Trump Aondoa Picha ya AI Iliyoonyesha Akiwa Kama Yesu Kwenye Mtandao Wake wa Kijamii

Global Publishers
April 14, 2026
0 Comments

Rais wa Donald Trump ameondoa picha ya akili mnemba (AI) aliyoiweka kwenye mtandao wake wa kijamii baada ya kukosolewa vikali na baadhi ya wafuasi wake pamoja na viongozi wa kidini.

Picha hiyo, iliyochapishwa usiku wa Jumapili, ilimuonyesha Trump katika taswira inayofanana na sura ya Yesu Kristo, jambo lililozua mjadala mkubwa mtandaoni na ndani ya duru za kisiasa na kidini.

Baadaye, Trump alikiri kuichapisha picha hiyo lakini akadai alidhani ilikuwa inamuonyesha kama daktari anayefanya kazi ya kusaidia watu, akiihusisha pia na taswira ya mfanyakazi wa Msalaba Mwekundu.

“Tulidhani ni picha yangu kama daktari,” alisema Trump alipoulizwa kuhusu tukio hilo, akisisitiza kuwa hakukuwa na nia ya kuudhi au kutoa tafsiri nyingine.

Hata hivyo, hatua hiyo ilizua upinzani kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake wa kihafidhina, ambao waliikosoa kama isiyo na heshima na yenye utata wa kidini. Baadhi walimtaka aombe radhi na kuondoa picha hiyo mara moja.

Tukio hili lilitokea wakati ambapo Donald Trump pia alikuwa ameingia kwenye mjadala mkali na Pope Leo XIV, ambaye amekuwa akitoa wito wa kumaliza vita na kuhimiza amani, hususan kuhusu mvutano unaohusisha Iran.

Katika majibu yake, Trump alikataa kuomba radhi, akisema hana sababu ya kufanya hivyo na akimkosoa papa kwa msimamo wake kuhusu sera za Marekani na vita vinavyoendelea.

Kwa mujibu wa taarifa, huu si mara ya kwanza kwa mtandao wa Trump kuondoa maudhui yenye utata, baada ya tukio la awali lililohusisha video iliyozua mjadala mkubwa na kusababisha kuondolewa kwake.

Tukio hilo linaendelea kuchochea mjadala kuhusu matumizi ya AI, siasa, na mipaka ya uhuru wa kujieleza katika mitandao ya kijamii.