Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kusukuma mbele ajenda ya uchumi wa bluu kama nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi nchini Tanzania na Zanzibar, uelewa kwa jamii za pembezoni mwa bahari bado ni mdogo, hali inayozua changamoto katika kunufaika kwa usawa na rasilimali za bahari pamoja na fursa zinazozalishwa kupitia sekta hiyo.
Kwa mujibu wa utafiti wa Mradi wa Ulimwengu wa Bahari ya Waswahili (Swahili Ocean World’s Project), unaoongozwa na Profesa Paula Uimonen na kufadhiliwa na Baraza la Utafiti la Sweden kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Stockholm, changamoto kubwa iliyobainika si tu uwepo wa sera ya uchumi wa bluu, bali namna inavyoeleweka na kutafsiriwa katika ngazi ya jamii.
Watafiti wanasema tafiti zilizofanyika katika maeneo ya Bagamoyo, Unguja na Pemba zimeonesha kuwa licha ya juhudi za Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza ajenda hiyo, jamii nyingi za maeneo hayo bado hazina uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya uchumi wa bluu.
Hali hiyo imesababisha sera kutafsiriwa kama fursa ya wachache badala ya kuwa ajenda jumuishi ya maendeleo.
Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo, watafiti hao wameendesha mikutano mbalimbali ya majadiliano na wadau katika maeneo ya utafiti ili kupata uelewa wa moja kwa moja kutoka kwa jamii kuhusu namna wanavyoishi na kutumia rasilimali za bahari.
Kupitia mchakato huo, wameandaa na kuchapisha chapisho maalumu la matokeo ya utafiti na mapendekezo ya sera, ambalo limezinduliwa Jumatano Aprili 15, 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jijini Dar es Salaam, likilenga kusaidia kuboresha uelewa wa uchumi wa bluu na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika fursa hizo.
Wakizungumza katika uzinduzi wa chapisho hilo watafiti hao wamesema matokeo yanaonesha pengo kubwa kati ya sera, uelewa wa jamii na uhalisia wa maisha ya wananchi hususan wavuvi wadogo na wanawake wanaotegemea bahari kwa maisha yao ya kila siku.
Mhadhiri Mwandamizi wa Ndaki ya Sayansi jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COSS-UDSM), Dk Thomas Ndaluka amesema utafiti umebaini kuwa jamii nyingi zinaona uchumi wa bluu kama ajenda ya watu wenye mitaji mikubwa, hali inayowafanya wavuvi wadogo kujihisi kutengwa na wakati mwingine kupoteza nafasi zao za uvuvi.
“Tumebaini kuna mtazamo kwamba huu ni uchumi wa matajiri. Hali hii imesababisha baadhi ya jamii kuondolewa katika maeneo yao ya uvuvi ili kupisha uwekezaji mkubwa,” amesema.
Hali hii inaonesha namna jamii ikikosa taarifa sahihi inavyoweza kupoteza fursa muhimu na kuendelea kukumbana na matatizo ya umasikini katikati ya fursa za kiuchumi.
Mkuu wa Ndaki hiyo ya Sayansi Jamii ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Christine Noe, amesema ushirikiano kati ya chuo hicho na wadau wa kimataifa umewezesha kufanyika tafiti na kupata majibu ya kisera yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa ajenda hiyo muhimu ya kitaifa ya uchumi wa bluu.
Amesema chapisho lililozinduliwa linaweka mapendekezo mahsusi ya kuhakikisha jamii zinashirikishwa kikamilifu katika mipango na miradi ya uchumi wa bluu badala ya kubaki watazamaji.
Kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Marine Hatchery, Sheha Hamduni, amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha malengo ya uchumi wa bluu, lakini akasisitiza kuwa mafanikio yake yanategemea namna sera zinavyowafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.
“Uchumi wa bluu kwa Zanzibar ni maisha ya watu. Ni muhimu mijadala ya sera isibaki kwenye makongamano bali iwafikie wananchi moja kwa moja ili kuwapa uelewa mpana na kunufaika na fursa zilizopo,” amesema.
Katika wito wa utunzaji wa mazingira ya bahari pamoja na utekelezaji wa majukumu ya uchumi wa blue, Meneja wa Tafiti za Mazingira wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Dk Rose Mtui amesema uchumi wa bluu unaweza kuwa injini ya maendeleo lakini mafanikio yake yanahitaji uelewa wa pamoja na usimamizi thabiti wa rasilimali za bahari.
Dk Rose ameongeza kwa msisitizo kuwa: “Uchumi wa bluu una mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, lakini bila kuzingatia athari za kimazingira katika usimamizi wa bahari, mafanikio yake hayawezi kuwa endelevu.”
Wakifafanua namna ya kufikisha taarifa za uelewa katika jamii, watafiti hao wamesema chapisho maalumu lililozinduliwa ni hatua muhimu ya kuunganisha matokeo ya utafiti na sera, likilenga kuongeza uelewa wa jamii, kuboresha ushirikishwaji na kuhakikisha uchumi wa bluu unakuwa chachu halisi ya maendeleo jumuishi kwa jamii nchini.
