Dar es Salaam. Wakati maegesho ya malori jijini Dar es Salaam yakiendelea kulalamikiwa kuchochea foleni za magari barabarani, Serikali imetoa Sh5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa eneo la kisasa la maegesho ya magari makubwa (malori) katika Kata ya Mwandege, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
Uwekezaji huo wa Mwandege, ambao upo umbali wa takribani kilometa 20 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam ni hatua muhimu inayotarajiwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kupunguza msongamano wa magari na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Barabara nyingi ndani ya jiji hilo zikiwemo ile ya Mandela, zimekuwa kero kwa watumiaji hasa nyakati za asubuhi na jioni huku sababu kutokana na foleni kubwa inayotajwa kusababishwa na maegesho ya malori ndani ya mji.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Jumatano Aprili 22, 2026, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesisitiza kuwa ujenzi wa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya usafiri kupitia maegesho hayo, akibainisha kuwa mpango huo haujabadilika na utekelezaji wake unaendelea kama ulivyopangwa.
“Maegesho hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya malori 360 kwa wakati mmoja, jambo litakalosaidia kupunguza msongamano na changamoto ya maegesho ya magari makubwa, huku yakiboresha mtiririko wa usafirishaji wa mizigo,” amesema.
Waziri Ulega ameongeza kuwa, mradi huo unatekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kujenga miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya usafirishaji.
Mbali na kuboresha huduma za usafirishaji, mradi huo pia unatarajiwa kufungua milango ya fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa Mwandege na maeneo ya jirani, ambapo biashara ndogo ndogo zikiwemo za chakula, vinywaji na huduma nyingine za kila siku zinatarajiwa kushamiri katika maeneo hayo, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi.
“Mwandege inakwenda kuwa kitovu kipya cha biashara. Mamalishe, vijana na wananchi kwa ujumla watanufaika moja kwa moja na uwepo wa maegesho haya,” ameongeza Waziri Ulega.
Akifafanua hatua zilizofikiwa katika mradoi huo, ameeleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi uko katika hatua za mwisho, na maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi yanaendelea kukamilishwa.
Katika kuchochea fursa za mradi huo, Waziri Ulega ametoa wito kwa wananchi, hususan vijana na wanawake, kujipanga kikamilifu ili kunufaika na fursa zitakazozaliwa na mradi huo, akisisitiza umuhimu wa kutumia nafasi hiyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo yao na eneo hilo.
