Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameutembelea mradi wa Mji wa AFCON Fumba uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 14 Aprili 2026, akiambatana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Riziki Pembe Juma, pamoja na wadau wa mradi wa AFCON Fumba Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amekagua maeneo mbalimbali ya uwanja huo wa kisasa wa AFCON unaojengwa na kampuni ya ORKUN GROUP ya Uturuki, unaotarajiwa kutumika kwa michuano ya AFCON mwaka 2027 itakayofanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea na kukagua miundombinu inayotarajiwa kujengwa kuzunguka uwanja huo, ikiwemo hospitali, barabara, migahawa, maduka makubwa (mall) pamoja na huduma nyingine muhimu zitakazouzunguka mji huo wa kisasa.
Uwanja huo unakadiriwa kuchukua watazamaji elfu 35, ukiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).





.jpeg)
