KOCHA wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, amefikisha mechi tano za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu alipoteuliwa kukiongoza kikosi hicho, huku akikiri wazi ana kazi kubwa ya kukinasua na janga la kutoshuka daraja.
Nsajigwa aliyejiunga na timu hiyo Februari 27, 2026 akichukua nafasi ya Mkenya, Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili Februari 25, 2026, ameiongoza Prisons katika mechi tano bila ya kuonja ladha ya ushindi.
Katika mechi hizo tano za Ligi Kuu ambazo Nsajigwa ameiongoza timu hiyo ikipoteza tatu na kutoka sare mbili, ingawa kwa ujumla kikosi hicho kimecheza mechi 19, kikishinda tatu, sare tano na kupoteza 11, kikiwa nafasi ya 15 na pointi 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Akizungumzia kiwango cha timu hiyo tangu ameteuliwa, Nsajigwa alisema bado kuna nafasi ya kufanya vizuri katika mechi 11 zilizobaki kutokana na gepu dogo la pointi lililopo na washindani wake, ingawa jitihada zaidi zinahitajika pia.
“Nafasi tuliyopo sio nzuri na tunahitaji kujipanga vizuri kwa mechi zetu zilizobakia, unapocheza mechi zaidi ya tano na haupati kile unachokusudia kiukweli inakatisha sana tamaa, japo sisi bado tuko vitani na tunapambana,” alisema Nsajigwa. Wakati anacheza soka, Nsajigwa aliitumikia Tanzania Prisons ya Mbeya, kisha kujiunga na Yanga kuanzia mwaka 2006 hadi 2012, huku pia akiwa ni nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Taifa Stars.
Katika ufundishaji, msimu huu wa 2025-2026, Nsajigwa aliiacha Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship ikishika nafasi ya nne na pointi 37, baada ya kucheza mechi 19, ikishinda 11, sare nne na kupoteza pia nne, ikifunga mabao 26 na kuruhusu 17.
Kwa upande wa Otieno aliyejiunga na Prisons, Julai 24, 2025, msimu wa 2025-2026 aliiongoza Tanzania Prisons katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara ambapo alishinda tatu sawa na sare na kupoteza nane, ikifunga mabao nane na kuruhusu 16.
Katika mechi hizo 14, Otieno aliiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia Gor Mahia, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB zote za kwao Kenya na timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’.