NYOTA wa kikapu, Abdul Kakwaya amesema kwa sasa anasikilizia timu itakayohitaji huduma yake huku akiendelea kujifua kwa ajili ya ligi ya DBL.
Kakwaya ambaye ni nyota wa zamani wa Vijana ‘City Bulls’, amesema kwa sasa anajifua na DB Oratory pamoja na kufanya mazoezi binafsi kila siku ili kujiweka fiti.
Amesema amekuwa akifanya mazoezi ya kukimbia barabarani kila siku asubuhi, eneo la Kigamboni na jioni anafanya pamoja na DB Oratory kwenye Uwanja wa Donbosco Oyster bay.
Kuhusu usajili amesema hadi sasa ameshashawishiwa na baadhi ya timu na wakati ukifika atatangaza timu atakayojiunga nayo mwaka huu.
“Timu tano zimekuwa zikinishawishi nisajili, naamini nitatangaza nitakayochezea hivi karibuni,” amesema Kakwaya na kuongeza amejipanga kufanya makubwa katika ligi hiyo mwaka huu.
Wakati huo huo, Kamishina wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Shabani Mahobonya amesema ligi hiyo inatarajiwa kuanza Mei 1 kwa mzunguko mmoja, itakayoshirikisha timu 32, huku 16 zikiwa ni za wanaume na 16 za wanawake.
Kwa upande wa wanaume ni Dar City (bingwa mtetezi), JKT, Stein Warriors, ABC,UDSM Outsiders, DB Oratory, Srelio, Vijana “City Bulls”, Savio na Mchenga BC.
Nyingine ni Chui, Mlimani BC, Kurasini Heat, Ukonga Kings, Magone na Pazi.
Upande wanawake ni Jeshi Stars, JKT Stars, Polisi Stars, Vijana Queens, DB Troncatti, Ukonga Queens, Tausi Royals, Pazi Queens na DB Lioness (bingwa mtetezi).
Nyingine ni Twalipo Queens, Real Dream, Kigamboni Queens, Kurasini Divas, City Queens, Mgulani Stars na UDSM Queens.
