‘Hausigeli’ aliyejaribu kuua mtoto wa tajiri yake atupwa jela miaka 15

Dar es Salaam. Ni moja ya matukio yaliyotikisa Jiji la Dar es Salaam, mfanyakazi wa ndani (house girl), Clemensia Milembe alipojaribu kusababisha kifo cha mtoto wa tajiri yake, Maliki Kitumbi (6), kwa kumkata koromeo kwa kutumia kisu.

Kutokana na ushahidi mzito wa upande wa mashtaka, ukiwamo wa uchunguzi wa kisayansi wa vinasaba (DNA), Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, alimhukumu msichana huyo kifungo cha miaka 15 jela.

Milembe na Elizabeth Makori walishtakiwa kwa kosa la kujaribu kuua, kinyume na kifungu 211 (a) cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code), lakini alimwachia huru Elizabeth baada ya kuthibitisha hakushiriki kwa namna yoyote kutenda kosa hilo.

Katika shauri hilo, ambalo hukumu yake ilitolewa Aprili 10, 2026 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama leo Aprili 13, Jamhuri iliwakilishwa na wakili wa Serikali Caroline Asenga, wakati utetezi ulikuwa mawakili Leonard Mburi na Sadick Muhimbi.

Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, tukio hilo lilitokea Julai 15, 2024 katika eneo la Goba Kinzudi, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambapo mshtakiwa alijaribu kusababisha kifo cha mtoto Maliki.

Milembe alikuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba aliyokuwa akiishi Maliki, na wajibu wake wa msingi ulikuwa kumwangalia Maliki, kwa kuwa wazazi wa mtoto huyo walikuwa wakienda kazini mapema asubuhi na kurudi jioni.

Jaji alisema hakuna ubishi kuwa mshtakiwa na waajiri wake hawakuwa na ugomvi, na hivyo walikuwa wakiishi kwa amani na utulivu katika nyumba hiyo.

Julai 15, 2024, mtoto Maliki Hashim, aliyekuwa shahidi namba 4 katika kesi hiyo, alirejea nyumbani kutoka shule na kumkuta mshtakiwa nyumbani na alimwogesha kama ilivyokuwa utaratibu kila mtoto anapotoka shule.

Baadaye, katika hali isiyo ya kawaida na ya kushangaza, mshtakiwa alichukua kisu na kuanza kumchinja mtoto huyo kwa kumkata shingoni na kusababisha avuje damu nyingi. Katikati ya kitendo hicho, mshtakiwa alihisi dhamiri mbaya.

“Hivyo alimwacha mvulana (mtoto) huyo, akatupa kisu chini na kukimbia,” alisema.

Mtoto Maliki alipopiga kelele kwa uchungu, majirani walikusanyika ili kuona kilichotokea, ndipo walimkuta akitokwa na damu nyingi. Wakati huo mama wa mtoto, Shani Charles, alikuwa mbali na nyumbani.

Wakati huo mama, aliyekuwa shahidi namba 1 kama alivyokuwa utaratibu wake, alikuwa katika Kituo cha Goba akifanya biashara yake ya ushonaji.

Baada ya kupigiwa simu na mmoja wa majirani, mama huyo alifika haraka eneo la tukio, na alimkuta mtoto wake akitokwa na damu nyingi, na akamkimbiza katika hospitali ya BNB iliyopo jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kutokana na majeraha mabaya aliyokuwa nayo mtoto, alipewa huduma ya kwanza na kupewa rufaa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo alipokelewa na kupewa huduma ya dharura.

Hospitalini hapo, pamoja na madaktari wengine, alihudumiwa na Dk Rashid Mwigamba, aliyekuwa shahidi namba 2, ambaye alimpa mwathirika msaada wa dharura na kumuunganisha na mashine ya kusaidia upumuaji (ventilator).

Hapo shahidi huyo alijitahidi kudhibiti damu iliyokuwa ikibubujika, na baada ya hali kuwa thabiti, alipelekwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), na baadaye kufanyiwa upasuaji.

Kulingana na ripoti yake, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa Maliki alikuwa na majeraha manne shingoni, na majeraha hayo yanaweza kusababisha ulemavu wa kudumu wa kupumua, kwani koromeo lilikuwa limekatwa kwa karibu asilimia 80.

Kisu kilichotumika kinapatikana

Wakati mtoto Maliki akipelekwa hospitalini, taarifa zilifikishwa Kituo cha Polisi Goba na shahidi wa nane, Abdalah Abdalah, ambapo shahidi wa saba ASP Yusuph Sembua na wa 12, Koplo Amri walifika eneo la tukio.

Wakiwa na shahidi namba nane, maofisa hao waliingia katika nyumba ya tukio na kupata kisu kilichokuwa na matone ya damu, wakafunga nyumba hiyo na kurudi Julai 16, 2024 kwa uchunguzi wa kina.

Katika awamu ya pili, makachero hao walipata sketi ya mshtakiwa ikiwa na matone ya damu na ilichukuliwa kama kielelezo P4, pamoja na sampuli za damu zilizokuwa ukutani.

Wakati huo, mshtakiwa alikuwa ametoroka kwenda kusikojulikana na alionekana baada ya siku saba, aliporudi mwenyewe kwa tajiri yake na kueleza kuwa alikuwa amejificha katika nyumba ambayo iliyokuwa haijakamilika.

Mshtakiwa alidai katika siku hizo hakula chakula chochote, na Julai 21, 2024 aliamua kurudi nyumbani kwa tajiri yake, na mama huyo kwa kushirikiana na majirani alimpeleka polisi.

Katika kumuunganisha na tukio hilo, shahidi wa 14, Inspekta Idd Ngotwike, alichukua sampuli za DNA kutoka kwa mshtakiwa pamoja na kielelezo P4 (blauzi na jaketi), na kuvipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakutenda kosa hilo, na alimtaja mshtakiwa wa pili, lakini kiukweli mwanamke huyo hakuwa amehusika kwa namna yoyote.

Jaji alinukuu maelezo hayo:“Nilimtaja tu Elizabeth, lakini hahusiki kabisa. Sijawahi kukutana na Elizabeth kabla ya siku alipokuja nyumbani kutafuta kuku wake. Sikuwa na nia ya kumkata Maliki. Nilijikuta tu nimeshika kisu. Nilikuwa nimepoteza fahamu nilipojaribu kumuua Maliki. Naomba mahakama inionee huruma.”

Elizabeth, aliyekuwa mshtakiwa wa pili, alishikilia msimamo kuwa hahusiki kwa namna yoyote na tuhuma hizo, na alishangaa kuhusishwa nazo.

Katika hukumu yake, Jaji Mbagwa alisema ili kuthibitisha kosa la kujaribu kuua, Jamhuri ina wajibu wa kuthibitisha uwepo wa dhamira ya kutenda kosa, na kwamba mshtakiwa alitekeleza dhamira hiyo.

“Hakuna ubishi kuwa kuna ushahidi mzito unaomuunganisha mshtakiwa (Clemensia) na tukio hili. Kuna ushahidi wa moja kwa moja kutoka kwa mwathiriwa mwenyewe, Maliki, aliyekuwa shahidi namba 4.

“Maliki aliiambia mahakama kuwa ni mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyemfanyia ukatili kwa kumkata koromeo. Mahakama ilipata nafasi ya kumwangalia Maliki na majeraha yake,” aliongeza.

“Zaidi, mshtakiwa alikiri mbele ya shahidi namba 16 kupitia kielelezo P12. Matokeo ya uchunguzi wa kisayansi pia yalimhusisha mshtakiwa na dhamira ya kuua,” alisema.

“Nia yake mbaya ilidhihirishwa na kitendo cha kumkata mtoto shingoni sehemu nyeti,” alisisitiza Jaji.

“Kiwango cha majeraha kilichoelezwa na Dk Mwigamba kinaonesha kwamba kama si matibabu ya haraka, mwathirika angefariki,” alisema.

Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji aliridhika kuwa shtaka limethibitishwa bila kuacha mashaka, na kumtia hatiani mshtakiwa.

Jaji alisema kwa mujibu wa kifungu 211(a) cha Kanuni ya Adhabu, adhabu ya juu ni kifungo cha maisha jela, lakini kutokana na maelezo ya kujutia kosa, alimhukumu miaka 15 jela.