Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kondoa Bernardin Mfumbusa afariki dunia

Dodoma. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetangaza  kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Bernardin Francis Mfumbusa, kilichotokea Aprili 14, 2026 majira ya saa 11:45 asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya dharura.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango ya mazishi inaendelea kufanyika ambapo marehemu anatarajiwa kuzikwa Aprili 22, 2026 katika Jimbo Katoliki Kondoa.

Askofu Mfumbusa alizaliwa Aprili 1, 1962 mjini Kondoa na kupadrishwa Juni 14, 1992. Baadaye aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Kondoa Machi 12, 2011 na kuwekwa wakfu Mei 15, 2011. Katika maisha yake ya utumishi, alilitumikia Kanisa kwa miaka 33 kama Padre na miaka 14 kama Askofu.

Mbali na majukumu yake ya kichungaji, marehemu alitambulika kama gwiji wa mawasiliano ndani ya kanisa. Aprili 9, 2026, Baba Mtakatifu Pope Leo XIV alimteua kuwa Rais wa kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (CEPACS) na pia mjumbe wa baraza la kipapa la mawasiliano ya jamii.

“Kanisa limempoteza Askofu na mtaalam mbobezi wa Mawasiliano ya Jamii,” imesema sehemu ya taarifa ya TEC na kuongeza kuwa,

“Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote,” imeongeza taarifa hiyo ikiwahimiza waamini kuendelea kuwa na imani na matumaini katika Kristo.