Taasisi za rushwa Afrika zakutana kujadili mikakati mipya

Arusha. Viongozi wakuu wa taasisi za kupambana na rushwa kutoka nchi za Afrika wamekutana jijini Arusha kujadili mbinu na mikakati mipya ya kuziba mianya ya rushwa katika bara zima.

Viongozi hao wa Kamati Tendaji ya Chama cha Mamlaka za Kupambana na Rushwa Afrika (AAACA) wameanza leo, Aprili 13, 2026, katika mkutano wa 13 unaowakutanisha wakuu wa taasisi za kupambana na rushwa kutoka nchi tisa wanachama kwa ajili ya kujadili njia za kuimarisha ushirikiano wa bara zima katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mkutano huo unafanyika wakati ripoti mbalimbali za kimataifa zikionesha kuwa Afrika hupoteza zaidi ya Dola bilioni 100 za Marekani kila mwaka kutokana na rushwa na mtiririko haramu wa fedha.

Pia, tafiti za taasisi za ufuatiliaji wa uchumi zinaonesha kuwa kiwango hicho kinaweza kuongezeka kwa mwaka endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa 13 wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mamlaka za Kupambana na Rushwa Afrika (AAACA) ulianza leo Aprili 13, 2026 jijini Arusha. Picha na Bertha Ismail

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Crispin Chalamila, amesema kamati hiyo inapitia utekelezaji wa maazimio ya awali pamoja na kuandaa ajenda mpya kwa ajili ya mkutano mkuu ujao utakaofanyika Kenya, utakaowakutanisha wawakilishi kutoka nchi 48 za Afrika.

Majadiliano makuu yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uchunguzi, kuboresha mifumo ya kurejesha mali zilizoibiwa, na kuimarisha vyombo vya kisheria vya kufuatilia mtiririko haramu wa fedha.

Wajumbe wa mkutano huo wanatoka Misri, Mali, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Algeria, Sierra Leone, Burundi, Zimbabwe pamoja na wenyeji Tanzania.

Mkutano huo unatarajiwa kupitisha maazimio ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikiano katika mapambano ya rushwa barani Afrika.

Akifungua kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuzuia na kugundua rushwa.

Amesema Tanzania imepiga hatua kwa kuweka huduma nyingi za umma katika mifumo ya kidijitali, hatua iliyopunguza mawasiliano ya ana kwa ana na hivyo kupunguza fursa za rushwa.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa 13 wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mamlaka za Kupambana na Rushwa Afrika (AAACA) ulianza leo Aprili 13, 2026 jijini Arusha. Picha na Bertha Ismail

“Huduma nyingi sasa zinapatikana mtandaoni, jambo linalosaidia kupunguza mawasiliano ya moja kwa moja ambapo rushwa inaweza kutokea.

“Serikali pia inaendelea kuboresha mifumo ya kuripoti ili wananchi waweze kuripoti vitendo vya rushwa kwa usalama,” amesema.

Rais wa AAACA, Hisham El Raqaybi, amesema mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika yanahitaji ushirikiano, dhamira ya kisiasa na mshikamano wa nchi zote.

Amesema rushwa inaendelea kuinyima Afrika rasilimali ambazo zingetumika katika sekta za afya, elimu na miundombinu.

“Hili ni vita ya pamoja, hakuna nchi inayoweza kushinda peke yake, tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja kama waafrika, kushirikiana,” amesema.