Dar es Salaam. Baada ya madai ya baadhi ya wananchi kuwa Ubalozi wa China nchini Tanzania hauna utaratibu mzuri wa kuomba hati ya kusafiria (visa), ubalozi huo umetaja hatua tano za kufuata ili kupata hati hiyo.
Madai ya baadhi ya watu (majina yamehifadhiwa), waliopata huduma katika ubalozi huo, ili upate huduma unapaswa kuamka alfajiri kwenda kupanga foleni, na muda ukifika wa mlango kufunguliwa watu huvutana na hata wakati mwingine huvunja mlango.
“Ukiingia ndani ya ubalozi saa tano na nusu wanafunga. Kama kulikuwa na watu nje, wanapaswa kuondoka, na hapo hakuna utaratibu wa miadi. Nilikwenda ili nisafiri, ila nimeahirisha kwa namna ambavyo Watanzania wanadhalilishwa,” ameeleza mwananchi aliyekuwa akihangaikia utaratibu wa kwenda China.
Malalamiko hayo pamoja na video zilizoonekana hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii zikionesha Watanzania wakiwa wamejazana ubalozi wa China, yameufanya ubalozi huo leo, Aprili 16, 2026 kutangaza hatua za kutatua changamoto za upatikanaji wa viza hizo nchini.
“Katika kulipatia ufumbuzi suala hili, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefanya mazungumzo na Ubalozi wa China kwa lengo la kubainisha hatua muhimu za kuchukuliwa na waombaji wa visa ya China, ili kurahisisha uchakataji wa maombi na kupata mrejesho kwa wakati,” imeeleza taarifa hiyo.
Hatua ya kwanza ya kuzingatia ni waombaji kuzingatia maelezo ya fomu na kujaza taarifa zao kwa usahihi kupitia mfumo wa mtandao wa maombi (COVA System) unaopatikana kwenye tovuti ya https://cova.mfa.gov.cn/
Baada ya hapo, waombaji wanapaswa kuhakikisha nyaraka zote zinazoambatanishwa kwenye mfumo wa maombi ya visa ni sahihi, kamili na zinakidhi vigezo husika, ili kupunguza mchakato wa uhakiki wa maombi.
“Waombaji wawasilishe maombi ya visa mapema iwezekanavyo, angalau siku 30 kabla ya tarehe ya safari, ili kuupa muda ubalozi kuchakata maombi husika. Ubalozi hufanyia kazi maombi ya visa takribani 150 kwa siku (zingatia ratiba ya siku za mapumziko ya Ubalozi wa China),” imeeleza taarifa hiyo.
Hatua itakayofuata, waombaji wafuatilie kwa karibu hatua (status) ya maombi ya visa kwenye mfumo wa maombi (COVA System) ili kubaini kama miadi (appointment) ya kwenda ubalozini kuwasilisha pasipoti imekubaliwa.
Aidha, wasafiri wa mara kwa mara wanashauriwa kuomba visa ya kuingia mara nyingi (multiple entry visa) ili kupunguza maombi ya mara kwa mara katika ubalozi huo.
Pamoja na hayo, Wizara ya Mambo ya Nje inasisitiza wadau wote kuheshimu na kuzingatia sheria, taratibu, mila na desturi za nchi wanazotembelea ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.