Trump Azua Mjadala Baada ya Kuposti Picha ya Yesu Akimkumbatia, Aendelea Kumkosoa Papa

Global Publishers
April 16, 2026
0 Comments

Rais wa Marekani Donald Trump ameibua mjadala mkubwa mtandaoni baada ya kushirikisha picha inayodaiwa kutengenezwa kwa teknolojia ya AI, ikimuonesha akikumbatiwa na Yesu mbele ya bendera ya Marekani.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Trump alisema picha hiyo ni nzuri licha ya kukosolewa na baadhi ya watu aliowaita “Radical Left.” Hatua hiyo imezua hisia mseto, huku baadhi ya watu wakiona ni jambo la kawaida la kisiasa, lakini wengine wakiliona kama kukosa heshima kwa masuala ya kidini.

Wakati huo huo, Trump ameendelea kumkosoa Papa Leo XIV, akishirikisha machapisho yanayodai kuwa kabla ya kuwa Papa, aliwahi kumkosoa yeye pamoja na Makamu wa Rais JD Vance kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa upande wake, Vance pia aliingia kwenye mjadala huo akimtaka Papa kuwa makini anapozungumzia masuala ya teolojia, akisisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuzingatia ukweli wanapotoa kauli zao.

Kauli na vitendo hivi vimeongeza mvutano kati ya wanasiasa wa Marekani na viongozi wa dini, hasa ndani ya jamii ya Wakatoliki, ambapo baadhi ya wachambuzi wanasema hali hiyo inaweza kuleta mgawanyiko wa kiimani na kisiasa.

Hadi sasa, Pope Leo XIV hajatoa tamko rasmi kujibu mashambulizi hayo, huku mjadala ukiendelea kushika kasi katika majukwaa mbalimbali ya kijamii.