Wanaofanya uandishi bila ithibati kusakwa

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Patrick Kipangula amesema bodi hiyo itaanza kupita mkoa hadi mkoa kufanya ukaguzi kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi bila kuthibitishwa na bodi hiyo.

Hatua hiyo ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria ya huduma za habari sura ya 229 ya sheria za Tanzania pamoja na Kanuni za Sheria ya Huduma za habari za mwaka 2017 ikiwa na lengo la kuimarisha weledi, uwajibikaji na heshima ya taaluma ya habari nchini.

Ikumbukwe bodi ilizinduliwa Machi 2025 na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo wa wakati huo, Profesa Palamagamba Kabudi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya taaluma ya waandishi wa habari.

Kipangula ameyasema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari walioshiriki kwenye kikao cha wenyeviti na makatibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na waandishi wa habari ulioandaliwa na Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, leo Jumatano Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP, David Misime akizungumza kwenye kikao cha wenyeviti na makatibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na waandishi wa habari ulioandaliwa na idara ya habari msemaji mkuu wa Serikali, leo Jumatano Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam.

Kipangula amesema wasio na ithibati hawana budi kupisha tasnia hiyo kwa kuwa sheria imeshaanza kufanya kazi na hadi sasa bodi hiyo imeshafikisha mwaka mmoja, huku akikiri kwamba bado kuna waandishi wa habari wanafanya kazi bila ithibati

“Tunaendelea kuwaondoa huku tukiendelea kuboresha mfumo wa kupata ithibati watu wapate kirahisi zaidi,” amesema.

Amesema wamepanga kuanza ukaguzi na wataanza kuzunguka mikoani huku akisema mwandishi wa habari akithibitishwa na bodi akapatiwa kitambulisho ni kinga itakayolinda taaluma yake.

Katika hatua nyingine amesema ni vizuri waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari zenye masilahi ya jamii.

Katika hatua hiyo waandishi wa habari wamekumbushwa kuzingatia misingi ya uandishi ikiwemo habari za hakika na vyanzo rasmi.

Ulinzi wa watoto, picha za maiti, ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu, uhakika wa taarifa na vyanzo vyake, kuepuka ubaguzi wa kijinsia na kutoeneza chuki.

“Kutumia kiangalifu akili unde (AI), kwa maana siku hizi teknolojia hii imekua na inahitaji umakini,” amesema.

Katika mkutano huo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema tasnia ya habari ina jukumu kubwa katika ustawi wa nchi, ikiwemo dira ya maendeleo, amani, umoja mshikamano, maridhiano na uchumi.

Amesema Serikali imekaa karibu na vyombo na waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao.

“Vyombo vya habari vikitumika ndivyo sivyo vinaweza kuleta madhara makubwa. Nawapongeza vyombo vya habari Tanzania kwa kutumia kalamu zao kuhamasisha amani, utulivu na umoja,” amesema Msigwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza kwenye kikao cha wenyeviti na makatibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kilichoandaliwa na idara ya habari ofisi ya msemaji mkuu wa Serikali, leo Jumatano Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam.

 “Ukiamua uandishi wangu wa habari utakuwa wa kuumiza watu basi utaumiza watu kwa kuwa uko mwenyewe. Lazima uwe na ajenda yenye manufaa kwako wewe na Watanzania,” amesema.

Amesema anatambua vyombo vya habari vina changamoto na Serikali imeanza kufanyia kazi ikiwemo kulipa madeni.

Msigwa amesema haiwezekani kuwa na waandishi wa habari wanaoishi kwa kutegemea posho za wanaowafanyia kazi, hivyo upo mpango wa kuwawezesha kiuchumi utakaoanza na mafunzo pamoja na mikopo.

Mhandisi Andrew Kisaka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), amesema hakuna Taifa lisilokosa migogoro na katika hali hiyo waandishi wa habari wanalo jukumu katika kuripoti na kusuluhisha.

Kenneth Simbaya, Mkurugenzi Mtendaji UTPC, amesema waandishi wa habari wanapaswa kukosoa kwa kutoa suluhisho ikiwa ni sehemu ya kujikita katika taaluma.

Akizungumzia uandishi wa habari wenye nia ya kujenga Taifa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Egbert Mkoko amesema tasnia hii ina mchango mkubwa katika ujenzi wa amani, taswira ya Tanzania na maadili ya jamii.

Washiriki wa kikao cha wenyeviti na makatibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kilichoandaliwa na idara ya habari ofisi ya msemaji mkuu wa Serikali, leo Jumatano Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam.

“Uandishi wa habari una nguvu kubwa sana ya kuimarisha demokrasia ya nchi, kujenga amani ya nchi, pia unaweza kubadilika na kubomoa kabisa Taifa,” amesema.

Kwa upande wa usalama, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema jeshi hilo linazingatia usalama wa waandishi wa habari na Watanzania wote kwa ujumla.

“Jeshi litaendelea kushirikiana na waandishi na vyombo vya habari pamoja na uhusiano bila kuathiri majukumu ya kila siku,” amesema.