Dar es Salaam. Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera amehitimisha ziara yake ya siku tisa nchini ambapo amekutana na makundi tofauti, akizungumza nao kuhusu yaliyotokea siku na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Chakwera, Rais mstaafu wa Malawi, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, Novemba mwaka jana, kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo atakayefanya ziara nchini kuhusu yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu iliopita.
Tayari kiongozi huyo amekutana na makundi mbalimbali ya viongozi wa kisiasa na Serikali na kufanya nao mazungumzo, ambayo hata hivyo yeye mwenyewe bado hakuyaweka wazi.
Ziara yake hiyo ilianza Aprili 8, 2026 alipowasili nchini na inakoma leo Aprili 16, 2026 ambapo anatarajiwa kuelekea London, Uingereza, kwa mujibu wa ratiba.
Chakwera alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, mawaziri akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye aliongoza ujumbe wa Serikali katika mazungumzo hayo.
Mbali na kukutana na ujumbe wa Serikali, Chakwera alifanya mazungumzo na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, pia vyama vya siasa vya ACT–Wazalendo, National League for Democracy (NLD), United Democratic Party (UDP), National Reconstruction Alliance (NRA), NCCR Mageuzi, Sauti ya Umma (Sau), Alliance for Democratic Change (ADC), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Ada-Tadea.
Vyama vingine ni pamoja na Democratic Party (DP), Tanzania Labour Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), United People’s Democratic Party (UPDP), Chama cha Kijamii (CCK), Demokrasia Makini, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mjumbe huyo maalumu, pia, alikutana na wadau mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na baada ya Uchaguzi Mkuu, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Othman Chande, Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Warioba na jumuiya zisizo za kiserikali
Viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wakizungumza na Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera leo Ijumaa, Aprili 10, 2026 jijini Dar es Salaam.
Wengine aliokutana nao ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jaji George Kazi, Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji George Masaju, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro.
Wachambuzi waeleza matarajio
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema matarajio ya kupatikana kwa suluhu katika mchakato wa maridhiano nchini yatategemea ripoti atakayoiwasilisha.
Amesema kwa sasa ni vigumu kujua kwani hadi sasa hakuna taarifa zaidi zilizopatikana kupitia mazungumzo yake na wadau mbalimbali nchini aliokutana nao.
Rais wa Zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewasili nchiniAprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi. Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.
Amesema ripoti hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha maridhiano, kwani kwa sasa mchakato huo unaonekana kukwama kutokana na baadhi ya wadau kuonekana kutokuwa tayari kushirikiana kikamilifu au wengine kuamiani kundi fulani halistahili kushiriki.
Mbunda amesema Chakwera ni mtu sahihi wa kusaidia kutafuta suluhisho, kwa sababu ni mtu aliyeshindwa katika uchaguzi, akieleza kuwa anaweza kuwasilisha ripoti yenye mapendekezo yatakayosaidia Tanzania kujinasua kutoka katika mkwamo uliopo.
“Kwa sasa Tanzania ni kama tunaishi kwa tahadhari na kutoaminiana. Maridhiano ni muhimu ili kuleta mshikamano, na kwa hakika yatachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushauri utakaojumuishwa katika ripoti hiyo,” amesema Mbunda.
Kwa upande wake, Profesa George Kahangwa amesema ujio wa Chakwera unaonyesha Jumuiya ya Madola imeshiriki kuliko ingekaa kimya, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini iwapo kulikuwa na Tume ya Rais pamoja na ile ya Chakwera.
Amesema matarajio yatategemea ripoti zao; ikiwa hazitakuwa na utofauti, basi juhudi hizo hazitakuwa na maana.
“Tunatarajia ripoti ya Chakwera itakuwa huru na itafanya kazi kwa undani. Hata hivyo, kutokana na muda aliopewa, nina wasiwasi kuwa Chakwera amekaa kwa muda mfupi na huenda asipate matokeo bora, ili upate kitu bora kinahitaji muda” amesema.
Amesema Chakwera amekuja na kukutana na baadhi ya makundi machache, ikiwemo wanasiasa, lakini ameliacha kundi muhimu la waathirika, hasa wale waliopoteza ndugu zao.
“Hatujamuona akizungumza nao, ilhali hilo ndilo kundi muhimu zaidi. Watu wamepoteza ndugu zao, na baadhi yao hawajapata hata miili yao. Nafikiri hili ndilo kundi lililopaswa kupewa kipaumbele kusikilizwa,” amesema
