Farid arejea kiwanjani baada ya dakika 2,880

HATIMAYE winga wa Yanga, Farid Mussa amecheza mechi kwa mara ya kwanza baada ya kuupiga dakika 16 za mwisho wakati Yanga ikiichapa Muembe Makumbi kwa mabao 4-0 katika Kombe la Muungano.

Kama ulikuwa umesahau ni kwamba, mara ya mwisho Farid kuonekana uwanjani akicheza mechi ilikuwa Septemba 12, 2025 kwenye mchezo wa kilele cha Wiki ya Mwananchi dhidi ya Bandari, alipocheza kwa dakika 45 za kwanza

Baada ya mchezo huo, winga huyo wa zamani wa Azam, amezikosa mechi 32 za mashindano tofauti msimu huu ambazo ni sawa na dakika 2,880 akikosekana uwanjani na hata kwenye misafara ya Yanga.

Farid juzi aliingia kuchukua nafasi ya Chadrack Boka dakika ya 74 Yanga ikiwa tayari ilishaweka wavuni mabao manne akicheza kama beki wa kushoto kwenye mchezo huo.

 Ndani ya muda huo, Farid aligusa mpira mara 17 pekee ambapo alipiga pasi zilizofika 15 lakini mbili zikipotea huku akiwa hajaruhusu krosi yoyote ndani ya muda aliocheza kwenye upande wake.

Wakati Farid akiingia, mashabiki walionekana wakimshangilia wakionyesha kwamba ni muda mrefu hawajamuona kwenye jezi za mabingwa hao na kuzusha taarifa tofauti.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema kiungo huyo alionyesha kitu tofauti kwenye mazoezi ambapo aliona ampe mechi hizo za Kombe la Muungano kuboresha uwezo wake.

Pedro alisema changamoto kubwa ambayo anakutana nayo Farid ni ubora wa wanaowania nafasi ambao wamekuwa wakicheza zaidi yake.

“Ni kweli Farid amepata nafasi jana (juzi), ni mchezaji mzuri lakini bahati mbaya sana kwake amekuwa akikutana na wakati mgumu kupata nafasi, lakini hivi sasa ameonyesha juhudi kubwa tumeona tumpe muda wa kucheza kwenye hizi mechi za Muungano,” alisema Pedro.

“Hakuna chuki wakati wa kupanga timu, kitu ambacho naweza kueleza ni suala la ushindani wa nafasi, sehemu nzuri ambayo angeweza kucheza ni kama beki wa kushoto lakini wenzake wamekuwa bora zaidi kwenye machaguo mawili ya juu, hilo ndio tatizo pekee.” 

Kiasili, Farid ni winga, lakini pia ana uwezo wa kucheza beki wa kushoto na amekuwa akitumika mara kwa mara eneo hilo.