UNAWEZA kusema hii ni kama sinema katika sakata la mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah na klabu hiyo hadi kufikia sasa ambapo uamuzi umetoka rasmi.
Sowah ambaye alitua Simba Agosti 2025 kipindi cha usajili wa dirisha kubwa akitokea Singida Black Stars, ishu yake ndani ya klabu hiyo kwa kile kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu, imegeuka kama sinema tangu mwanzo ilivyoanza.
Awali zilitoka taarifa za Sowah kusimamishwa na klabu hiyo Februari 25, 2026 wakati kikosi hicho kikiwa Dodoma kinajiandaa kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji.
Katika kusimamishwa huko, Sowah alikuwa akituhumiwa kwa utovu wa nidhamu na kabla ya kusimamishwa na klabu, tayari alikuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi tano aliyopewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kikao chake cha Desemba 15, 2025. Adhabu hiyo ilimalizika Februari 25, 2026.
Mwanaspoti limewahi kuripoti, wakati Sowah akisimamishwa, alitakiwa kutoa maelezo mbele ya Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo jambo ambalo alilifanya.
Kabla ya kufahamika nini kilijadiliwa na kamati hiyo kutokana na maelezo ambayo Sowah aliyawasilisha kama alivyotakiwa, Mwanaspoti likapenyezewa mshambuliaji huyo raia wa Ghana anadaiwa kuandika barua ya kuvunja mkataba na alipotafutwa mwenyewe kipindi hicho, hakupatikana, huku kiongozi mmoja wa Simba akiomba apewe muda kidogo wa kufuatilia kabla ya kulizungumzia.
Hata hivyo, Aprili 14, 2026 ikiwa imepita takribani mwezi mmoja na siku 20 tangu zilipotoka taarifa za kusimamishwa Sowah na klabu hiyo, uongozi wa Simba umeibuka na kutangaza kumpeleka kufanya mazoezi na kikosi chao cha vijana chini ya miaka 20 kinachonolewa na gwiji wao, John Bocco.
Simba imebainisha uamuzi huo umetokana na uongozi wa klabu hiyo kumpa Sowah adhabu mbili kutokana na utovu wa nidhamu na kumpeleka timu ya vijana ni sehemu ya matazamio.
Kwa sasa Bocco anayemiliki leseni B ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), amekabidhiwa programu nzima ya maendeleo ya vijana katika klabu hiyo huku akitambulisha kuchukua majukumu hayo Desemba 26, 2025.
Akizungumzia uamuzi wa kumpeleka Sowah kufanya mazoezi na timu yao ya vijana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Ni kweli Jonathan Sowah tulimsimamisha kutoka kwenye kambi yetu. Mwezi wa tatu tulisafiri kwenda Dodoma kucheza na Dodoma Jiji. Tukiwa pale tukiwa na Sowah akaamrishwa atoke kambini na kurejea Dar es Salaam.
“Sowah alikuwa akituhumiwa kwa makosa kadha wa kadha ya utovu wa nidhamu ambayo ni malalamiko yaliyokuja kutoka kwenye benchi la ufundi. Baada ya pale akarejeshwa kutoka Dodoma akarejea Dar es Salaam kusubiri taratibu za klabu ziweze kukamilika na hatimaye haki yake iweze kupatikana.
“Baada ya pale akawa amepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya Simba Sports Club ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake, Kamanda Kova (Suleiman), Sowah akaitwa mbele ya kamati akasomewa mashtaka yake yote yanayomkabili na yapo ambayo amekiri na mengine akatoa maelezo na baada ya pale kamati ikajiridhisha mchezaji huyu ana makosa ya utovu wa nidhamu. Baada ya kujiridhisha huko akapewa adhabu.
“Adhabu ya kwanza ni faini na adhabu ya pili ameamrishwa aende akafanye mazoezi na timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Adhabu hii inaanza mara moja kuanzia hivi sasa na atakuwa akifanya mazoezi na timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ikiwa ni kipindi cha matazamio kumwangalia kama kutakuwa kuna mabadiliko yoyote ndani yake kwenye upande wa nidhamu basi adhabu yake hiyo itaisha na atarejea timu kubwa kwenda kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
“Kwa hiyo huo ndio mustakabali wa Sowah na Simba Sports Club ya kwamba yupo kwenye kuitumikia adhabu yake aliyopewa ambayo ni kufanya mazoezi na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ikiwa ni kipindi cha matazamio.”
Februari 25, 2026 wakati Simba ikiwa Dodoma siku hiyo ikijiandaa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, zilitoka taarifa za Sowah kurudishwa Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa ni kuhitajika na Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili za utovu wa nidhamu.
Miongoni mwa kile kilichoelezwa anachotuhumiwa nacho Sowah hadi kufikia hatua ya kusimamishwa ni kuchelewa mazoezini huku akitakiwa kutoa maelezo ya kina, jambo ambalo alilifanya mbele ya kamati hiyo. Hata hivyo, siku chache mbele baada ya kujieleza, ziliibuka taarifa za mshambuliaji huyo raia wa Ghana kuandika barua ya kuvunja mkataba na Simba.
Mapema jana akizungumza na Kituo cha Redio cha Crown FM, Sowah alivunja ukimya na kuamua kuweka wazi kile kinachoendelea ndani ya klabu hiyo kumhusu yeye ikiwa umepita takribani mwezi mmoja na siku 20 tangu asimamishwe klabuni hapo. Sowah aliyetua Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu akitokea Singida Black Stars, alisema kwa sasa yupo Dar es Salaam, lakini hafanyi mazoezi na kikosi cha Simba.
“Ni nini ninachoweza kusema kuhusu utovu wa nidhamu?” Sowah alianza kwa kugusia utovu wa nidhamu anaotuhumiwa nao.
“Unajua, binadamu tuna aina mbili au tuna aina tofauti za binadamu tulionao katika ulimwengu huu. Natumai unajua hilo. Hivyo hata wewe unayeniuliza una upande wako mzuri na una upande wako mbaya.
“Ikiwa mimi unaweza kusema ni mtaalamu, nikiwa mtaalamu, sina upande wangu mzuri, sina upande wangu mbaya? Moja kwa moja mimi ni binadamu, hivyo nitakuwa na mazuri na mabaya, sawa?
“Ikiwa nina mazuri na nina mabaya, je, umejiuliza ulinitendea nini ili mimi nibadilike na kuelekea upande wangu mbaya? Hivyo tunakubaliana kwamba inaweza kuwa kuna jambo fulani karibu nawe.”
Sowah aliendelea kwa kusema: “Watu hawataniwahi kunipata nikiwa huko nje na uniambie huyu hana nidhamu. Hapana. Wakati wowote utakaonipata kusema sina nidhamu ni uwanjani. Ndiyo maana nakuambia tuna aina mbili za binadamu; una upande wako mzuri na upande wako mbaya. Ninapocheza mpira na nikipoteza, nakasirika sana. Unanielewa?
“Wakati sifungi bao, nakasirika kwa sababu lengo langu ni kufunga bao, hivyo ikiwa sipati bao hilo, nahitaji kutafuta njia na namna ambayo inaweza kupata bao hilo; iwe nitapata bao na kupata kadi nyekundu, au nitapata bao na kupata kadi ya njano, sijali. Lengo langu ni kupata bao, ninataka kila wakati timu yangu iwe ya kwanza, huyo ndiye mimi.
“Mimi si mtu mchoyo, hivyo kila wakati watu walizoea kuona akiwa uwanjani hana heshima. Ndiyo, ni uwanjani tu ambapo unaweza kunipata. Watazame watu kama Balotelli (Mario), watazame watu kama Diego Costa… Watazame watu hawa leo wako wapi?”
Sowah ambaye huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Simba akiwa amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu Bara, hakuishia hapo, ameendelea kwa kusema hajui ni nani anasambaza taarifa za kwamba yeye ni mtovu wa nidhamu.
“Kuhusu hilo, sijui kitu chochote, sijui kitu chochote. Sijui nani aliyeleta hizo habari. Unaelewa? Sijui kitu chochote kwa hiyo sitaki tu kulizungumzia.
“Kuhusu Simba, siwezi kuizungumzia Simba sasa hivi. Siwezi kuzungumza chochote kuhusu Simba.”
Nyota huyo ambaye msimu uliopita akiwa Singida Black Stars akicheza mechi 14 za Ligi Kuu Bara kwa takribani miezi sita akitua dirisha dogo na kufunga mabao 13, alisema: “Bado niko kwenye klabu (Simba). Nazungumza na wewe. Bado niko Tanzania.”
Kuhusu kuhudhuria kamati ya nidhamu na kilichojiri, Sowah alijibu kwamba alienda akisema: “Ndiyo, nilienda kule. Hicho ndicho ninachosema. Sitaki kuwazungumzia sasa hivi. Sitaki kuzungumza chochote kuhusu klabu kwa sasa.
“Mkataba wangu bado unafanya kazi. Kwa hiyo mimi ni mchezaji wa Simba. Sitaki tu kusema chochote kuhusu wao. Namaanisha bado niko Dar es Salaam.”
Alipoulizwa ishu za kuhudhuria mazoezi, alisema: “Hapana, hapana, hapana, hapana.”
Hata hivyo, Sowah amewatoa wasiwasi mashabiki wake akisema: “Hawapaswi kuwa na wasiwasi. Ndiyo maana wakati mwingine nahitaji kuja kwenye vyombo vya habari ili angalau nionekane kwao, nizungumze nao mara moja moja. Hapana, wasiwe na wasiwasi. Kila kitu kitakuwa sawa. Ninachoweza kusema ni kwamba nahitaji maombi yao na wanikumbuke kwenye maombi. Hivyo tu.”
Mshambuliaji huyo tangu Desemba 7, 2025 wakati Simba inafungwa 2-0 dhidi ya Azam, hajacheza mechi ya Ligi Kuu Bara hadi sasa wakati kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kikishuka dimbani mara 12.
Mbali na Ligi Kuu Bara, Sowah mara ya mwisho kucheza ndani ya Simba ilikuwa Februari 14, 2026 katika mechi ya kuhitimisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kushinda bao 1-0 dhidi ya Stade Malien. Katika mechi hiyo, Sowah aliingia dakika ya 84 kuchukua nafasi ya Seleman Mwalimu, hivyo akatumika kwa dakika sita pekee. Tangu hapo, amekosa mechi 12 mfululizo zikiwemo tatu za Kombe la Shirikisho la CRDB na tisa Ligi Kuu Bara.
Msimu huu, akiwa na mabao matatu Ligi Kuu Bara aliyofunga dhidi ya Fountain Gate (1) na Mbeya City (2), amecheza mechi nne dhidi ya Fountain Gate (dk 90), JKT Tanzania (dk 30), Mbeya City (dk 60) na Azam (dk 6).