Dodoma Jiji yafunika vigogo Bara

WAKATI Dodoma Jiji ikiwa ugenini Jumatano hii kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kucheza dhidi wenyeji wao, Coastal Union, Walima Zabibu hao ndio timu yenye kiwango bora zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara huku ikizizidi kete vigogo Simba, Yanga, Singida Black Stars na Azam kwa mujibu wa takwimu.

Takwimu za mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Bara msimu huu, zinaonyesha Dodoma Jiji ndiyo timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi kuliko vigogo hao, licha ya kupoteza mechi moja dhidi ya Azam kwa mabao 3-0, timu hiyo ya Jiji imevuna pointi 10, moja zaidi ya Simba, Yanga na Singida Black Stars zenye pointi tisa kila moja.

Simba imevuna pointi tisa kutokana na ushindi wa mechi mbili dhidi ya TRA United (3-0) na Coastal Union (2-0) huku ikitoa sare tatu dhidi ya TRA (0-0) katika mechi ya mzunguko wa pili, Pamba Jiji (1-1) na Azam (0-0).

Kama ilivyo kwa Simba, Yanga nayo imetoa sare tatu dhidi ya Azam (0-0), TRA United (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1) huku ikishinda mbili dhidi ya Tanzania Prisons (3-0) na Pamba Jiji (3-0).

Singida Black Stars imechapwa mechi mbili dhidi ya Azam (2-1) na TRA United (2-0), imeshinda tatu dhidi ya Mbeya City (4-1), Tanzania Prisons (2-1) na KMC (1-0). Azam yenyewe imeshinda mechi moja dhidi ya Singida Black Stars na kutoa sare nne dhidi ya Yanga, Mashujaa, Simba na Mbeya City, katika mechi hizo imefunga mabao mawili.

Coastal Union ambayo itakuwa mwenyeji wa Dodoma Jiji, katika mechi tano zilizopita imeshinda moja dhidi ya Tanzania Prisons kwa mabao 4-1, imetoa sare dhidi ya JKT Tanzania (1-1) na Mtibwa Sugar (1-1), imechapwa dhidi ya Singida BS na Simba.

Katika mechi hizo tano, Dodoma Jiji imeshinda tatu dhidi ya KMC (2-1), TRA United (3-0) na Fountain Gate (3-0) huku ikitoa sare moja dhidi ya Simba (0-0). Wababe hao wa kanda ya kati, ni wababe pia kwa kufunga mabao mengi, wamefunga manane sawa na Singida Black Stars, wameruhusu manne.

Takwimu zinaonyesha nyuma na Dodoma Jiji na Singida Black Stars, Yanga inafuata ikiwa na mabao saba ya kufunga huku Simba ikiwa na sita katika michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa timu zilizoruhusu mabao machache zaidi katika mechi hizo ni Yanga, Simba na Azam ambao kila mmoja ameruhusu bao moja.

Dodoma Jiji itakapokuwa ugenini dhidi ya Coastal Union, inazikutanisha timu hizo ambazo duru la kwanza matokeo yalikuwa mazuri kwa wageni wakishinda 2-0.

Katika msimamo wa ligi, Dodoma Jiji imekusanya pointi 24, ikishika nafasi ya nane, wakati Coastal Union ni ya 13 na pointi 16, zote zikicheza mechi 18.