Polisi Zanzibar Watoa Taarifa Rasmi Kuhusu Kifo cha Mtalii wa Marekani

Mwanamke raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 31, Ashly Robinson maarufu mtandaoni kama Ashlee Jenae enzi za uhai wake.

Polisi Zanzibar wamethibitisha kuwa kifo cha mwanamke raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 31, Ashly Robinson maarufu mtandaoni kama Ashlee Jenae, hakikutokana na tukio la uhalifu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, uchunguzi wa awali umebaini kuwa hakuna dalili zozote za uhalifu katika tukio hilo lililotokea wakati mwanamke huyo akiwa likizoni nchini Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda Mapujira amesema tukio hilo lilitokea Aprili 9, 2026 katika eneo la Nungwi, ambapo marehemu alikuwa amefikia katika hoteli ya Zuri Zanzibar pamoja na mchumba wake.

Ameeleza kuwa kabla ya tukio hilo, wawili hao waliripotiwa kuwa na kutokuelewana, hali iliyosababisha uongozi wa hoteli kuwatengea vyumba tofauti ili kupunguza mvutano.

“Iliripotiwa kuwa kulikuwa na kutoelewana kati yao, na baada ya hapo uongozi wa hoteli ukaamua kuwatenganisha vyumba, hivyo kila mmoja alikuwa na chumba chake,” amesema Kamanda Mapujira.

Aidha, amesema tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Nungwi baada ya wafanyakazi wa hoteli kubaini hali isiyo ya kawaida kwa mgeni huyo na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mwanamke huyo alipatikana akiwa katika hali mbaya lakini bado alikuwa hai, ambapo alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu kabla ya kufariki dunia siku iliyofuata, Aprili 10, 2026.

Ashly Robinson maarufu mtandaoni kama Ashlee Jenae enzi za uhai wake akiwa na mchumba wake.

Mwili wa marehemu bado upo nchini ukisubiri kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na mipango ya kusafirishwa kurejeshwa nchini Marekani kwa ajili ya mazishi.

Taarifa zilizokuwa zinasambaa awali mitandaoni zilidai uwepo wa tukio la uhalifu, lakini jeshi la polisi limezitupilia mbali taarifa hizo na kusisitiza kuwa uchunguzi wao haujaonesha ushahidi wowote wa tukio la jinai.

Kwa mujibu wa familia na taarifa za karibu, marehemu alifika Zanzibar kwa ajili ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Aprili 5, ambapo mchumba wake alimfanyia tukio la kumposa wakati wa safari hiyo, tukio lililoelezwa kuwa la furaha kabla ya kifo chake kutokea.