katika mazingira maalum timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi, utam-bulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalum kwa TPLB angalau siku 7 (saba) kabla ya tarehe ya mchezo husika.”

Mmoja wa viongozi kutoka ndani ya Bodi ya Ligi Kuu, amelimabia Mwanaspoti kuwa: “Simba ina viwan-ja viwili ambavyo ni Benjamin Mkapa na ule wa Arusha Sheikh Amri Abeid, tayari walishatuma maombi pale kwa Mkapa ila wanasubiri majibu, lakini huku bado hawajatoa taarifa ya wapi watakwenda ku-chezea.”

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Gabriel Maswele, alisema ni kweli kuna maboresho yanayoendelea uwanjani hapo, ila hawezi kujibu kama unaweza kutumika kwenye mechi hiyo.

“Katibu Mkuu alishatoa tamko la kufunga uwanja, lakini Simba wameleta maombi yao kutaka kuutumia katika mechi ya dabi, ingawa bado tunaendelea na maboresho ambayo yako pazuri japo ‘pitch’ (se-hemu ya kuchezea) bado haijaguswa,” alisema meneja huyo.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Mpaka sasa sina taarifa, mabosi zangu hawajanipa niwa-tangazie, kwa hiyo mashabiki zetu na wa timu pinzani wanashauku, kwa hiyo tuvute subira tukishajua ni wapi tutakuja kuwaambia.”

Mtu mmoja kutoka Simba, ameliambia Mwanaspoti kuwa, klabu hiyo chaguo la kwanza ni Uwanja wa Benjamin Mkapa ndiyo maana wamepeleka maombi ya kuutumia kwa ajili ya dabi hiyo.

“Simba inataka Uwanja wa Benjamin Mkapa ingawa una maboresho, kwa hiyo wamenyamaza kwa sababu bado muafaka haujapatikana na maombi waliyotuma viongozi pale Kwa Mkapa bado hayaja-jibiwa,” alisema mtu huyo.

Hata hivyo, pia kulikuwa na taarifa kwa mechi hiyo kurudishwa tena Zanzibar, lakini Kamshna wa Michezo Zanzibari, Ameir Mohamed alisema: “Mpaka naondoka ofisini (jana) sijapokea taarifa yoyote ya maombi ya uwanja kwa Simba, licha ya kwamba timu zote zipo Zanzibar.”

Simba tayari imeshafika Zanzibar tayari kushiriki Kombe la Muungano ambapo leo Alhamisi itacheza dhidi ya Mafunzo, ikiwa ni mechi ya robo fainali, ikishuhudiwa juzi Jumanne Yanga ikitinga nusu fainali kwa kuichapa Muembe Makumbi mabao 4-0.