BAADA ya kukabidhiwa majukumu ya kuiongoza Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ na benchi lake la ufundi wanatarajia kuanza mtihani wao Jumatano hii watakapoikabili Simba katika mchezo wa Ligi Kuu.
Minziro na msaidizi wake, Mathias Wandiba walitambulishwa Aprili 10, 2026 kikosini humo kuiongoza timu hiyo kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Mohamed Ismail ‘Laizer’.
Kocha huyo mwenye uzoefu, rekodi na historia zake kwenye soka juzi akiwa jukwaani aliishuhudia Fountain Gate ikichezea kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Azam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora, huku Simba ikitakata kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Fountain Gate inatarajia kuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujiweka nafasi nzuri.
Hadi sasa, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba ipo nafasi ya pili kwa pointi 36, ikiachwa pointi nane na watani zao Yanga waliopo kileleni, huku Founatin Gate inakamata nafasi ya 14 kwa pointi 16 baada ya zote kucheza mechi 17.
Minziro alitua kikosini humo akitokea Bigman FC ya Ligi ya Championship, huku akiwa tayari ameshazifundisha timu kadhaa kwa mafanikio ikiwemo KMC, Geita Gold na Singida Big Stars alizozipandisha Ligi Kuu, huku Mbao FC akiitumikia nusu msimu kabla ya kushuka nayo daraja.
Meneja wa Fountain Gate, Elias Zamkufo, ameliambia Mwanaspoti kuwa, wanafahamu mchezo huo kuwa mgumu, lakini kwa uzoefu wa benchi la ufundi wanaamini timu hiyo itashinda na kujinasua nafasi za chini.
Alisema wachezaji wote wako fiti na waliokuwa majeruhi Daniel Joram na Ibrahim Parapanda wamerejea, huku akitoa tahadhari kwa nyota wa kikosi chao kuwa makini na wapinzani kwa kudhibiti mchezaji mmoja mmoja.
“Tunajua Simba ni timu kubwa na ukifanya makosa wanakuadhibu, hatupaswi kumdhibiti mchezaji mmoja bali kuwakabili wote, tunashukuru Kocha wetu anao uzoefu na ushindani kwenye soka.
“Mbinu zake zinaweza kutupa kitu, kimsingi tuko tayari kwa ajili ya mchezo huo ili kupata pointi tatu ambazo zitatupandisha nafasi nzuri kwenye msimamo, mashabiki waje kwa wingi kutusapoti,” alisema meneja huyo.
Kocha msaidizi wa Fountain Gate, Mathias Wandiba alisema wanaenda kwa tahadhari na kuwaheshimu wapinzani na wanafahamu mechi haitakuwa rahisi.
“Hatujaweka ufundi mwingi kwakuwa ni muda mfupi lakini zaidi tumewaandaa kisaikolojia wachezaji wakapambane uwanjani, dhamira yetu ni timu ishinde ili tujinasue huko chini na tusishuke daraja,” alisema Wandiba.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, alisema: “Tumewaandaa wachezaji vizuri kimwili na kimbinu, mechi iliyopita tulionesha hali ya kusaka ushindi na jambo la faida ni kuendelea kupata matokeo mazuri mfululizo.
Simba inaingia kwenye mechi hii ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 3-0 duru la kwanza dhidi ya Fountain Gate, huku pia ikitoka kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
