Moshi. Baadhi ya wakulima mkoani Kilimanjaro wamelalamikia kuadimika kwa mbolea ya kukuzia (Urea), hali inayoibua hofu ya kutopata mazao katika msimu huu wa kilimo, licha ya kuwepo kwa mvua za kutosha.
Wakulima hao wamesema, licha ya changamoto ya upatikanaji wa mbolea hiyo, bado wanakumbana na changamoto ya bei kubwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaouza mfuko wa kilo 50 kwa Sh150,000 badala ya bei elekezi ya ruzuku ya Sh75,000.
Mwananchi imepita katika maduka mbalimbali yanayouza pembejeo za kilimo mkoani hapa na kubaini kuwa mbolea hiyo haipatikani, jambo linaloongeza wasiwasi miongoni mwa wakulima hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao wamesema kukosekana kwa mbolea ya kukuzia kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mahindi, hivyo kuhatarisha upatikanaji wa mavuno katika msimu huu.
Mmoja wa wakulima wa mahindi kutoka Lyamungo, Yesse Shoo, amesema kwa siku kadhaa amekuwa akitafuta mbolea hiyo bila mafanikio, jambo linalohatarisha uzalishaji wa zao hilo.
“Nimetafuta mbolea hii kwa zaidi ya siku nne. Ukienda kwenye duka hili wanakwambia hakuna, nenda sehemu fulani, ukifika kule unaambiwa hakuna. Unaagiziwa tena sehemu nyingine, unaambiwa kuna sehemu imepatikana inauzwa Sh120,000, ukifika nako hakuna,” amesema.
Aidha, mkulima huyo ameiomba Serikali iwasaidie kutatua changamoto hiyo ya mbolea kutokana na kuadimika kwake.
“Tumezunguka kutafuta mbolea. Tunaomba Serikali itusaidie changamoto hii ya mbolea, maana haya mahindi tuliyootesha yakipitiliza muda wake wa kuweka mbolea, haifanyi kazi tena, maana muda unakuwa umeshapita.
“Kwa sasa tunahofu kiasi kwamba, hata kama mvua inanyesha, mavuno yatakuwa machache, hivyo Serikali itufikirie tupate mbolea angalau kwa muda huu uliobaki,” amesema.
Mkulima mwingine wa mahindi, Teddy Mushi, amesema licha ya kwamba mbolea imekuwa adimu, upatikanaji wake umekuwa wa changamoto na hata ikipatikana, hupatikana kwa gharama kubwa.
“Mbolea imekuwa changamoto kubwa, na hata wale ambao wana mbolea hizi wanauza ghali. Mfuko wa kilo 50 wanauza Sh150,000 badala ya Sh75,000 ya bei ya ruzuku, na hii tunaipata kwa kubembeleza. Kwa kweli, hii ni changamoto kubwa.
“Serikali inatakiwa kuwa makini na hili, maana tumewekeza kwenye kilimo hiki, lakini tunachokiona mwaka huu ni kwamba mavuno yatakuwa kidogo sana. Kwa kweli, hatujawahi kukumbana na changamoto hii,” amesema.
Mmoja wa wauzaji wa pembejeo za kilimo mkoani hapa, Ayubu Myone, amesema upatikanaji wa mbolea umekuwa wa shida, na kwamba hawajui ni lini changamoto hiyo itaisha.
“Wiki hizi tatu zilizopita, mbolea ya kukuzia imekuwa shida. Hofu yangu ni kwamba Serikali iangalie, kwa sababu kutakuwa na mavuno kidogo upande huu wa Kaskazini. Tunakonunulia wanasema hakuna mbolea, na sababu hatuelezwi,” amesema msambazaji huyo wa mbolea.
Aidha, amesema kukosekana kwa mbolea hiyo kunawapa changamoto, kutokana na kwamba kila siku wakulima wanafika kuchukua mbolea, lakini haipatikani, hali inayowapa usumbufu mkubwa.
“Wakulima wanakuja, wanauliza mbolea kila siku, hakuna. Hatujui shida ya Serikali ni nini au ni nini kimetokea kwa wasambazaji wakubwa wa mbolea. Maana Serikali imetoa ruzuku, na ruzuku yenyewe ndiyo hivyo haionekani.
“Mbolea isipopatikana, hakutakuwa na mavuno yoyote. Hili litakuwa janga kubwa, hivyo tutegemee kilio kikubwa kutoka kwa wakulima,” amesema.
Meneja wa Udhibiti wa Mbolea Kanda ya Kaskazini (TFRA), Gothard Liampawe, amesema changamoto ya mbolea imebainika katika wilaya za Siha, Hai na Moshi, na kwamba inatokana na mahitaji ya mbolea hiyo kuwa makubwa.
Aidha, amesema Serikali imeweka mpango madhubuti kuhakikisha mbolea inapatikana na kuhakikisha mawakala wanaagiza mbolea kwa wingi kulingana na mahitaji yaliyopo.
“Kwa sasa tuna jumla ya tani 247.5 za mbolea ambazo mawakala na wasambazaji wameshafanya malipo, na mbolea zimeshaanza kupakiwa kwa mawakala tofauti tofauti,” amesema Liampawe.
Aidha, ametoa angalizo kwa mawakala wasio waaminifu wanaouza mbolea nje ya mfumo wa ruzuku, akisema wakibainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
“Kuna baadhi ya mawakala wamekuwa si waaminifu, wanauza mbolea nje ya mfumo wa ruzuku. Tunaendelea kufuatilia, na pale itakapothibitika kwamba wamekiuka taratibu, tutachukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wote, ikiwa ni pamoja na kufunga akaunti zao katika mfumo, kusitisha huduma na kufuta leseni zao, pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria,” amesema.
