Kigwangalla asimulia maisha yalivyo bila cheo

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema tofauti kati ya kuwa na mamlaka na kukosa ni kubwa, akieleza kuwa pamoja na nguvu, fursa, heshima na mtandao mpana wa marafiki vinavyokuja na cheo, hali hubadilika mara tu mamlaka yanapoondoka.

Amesimulia kuwa katika maisha yake ya sasa bila kuwa waziri wala mbunge, hata baadhi ya watu aliowaona wa karibu wamepotea, huku huduma alizokuwa akizipata kwa urahisi hapo awali sasa zikihusisha urasimu na wakati mwingine wahusika kutopokea simu wala kujibu baruapepe.

Dk Kigwangalla, aliyekuwa Mbunge wa Nzega Vijijini kwa miaka 15, Naibu Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema mabadiliko hayo ya maisha ndilo jambo gumu zaidi kulizoea unapoishi ukiwa raia wa kawaida, baada ya kupoteza vyeo.

Kwa upande mwingine, amesema maisha bila cheo yamempa nafasi ya kufanya shughuli zake binafsi zikiwemo biashara kupitia kampuni yake ya HK Group, pia kuwa karibu na familia.

Mwanasiasa huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ubunge wake ulikoma mwaka 2025. Hata alipowania tena nafasi hiyo, alianguka katika mchakato wa kura za maoni akipata kura 1,715 dhidi ya Neto Kapalata aliyepata kura 2,570 na kuteuliwa na chama hicho kugombea Nzega Vijijini.

Kwa upande wa uwaziri, ulikoma Juni mwaka 2020, baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu akiwa Maliasili na Utalii Tangu Oktoba 7, 2017 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli.

Dk Kigwangalla, amesimulia hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo, amesema alipokuwa na vyeo, kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata, kumbe wote walikuwa marafiki wa waziri, si wa Dk Kigwangala.

“Ukiwa na vyeo, kila jambo ukitaka unatoa maelekezo linafanyika haraka. Kila ofisi utakayopiga hodi kuomba jambo lako utapewa mara moja,” amesema.

Lakini baada ya kutoka kwenye nafasi hizo, amesema kuna watu alioamini walikuwa marafiki zake, walipendana na kushirikiana, lakini wengi wakatoweka.

“Wanakuona wewe tena huna cha kuchangia, yaani wewe tena si mbia kwa hivyo wanakukwepa, wanakukimbia wengine wanahisi labda utawaombaomba hela au fursa na wao hawatapata chochote kwako,” amesema.

Katika nyakati kama hizo, amesema watu wanakuepuka na hilo linasababisha ugumu kiasi.

“Nilipokuwa mfanyabiashara kabla sijawa kwenye siasa nilikuwa napata mikopo benki kirahisi sana kwa sababu tu ya kutimiza vigezo. Baada ya kutoka kwenye uwaziri na baada ya kutoka kwenye ubunge, sasa hiyo haipatikani tena yaani hata ile ya mwanzo ile ya zamani kabla sijawa na cheo chochote hairudi tena,” amesema.

Hiyo inatokana na watu kukutazama kwa jicho tofauti na walivyokutazama awali ulipokuwa na vyeo vya ubunge na uwaziri.

“Ukipiga simu ukiwa waziri, utajibiwa mheshimiwa mtume kijana alete nyaraka, tayari utasikia mkopo umetoka fedha zimeingia kwenye akaunti. Ukitoka ukibaki kuwa mbunge kuna kaheshima fulani kanapungua lakini angalau wanajua bado mheshimiwa wakati wowote unaweza ukateuliwa.

“Ukitoka kabisa kwenye ubunge hata simu hawapokei, baruapepe hazijibiwi naiona hiyo lakini ndio maisha yalivyo,” amesema.

Amesema unachotakiwa kujua ni kwamba hakuna kinachodumu kwenye maisha, kila kitu kitapita,kama kilikuwa na mwanzo basi kitafika mwisho.

Nafuu kwa familia, maisha binafsi

Dk Kigwangalla amesema kutokuwa na vyeo kumempa muda kukaa na familia, kufanya mambo yake binafsi na kujitathmini.

“Nilikuwa na vitu vingi ambavyo nilikuwa nafanya kabla sijaingia kwenye siasa na nilipoingia kwenye siasa vingi vilisimama vingine vilikufa, vingine viliharibika,” amesema.

Katika kipindi hicho, amesema amepata nafasi ya kufungua biashara zake na kuhusu siasa huenda siku zijazo.

Alivyopokea taarifa ya kutemwa

Katika mahojiano hayo, Dk Kigwangalla amesimulia alivyopokea taarifa ya kutokuwa sehemu ya wateule wa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli mwaka 2020, amesema alipokea hilo akiwa kwenye kikao binafsi.

“Nilikuwa nimetoka nyumbani kama saa 9:00 alasiri hivi nikamaliza kupiga lunch (chakula cha mchana) naenda kikao binafsi kwenye hoteli moja Dar es Salaam,” amesema.

Akiwa kikaoni, amesema mkeka wa wateule wapya ukatoka naye hakujua kwa kuwa walikuwa katika mazungumzo na wenzake kwenye kikao hicho.

“Niko nazungumza na mtu akatokea kijana mmoja alikuwa msaidizi wangu nilipokuwa Wizara ya Afya, akaingia na yeye hapo hotelini, alikaa kwenye meza nyingine akaniona akaja kuniamkia akaniambia ‘pole bosi’, nikamwambia pole nini?

“Akaniambia ‘hujasikia kumbe? samahani mkuu’. Nikamwambia nini? Akasema ‘naona wametangaza Baraza la Mawaziri jina lako halimo’. Alieleza moja kwa moja. Ikapita ganzi, ikapita shaaa… kwa sababu ghafla yaani,” amesema.

Amesema alipokea taarifa hizo kipindi ambacho alikuwa na imani angerudishwa kwenye wizara aliyoiongoza kwa kuwa kulikuwa na rekodi nzuri za utendaji wake na takwimu zilionyesha.

“Nilikuwa na rekodi nzuri kwenye Serikali, nilifanya kazi nzuri, sikuwa na kashfa yoyote umri bado mdogo, kwa hiyo nilikuwa naamini tu kwamba nitateuliwa tu, nitaendelea kufanya kazi mbona nimefanya kazi nzuri nikiziangalia takwimu.

“Mimi ni mwanasayansi kwa hiyo naangalia sana matokeo ya takwimu, kwa hiyo naangalia tulikuwa hapa tumetoka hapa tumekuja hapa na mimi ndio nilikuwa kiongozi, nilikuwa naamini tu nitateuliwa, si kwamba nilikuwa na uhakika, lakini nilikuwa naamini tu huenda nitateuliwa,” amesema msomi huyo wa Shahada ya Uzamivu ya Afya ya Jamii.

Ilivyotokea hakuteuliwa, amesema akakubaliana na matokeo na kuendelea na kikao chake na kilipoisha aliondoka. Akiwa njiani alipigiwa simu na mkewe kupewa pole kuhusu hilo.

“Mke wangu akaniambia nimeshawaambia watoto, nikamwambia sawa, nakuja na mimi. Bahati nzuri nilikuwa nishahama kutoka nyumba ya Serikali, nimekuja kwenye nyumba yangu binafsi kwa hiyo hakukuwa na ile hamahama ile,” amesema.

Hisia unapoteuliwa, kuachwa

Katika mahojiano hayo, Dk Kigwangalla amesema taarifa ya kuteuliwa inaleta hisia kwamba unathaminiwa, unakubaliwa kwa kawaida mteuliwa anajisikia vizuri.

Kwa upande wa kutenguliwa au kuachwa kwenye uteuzi, amesema kibinadamu kunaleta dhana kama vile umekataliwa, umeonekana hutoshi kwenye jukumu husika, hauna maarifa au umekosea.

Kutenguliwa kwa mujibu wa Dk Kigwangalla, kunaleta sintofahamu kidogo kwa kuwa mtu unadhani haukubaliki na hisia nyingine nyingi mchanganyiko.

Lakini kwake, amesema anaamini kila kilicho na mwanzo hakikosi mwisho, hivyo hata unapoteuliwa anaamini itafika siku utatenguliwa au kuachwa.

“Ukijua hivyo utajua tu kwamba cheo ni dhamana. Yaani cheo ni kama mkopo hivi. Unapewa ili ufanyie mambo fulani halafu baadaye urudishe,” amesema.

Katika mahojiano hayo, Kigwangalla amewashauri wenye vyeo kujifunza kuishi na nafasi walizonazo, kwa kutambua kwamba ni dhamana ya mpito na si mali yao, wakizivaa kama wanazimiliki zitawapa shida baada ya kuzikosa.

“Hautoweza kurudi kuishi na kufanya kazi zako kwa sababu utakuwa umenasa kwenye uraibu wa cheo. Anayekupa cheo leo, kama hivi vyeo vikubwa, ukae ukijua kuna siku yaani kitaondoka kwa tangazo moja tu, halafu hauambiwi kwa nini kimeondoka,” amesema.

Amesisitiza unapokuwa na cheo ni muhimu kujifunza kuithamini nafasi unayopewa, lakini usiizoee au kuifanya mali yako, ichukulie kama mkopo.

Alipoulizwa kuhusu ukimya wake wa takriban miezi sita baada ya kukosa ubunge, Dk Kigwangalla amesema baada ya kushindwa katika mchakato wa ndani wa CCM wa kuwania ubunge, aliamua kukaa kimya kutafakari nini kilitokea hadi kuanguka na namna ya kuanza maisha nje ya mfumo wa uongozi.

“Niliamua kutumia ukimya huo kujipanga upya, kuwa na familia na kusimamia miradi yangu ya kiuchumi,” amesema.

Alianza ubunge mwaka 2010 Jimbo la Nzenga kabla halijagawanywa kuwa Nzega Mjini na Vijijini; kutoka mikononi mwa Lucas Selelii aliyekuwa mbunge.

Kwenye mchakato wa ndani ya CCM uliozua mvutano kati ya Selelii na Hussein Bashe. Bashe alimmbwaga Selelii kwa kura 14,200 dhidi ya 2,700, lakini wote wawili hawakuteuliwa; badala yake CCM ikamteua Kigwangalla.

Baada ya Jimbo kugawanywa, Bashe alichukua Nzega Mjini Kigwangalla alihamia Nzega Vijijini hadi 2025.

Pamoja na kutoteuliwa katika mchakato wa ndani wa kuwania ubunge 2025, Dk Kigwangalla amesema hakuwahi kulalamika wala hana mtu wa kumlaumu na yuko sawa kwa kile kilichotokea.

“Safari ya uongozi ilikomea mwaka jana, lakini pia safari mpya inaanza. Kwa hivyo, sasa wakati naanza hii safari mpya nilihitaji kutafakari na kuona sasa naianzaje upya hii ngwe ya pili ya maisha yangu,” amesema.

Afafanua kuomba kazi mtandaoni

Katika mitandao ya kijamii, kulisambaa ujumbe ulioonyesha Dk Kigwangalla, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa LinkedIn ameomba kazi ya ujumbe wa bodi kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa.

Alipoulizwa iwapo aliiomba kazi hiyo, amesema hakuwa anaomba kazi, bali alikuwa anahuisha taarifa zake katika ukurasa wa mtandao huo na baadaye kukuta zimesambaa kama anaomba nafasi.

Amesema katika ukurasa huo, taarifa zilizokuwepo zilionyesha yeye ni waziri, nafasi ambayo kwa sasa hana. Alipozibadilisha na kuweka kwamba hayuko na shughuli, ndipo zile mpya zilipojichapisha.

“Mfano LinkedIn yangu ilikuwa inanionyesha mimi ni waziri wa Maliasili sijui ni mbunge wa Nzega Vijijini, kwa hivyo nilienda nikatoa ile, sasa moja kwa moja ikaonekana kwamba kuna sehemu unaulizwa sasa wewe umetoka kwenye kazi zote kwa hiyo saa hizi una kazi gani?

“Ikauliza ungependa upate kazi gani nikawa najibu. Kwa hiyo nilipojibu ikaleta tangazo la kuomba kazi. Sasa nilipoonekana naomba kazi mimi sikuwa na habari,” amesema.

Amesema alishangaa kuona taarifa imesambaa na kwa kuwa alikuwa mapumzikoni, akaamua kukaa kimya asijibu, kwani malengo yake ilikuwa kuhuisha taarifa na kuonyesha kwamba kwa sasa hana kazi ya umma au kitaifa.

Hata hivyo, amesema taarifa hiyo pamoja na kuchukuliwa vibaya na umma, kampuni nne zimemtafuta kumwomba awe mjumbe wa bodi.

“Mimi ni msomi wa uhakika, nina shahada nne ni msomi wa kimataifa, nina machapisho kadhaa na kitabu. Nimepita kwenye nafasi za uongozi wa kitaifa kama waziri, nimekaa bungeni miaka 15 nimekaa kwenye chama, unaachaje kunipa nafasi ya kuwa mjumbe wa bodi kwenye taasisi yako,” amesema.

Hata hivyo, amesema isionekane kuwa alikuwa anaomba kazi kwa sababu anayo nafasi ya kuzipata kazi hizo bila kutuma maombi hadharani.

“Ile ilikuwa tu ni mambo ya sarakasi za mitandao lakini Watanzania bwana, sijui wananipenda, wanapenda kuniamsha huko niliko ilikuwa nimejificha ili nije niongee ama ni nini, yaani wakageuza kakitu fulani kadogo sana kikawa kikubwa,” amesema.

Amesema kuna marafiki zake waliomtafuta kumuuliza iwapo yupo katika hali ngumu kiasi cha kuomba kazi, lakini si hivyo.

Katika mahojiano hayo, Dk Kigwangalla amesema kwa sasa amejikita na shughuli zake binafsi za kibiashara kupitia kampuni yake ya HK Group, ambayo ndani yake kuna kampuni tanzu za kilimo, uchambuaji wa zao la pamba, ufugaji, utalii na taasisi za elimu.

Ameeleza kampuni hiyo ni mwamvuli ambao ndani yake kuna kampuni nyingine ndogondogo zinazosimamia shughuli hizo anazozifanya katika mikoa mbalimbali nchini.

“Tutakuwa tuna mabucha kwa hiyo tunatoa nyama kwenye shamba letu tunaleta, tunatoa mchele tunaleta, tunauza, tunakusanya maharage, choroko, dengu tunaleta, tunauza,” amesema.