Simba Queens yaendeleza moto WPL

SIMBA Queens imeendeleza ubabe wa Ligi Kuu ya Wanawake baada ya leo Aprili 22, 2026 kuitandika Fountain Gate Princess mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Ushindi wa leo umeifanya Simba iendelee kusalia kileleni na pointi 40 kwenye mechi 14 ikishinda 13 na sare moja.

Licha ya Simba kuondoka na ushindi huo, lakini Fountain ilionyesha kiwango kikubwa hasa kwa kipa Nusra Khamis aliyeokoa mashambulizi matatu ya hatari.

Hadi dakika ya 86 kipa huyo aliipa matumaini Fountain kuondoka na pointi moja dhidi ya mabingwa mara nne wa Ligi Kuu ya Wanawake.

Licha ya kuokoa michomo hiyo dakika ya 87 Simba walitibua hesabu hizo kufuatia kona iliyochongwa na mshambuliaji Jentrix Shikangwa iliyosababisha beki wa Fountain kujifunga.

Dakika tatu baadaye, Aisha Mnunka akaongeza bao la pili kufuatia kona nyingine iliyochongwa na Zawadi Usanase.

Fountain ilikuwa nafasi ya nne na pointi 20 sawa na Mashujaa na Alliance lakini kipigo cha leo kinaishusha hadi nafasi ya tano huku Wazee wa Mapigo na Mwendo wakipanda nne bora baada ya kushinda leo.

Mechi nyingine zilizopigwa za raundi ya 14, Yanga Princess iliitandika wenyeji mabao 3-0, Ruangwa ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Bunda Queens na Mashujaa ikishinda bao 1-0 dhidi ya Geita Queens.