Aweso aonya upotevu wa maji, lugha chafu za watumishi

Dodoma. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameziagiza bodi za maji nchini kuhakikisha wanakomesha uvujaji wa maji na kuwahimiza watumishi wawe na lugha nzuri kwa wateja kuliko kauli za kuwavunja moyo.

Aweso ametoa maagizo hayo jana Jumatano Aprili 15, 2026 wakati akizungumza na watumishi na viongozi kwenye uzinduzi wa bodi ya 10 ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), akionya upotevu wa maji hautavumiliwa kwa mamlaka husika.

Alitoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya Duwasa kuwa imekuwa na upotevu wa maji kwa kiwango cha asilimia 33.7 ambacho ni zaidi ya wastani wa juu wa upotevu wa maji kwa Taifa na dunia wa asilimia 20.

“Upotevu huu hauvumiliki, sitanyamaza katika hili na niseme hapa kuwa, baadhi ya  watumishi wenu wanasababisha hali hiyo ikiwemo kuwaunganishia wenye mahoteli makubwa na viwanda kinyemela, nataka muanze kutathimini hayo maji yanayopotea ni fedha kiasi gani zinapotea,” amesema Aweso.

Katika kusisitiza hilo, amesema: “Nakuagiza Mwenyekiti wa bodi hii mpya, Jumatatu tukutane mbele ya menejimenti ya wizara mtueleze mnafanya nini kumaliza matatizo haya na mkakati wa kuongeza maji katika Jiji la Dodoma ambalo linakuwa kwa kasi, shughulika na hawa baadhi ya watumishi wasiokuwa na uaminifu msiwavumilie.”

Waziri Aweso amekemea tabia ya ubambikiziaji wa bili za maji kwa wananchi, kuchelewesha kuunganishiwa maji hata wanapokuwa wamelipa na lugha mbaya kwa baadhi ya watumishi akisema hali hiyo inapaswa kukomeshwa na wenye jukumu hilo ni bodi ya maji.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amewaomba viongozi wa mikoa na wilaya kupitia kamati za ulinzi na usalama ili wasaidie kwenye ulinzi wa miundombinu na watakaokamatwa kwenye uhalifu huo, washtakiwe kwa uhujumu uchumi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Rose Ambrose ameonya watumishi wenye lugha zisizofaa kwa wateja akisema watakaobainika kwa namna yoyote hawatavumiliwa kwani lazima watambue kuwa  wana haki zao ambazo ni lazima ziheshimiwe.

Ambrose amesisitiza udhibiti wa maji yanayovuja akisema yanasababisha hasara na wakati mwingine hasara hizo haziwi na msingi bali zinatokana na uzembe mtupu kwa watumishi wenye jukumu hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Duwasa, Aron Joseph amesema uzalishaji wa maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hiyo upo kwa asilimia 55 ambapo wanazalisha lita 88 milioni kwa siku ambayo wanahudumia wateja 98,896.

Joseph amesema changamoto nyingine ni mtandao wa maji taka usiotosheleza ambapo ndani ya Jiji ni wateja 6,738 pekee ndiyo wanahudumiwa na mtandao huo wenye kilomita 119. Amesema kwa kushirikiana na bodi mpya itakayoongozwa na Fadhiri Chibago, wanatarajia kuongeza mtandao na kuboresha miundombinu yake.