Wavalia njuga umri wa kuolewa mwanamke usianzie chini ya miaka 18

Dar es Salaam. Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), imedhamiria kuhakikisha sheria ya ndoa inabadilika na kuondoa umri wa kuolewa kwa mwanamke kuwa chini ya miaka 18.

Ikumbukwe, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inaruhusu mvulana kuoa kuanzia umri wa miaka 18, na msichana kuolewa kuanzia miaka 14 na miaka 15 kwa kibali cha wazazi, ambapo wadau wamekuwa wakipigia kelele sheria hiyo wakisema inamnyima mtoto wa kike haki zake za msingi hasa ya kupata elimu.

Akizungumza jana Aprili 13,2026 jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa mtandao huo, Mratibu wa programu ya  tathimini na ufuatiliaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ambalo ni sekretarieti ya Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, Irene Ernest amesema wamekuwa wakikutana na wizara za Serikali ili kushirikiana kwenye mchakato mzima wa kubadilisha sheria hiyo.

“Tunafanya uchechemuzi wa kisera kuhakikisha sheria ya ndoa inabadilika na mtoto haolewi chini ya miaka 18, pia tunashirikiana na mitandao mingine kuhakikisha urudishaji wa watoto shuleni unakuwa wenye tija,” amesema.

Irene amesema wanapanga mikakati na taasisi na wizara mbalimbali kama ya Katiba na Sheria, Maendeleo ya Jamii na Elimu kuona namna ya kubadilisha sheria hiyo.

“Mipango ni kuona watoto wanafanikiwa kumaliza elimu zao bila ya kulazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo, tunashirikiana na mitandao mbalimbali viongozi wa kidini na mila kuhakikisha sheria inabadilika,” amesema.

Akifafanua zaidi Irene amesema kwa sasa Serikali ikishirikiana na mtandao, viongozi wa kidini, mila na wadau wengine inapanga mkakati wa kukusanya taarifa na maoni ya kukubali au kupinga mabadiliko ya sheria hiyo.

“Kuhusu suala la mimba shuleni ni kikwazo kwa kuwa inakiuka haki za binadamu tunataka pia kiuhalisia kumaliza hili tatizo ili watoto wasome,” amesema huku akipigilia msumari suala la elimu ya afya ya uzazi ili watoto wajitambue.

Mkurugenzi Shirika la Teens Corridor, Sophia Nshushi amesema mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ndipo wanapofanyia kazi bado kuna ndoa za utotoni huku akitaja sababu moja wapo ni umaskini.

Amesema kwa sasa kama mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni wanatoa elimu shuleni, kwenye jamii kuonyesha madhara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, Tike Mwambipile, amesema wamekuwa wakifanyia kazi eneo la mtoto wa kike haolewi akiwa umri chini ya miaka 18

Kuhusu kupandisha umri wa miaka 18 amesema wanatamani kuona mabadiliko hayo na kama wanawake wanasheria bado wanahitajika kufanya uchechemuzi ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuzuia ndoa za namna hiyo zisifanyike.