UCHAMBUZI WA MALOTO: Kiapo cha Trump Iran kinavyochokonoa vita na China

Cuban Missile Crisis, au kwa Kiswahili “Mgogoro wa Makombora Cuba”, ni siku 13 tete, zilizokaribia kubadili zama za vita baridi hadi kuwa vita kamili ya nyuklia. Ni kuanzia Oktoba 16 mpaka 28, 1962. Rais wa Marekani alikuwa John Kennedy.

“October Crisis in Cuba” na “Caribbean Crisis”, ni majina mengine ya mgogoro huo. Marekani na Dola ya Sovieti (USSR), zilikaribia kuchapana. Chanzo chake kinatengeneza taswira ambayo dunia ipo nayo kwa sasa. Ni kiapo cha Marekani kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz na bandari za Iran kijeshi.

Makombora ya nyuklia ya Thor (PGM-17 Thor) ni ya kwanza ya balistiki ya masafa ya kati (IRBM), yaliyotengenezwa na Jeshi la Anga la Marekani (USAF) mwaka 1959. Baada ya matengenezo ya PGM – 17 Thor kukamilika, Marekani walipeleka makombora hayo UK ili kuidhibiti Soviet. Marekani na UK, waliuita mpango huo kwa jina la “Project Emily”.

Mwaka 1960, Marekani walipeleka Italia na Uturuki Makombora ya Nyuklia ya Jupiter (PGM-19). Wasifu wa PGM-19 unafanana na PGM – 17 Thor. Yote ni makombora ya masafa ya kati (IRBM). PGM – 19 yalikuwa na uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia vya megaton 1.5. Shabaha ya kupeleka zana hizo Italia na Uturuki ilikuwa maandalizi ya kuikong’ota Sovieti.

Kutoka UK hadi Italia na Uturuki, makombora ya PGM – 17 Thor na PGM 19, yalitegwa kuelekea mji mkuu wa Urusi, Moscow, yalipokuwa makao makuu ya Soviet. Dola ya Soviet, iliyokuwa inaongozwa na Nikita Khrushchev, kwa wakati huo, ilitafsiri vitendo hivyo vya Marekani kama uchokozi usiovumilika. Kisha tena, Marekani wakaanzisha mpango walioupa jina (codename), Mradi wa Kicuba “Cuban Project”.

Mradi wa Kicuba uliitwa pia “Operation Mongoose”, ambalo ni jina lililopitishwa kwenye kikao kilichofanyika Ikulu ya Marekani, White House, Novemba 4, 1961, chini ya uongozi wa Rais Kennedy. Operation Mongoose ilihusu mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia, na kufanya ionekane yalitekelezwa na vyombo vya dola vya Cuba. Lengo lilikuwa kuwatia hasira wananchi ili wampindue aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro.

Katika kuikabili Marekani na visa vyake, Khrushchev na Castro, walikutana haraka na kufanya uamuzi wa kujenga mitambo ya makombora ya nyuklia (Underground Missile Silo), nchini Cuba. Marekani na Cuba ni jirani mithili ya pua na mdomo. Ujenzi ulianza haraka. Oktoba 1962, ndege ya kijasusi ya Marekani, Lockheed U-2, au kwa jina lingine “Dragon Lady, ilifanikiwa kunasa picha ya ujenzi wa mtambo huo wa makombora ya nyuklia nchini Cuba.

Picha hiyo iliitisha Marekani. Kennedy aliitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Taifa (NSC), pamoja na watu wengine muhimu, na kuunda Kamati ya Utendaji ya Baraza la Usalama la Taifa (Excomm). Kennedy alishauriwa kuivamia Cuba kwa mashambulizi ya anga, ili kusambaratisha mitambo ya makombora ya nyuklia. Hata hivyo, Kennedy alichagua njia ya kudhibiti bahari ili makombora zaidi kutoka Soviet yasifike Cuba.

Njia hiyo ambayo Kennedy aliamua kuitumia, huitwa “Blockade”, yaani mpango wa kitumia nguvu ya kijeshi kuzuia meli za Soviet kuingia Cuba. Blockade ni mpango wa kijeshi wa kuzuia chakula, silaha, mawasiliano, au vitu vingine vyovyote, kuingia au kutoka mahali husika. Blockade huweza kuhusu udhibiti hata wa wawatu kuingia au kutoka kwenye nchi au eneo fulani.

Kennedy alikwepa kutumia neno “Blocked”, kwa hofu kwamba lingeamsha vita ya moja kwa moja, badala yake aliita “Quarantine”, yaani karantini. Tangazo la Marekani kuzuia meli za Soviet kuingia Cuba alisema ilikuwa kuiweka nchi hiyo kwenye karantini. Mvutano huo ambao ulikaribia kuiingiza dunia kwenye janga la vita ya nyuklia, ulimalizwa kwa mazungumzo.

Kennedy na Khrushchev walifanya mazungumzo na kukubaliana kusitishwa kwa mpango wa makombora ya nyuklia Cuba, vilevile Marekani ikasaini kutoivamia na kuiingilia Cuba. Makubaliano mengine, Marekani waliridhia kuondoa makombora yao Italia, Uturuki na UK, yaliyokuwa yameelekezwa Moscow. Hatimaye, Marekani na Urusi walifungua mwanzo mpya wa mawasiliano ya moja kwa moja baina ya viongozi wa nchi hizo mbili.

Mpango huo wa mawasiliano unaitwa Moscow – Washington hotline, zamani mfumo huo Marekani ulijulikana kama Washington – Moscow Direct Communications Link. Tangu mwaka 2008, Moscow – Washington hotline imekuwa ikitumia njia ya mtandao wa kompyuta, tofauti mwanzoni ulipokiwa ukitumia simu. Hadi sasa, mambo yakiwa magumu, viongozi wa Marekani na Urusi, huzungumza moja kwa moja.

 Blockade haikufanikiwa mwaka 1962, amani ikatafutwa na Moscow – Washington hotline ilizaliwa mwaka 1963. Kutoka Oktoba 28, 1962, siku makubaliano ya kimsingi yalipofikiwa baina ya Marekani na Soviet (Urusi), hadi leo, ni miaka 63, miezi mitano na siku 18. Msamiati wa blockade unatikisa dunia kwa mara nyingine. Ni neno linalotamkwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Wakati Kennedy alilikwepa na kuita karantini, Trump mwenye uthubutu usiokokotoa hatari, ametangaza kuifunga Iran kwa kizuizi cha kijeshi (naval blockade). Kwamba, hakuna meli kuingia au kutoka Iran au kwenye Mlango Bahari wa Hormuz. Maana yake ni kuwa Iran itashindwa hata kuiuzia China mafuta. Je, China watakubali?

Asilimia 90 ya mafuta ya Iran, yananunuliwa na China. Maana yake, China imekuwa mnufaika mkubwa wa mafuta ya Iran, ambayo nayo inapata unafuu mkubwa wa kuishi, kutokana na vikwazo ambavyo wamewekewa na nchi za Magharibi. Kwa kununua mafuta, China imekuwa mkono wa kuume kwa Wairan.

Iran hutumia mtandao wa satelaiti wa China, unaoitwa Chinese BeiDou Navigation Satellite System (BDS). Mfumo huo ndiyo huisaidia Iran kurusha makombora na ndege zake zisizo na rubani (drones), na kufika mahali wanapokusudia kwa uhakika. Sarafu ya China, Yuan, ndiyo imekuwa mkombozi wa Iran katika kukabiliana na vikwazo. Iran na China wamekuwa wakifanya biashara kwa mtindo wa kubadilishana bidhaa (barter trade).

Marekani na Israel walipoanza kuishambulia Iran Februari 28, 2026, waliwapa Iran chanzo kipya cha mapato. Iran walidhibiti Hormuz na kupitisha meli ambazo zililipa ushuru kwa Yuan na kwa sarafu za kidigitali (cryptocurrency). Kwa maana hiyo, mipango ya Iran imekuwa ikiinufaisha China, hasa katika kukuza thamani ya sarafu yake.

Ongezea kuwa malighafi nyingi za vifaa vya kijeshi ambavyo Iran huunda, zinatoka China. Rada za Iran na mifumo yao ya uchunguzi wa kiusalama (security tracking), kila kitu kinatoka China. Swali ni je, Trump kuifunga Iran, China inaweza kubaki kimya? Ikose mafuta, manufaa ya kibiashara na tawi la kukuza thamani ya sarafu yake?