Mabadiliko ya makocha Ligi Kuu yazua maswali, wenyewe wataja sababu

KATIKA kipindi cha misimu miwili ya Ligi Kuu Bara 2024-2025 na 2025-2026, mabenchi ya ufundi ya-mekuwa moja ya maeneo yenye mabadiliko makubwa zaidi kiasi cha kuacha maswali kwa wadau na wapenzi wa soka la Tanzania.

Mabadiliko haya hayaji tu kutokana na kufukuzwa kwa sababu ya matokeo mabaya, bali kuna sababu tatu zimeainishwa na wadau na baadhi ya makocha hao wameeleza moja ni presha ya matokeo ya haraka, ambapo klabu nyingi sasa zinataka mafanikio ya papo kwa papo bila kutoa muda wa kujenga timu.

Pili ni makubaliano ya pande zote mbili, ambapo kocha na klabu hukubaliana kuachana baada ya kuona mwelekeo hauendi sawa bila mgogoro mkubwa. Tatu ni soko la makocha ambalo limekuwa na ushin-dani mkubwa, ambapo baadhi ya makocha wameondoka baada ya kupata ofa nono zaidi ndani au nje ya nchi.

Msimu huu wa 2025-2026 ukiwa umefikia raundi ya 19, tayari jumla ya makocha 38 wameshuhudiwa wakizinoa timu 16 za ligi hiyo, hali inayoonyesha kazi hiyo ya ufundi imekuwa kama kaa la moto kwa sasa Ligi Kuu Bara.

Katika kundi la timu 16 za Ligi Kuu, ni Azam, Namungo, Pamba Jiji na JKT Tanzania, pekee ambazo hadi sasa zinasimamiwa na makocha walewale walioanza nao msimu huu. Makocha hao ni Florent Ibenge (Azam), Juma Mgunda (Namungo), Ahmad Ally (JKT Tanzania) na Francis Baraza (Pamba Jiji).

Lakini nyingine 12, zimekuwa chini ya usimamizi wa makocha tofauti 35 tangu msimu ulipoanza hadi sasa.

Hata hivyo, takwimu hizi ni matokeo ya msimu wa 2024-2025 ambapo kulikuwa na dalili za kuongezeka kwa mabadiliko ya makocha katika klabu mbalimbali.

Katika msimu wa 2024-2025, orodha ya makocha walioachana na klabu zao baada ya makubaliano ya pande mbili ilijumuisha majina mengi makubwa na yenye uzoefu.

Fikiri Elias (KenGold), David Ouma (Coastal Union), Youssouph Dabo (Azam FC), Mwinyi Zahera (Na-mungo), Goran Kopunovic (Pamba Jiji), Patrick Aussems (Singida Black Stars), Miloud Hamdi (Singida Black Stars/Yanga), Mbwana Makata (Tanzania Prisons), Paul Nkata na Melis Medo (wote Kagera Sug-ar).

Huku wengine wakiwa Francis Kimanzi (Tabora United sasa TRA United), Abdihamid Moalin (KMC), Mi-guel Gamondi na Sead Ramovic (wote Yanga), walikuwa sehemu ya wimbi hilo.

Katika orodha hiyo, Yanga ilijitokeza kama moja ya klabu zilizopitia mabadiliko mengi ya benchi la ufundi licha ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na Singida BS, KMC na Kagera Sugar ambayo ilishuka daraja.

Hata hivyo, wakati huo bado kulikuwa na baadhi ya timu ambazo hazikufanya kabisa mabadiliko ya ma-benchi yao ya ufundi ambazo ni Simba chini ya Fadlu Davids, JKT Tanzania (Ahmad Ally) na Dodoma Jiji (Mecky Mexime).

Hata hivyo, msimu wa 2025-2026, wimbi hilo limeonekana kuwa kubwa zaidi, jambo linalomaanisha kuwa karibu kila timu imekwishapitia mabadiliko ya kocha au kuwa na zaidi ya kocha mmoja ndani ya msimu mmoja. 

Msimu huu, Simba imekuwa moja ya timu iliyofanya mabadiliko mengi zaidi, ilianza na Fadlu Davids, ambaye hata kabla ya ligi kuanza aliondoka ikiwa ni siku chache baada ya Ngao ya Jamii, kisha timu ika-wa chini ya Hemed Suleiman “Morocco” kwa muda mfupi, ikafuatiwa na Selemani Matola, baadaye Dimitar Pantev na sasa, Steve Barker.

Fountain Gate kwa upande wao walikuwa na Ortega Deniran kabla ya msimu kuanza, kisha Denis Kitambi, Mohamed Isamial “Laizer” na sasa Fred Felix “Minziro”.

Yanga, Mbeya City, KMC, Singida Black Stars na Coastal Union zinafuatia kwa kunolewa na idadi kubwa ya makocha msimu huu ambapo kila moja imekuwa chini ya usimamizi wa makocha watatu tofauti.

Yanga ilianza na Romain Folz kisha ikawa chini ya usimamizi wa muda wa Patrick Mabedi na sasa iko chi-ni ya Pedro Goncalves wakati Coastal Union ilianza na Ali Ameir akafuatia Mohamed Muya na sasa inanolewa na Fikiri Elias.

Mbeya City ilinolewa na Malale Hamsini baadaye ikamchukua Mecky Maxime na sasa Salum Mayanga.

Kwa upande wa KMC, kocha waliyeanza naye ni Marcio Maximo kisha ikawa chini ya Mohamed Abdal-lah ‘Baresi’ na sasa iko chini ya kaimu kocha, Imani Mwalupetelo.

Nayo Singida Black Stars ilianza kuwa chini ya Miguel Gamondi ambaye baada ya kuanza kuinoa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, akarithiwa na David Ouma na kwa sasa kocha mkuu ni Muhibu Kanu.

Timu za TRA United ilikuwa chini ya Kassim Otieno kabla ya Etienne Ndayiragije, Dodoma Jiji ilikuwa chini ya Vincent Mashami kabla ya Amani Josiah, Mtibwa Sugar ilikuwa chini ya Awadh Juma kabla ya Yusuf Chipo, Tanzania Prisons ilikuwa chini ya Zedekiah Otieno kabla ya Shadrack Nsajigwa na Mashujaa ikiwa chini ya Mayanga kabla ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, zote zimekuwa chini ya makocha wakuu wawili kwa nyakati tofauti msimu huu.

Kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids ambaye baada ya kuondoka Simba alitua Raja Casablanca ya Morocco, alisema: “Katika klabu kubwa mara nyingi, matokeo yanahitajika kwa haraka sana. Huna mu-da wa kujenga timu kwa utulivu kama watu wanavyofikiri. Nina furaha kwa sababu nilikuwa na wakati mzuri Simba japo sikumaliza projekti yangu lakini ulifika muda wa kukabiliana na changamoto nyingine na ndio maisha ya mpira yalivyo.”

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, naye alieleza: “Unahitaji muda kujenga timu yenye ushindani, lakini muda huo mara nyingi haupo. Hiyo ndiyo changamoto kubwa ya ukocha hapa.”

Kocha huyo aliongeza: “Kumekuwa na shinda pia ya baadhi ya viongozi kuingilia masuala ya kiufundi, hilo nalo ni tatizo.”

Kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohammed Badru ambaye kwa sasa anasimamia mradi wa Yanga Soccer School, anaongeza kwa kueleza mazingira ya sasa ya klabu nyingi nchini.

“Timu zina mahitaji makubwa sana. Kocha anapokuja anatakiwa afikie viwango vya viongozi. Matokeo yakikosekana, uvumilivu unakuwa mdogo sana,” alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa kocha wa Azam, Yousouph Dabo alisema hali hiyo ni sehemu ya maisha ya ukocha.

“Ukocha ni kazi yenye presha kubwa sana. Wachezaji wanaweza kubaki lakini kocha ndiye wa kwanza kuwajibika matokeo yakikosekana,” alisema.

Aprili 5 mwaka huu wakati Singida Black Stars inavunja benchi zima la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha mkuu, David Ouma sambamba na Meneja Mkuu, Othmen Najjar, taarifa ya klabu hiyo ilisema uamuzi huo ulikuja kufuatia matokeo mabaya yasiyoridhisha katika kipindi cha karibuni kwa wakati huo.

Hivi karibuni Najjar alipozungumza na kituo cha redio cha Mosaique FM kutoka Tunisia, alisema kati ya mambo aliyokumbana nayo klabuni hapo hadi anaondoka ni mgawanyiko, kuingiliwa majukumu na ishu ya masuala ya kishirikina, huku Singida taarifa yake ikisisitiza ni ishu za matokeo yasiyoridhisha.