Azam yaifuata Yanga, Ngita akiimaliza KVZ

AZAM FC imefanya kweli ikiichapa KVZ kwa mabao 2-0 na kukata tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Muungano, ikiimfuata Yanga.

Mabao mawili ya mshambuliaji Mkongomani Jean Ngita akifunga moja kila kipindi  yametosha kuihakikishia Azam ushindi huo kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Ngita amefunga bao la kwanza katika dakika ya 40 kwa kichwa cha kudundisha  akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha wa timu hiyo katika mchezo huo, kiungo Yahya Zayd.

Mkongomani huyo amepigilia msumari wa pili dakika ya 54 akimalizia vizuri krosi ya Ashraf Kibeku na kulizamisha jahazi la KVZ

KVZ haikuwa na nguvu ya kuipangua ngome ya Azam licha ya kujaribu kupanga mashambulizi yake, ambapo dakika ya 38 imepiga shuti pekee lililolenga lango, lakini likawa jepesi kwa kipa Issa Fofana aliyerudi langoni baada ya muda mrefu.

Ushindi huo unaipeleka Azam kwenda kukutana na bingwa mtetezi, Yanga, kwenye mchezo wa nusu fainali utakaopigwa Aprili 25, saa 2:15 usiku katika Uwanja wa New Amaan.

Azam kwenye mchezo huo imewatumia wachezaji wengi ambao wamekuwa hawapati nafasi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

KVZ inaungana na Muembe Makumbi City kuaga mashindano hayo, ikiendelea kuonyesha unyonge wa timu za Zanzibar kutolewa dhidi ya zile za Bara.

Mechi hizo zitaendelea kesho kwa michezo miwili kupiga ambapo robo fainali ya tatu itawakutanisha Mlandege dhidi ya Singida Black Stars itakayochezwa kuanzia saa 10 jioni.

Nusu fainali ya tatu itapigwa kunzia saa 2:15 usiku ikiwakutanisha Mafunzo na Simba.