Upasuaji Aga Khan ulivyorudisha tabasamu kwa Watanzania 16 wenye majeraha

Dar es Salaam. Upasuaji wa bure wa urekebishaji wa viungo uliofanywa kwa watu 16 waliokuwa na ulemavu pamoja na majeraha yaliyosababishwa na ukatili, ajali za moto umetajwa kurejesha tabasamu na matumaini kwa Watanzania hao.

Kambi hiyo maalumu ya kumi kufanyika nchini, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam (AKH, D), kwa kushirikiana na taasisi ya Reconstructing Women International (RWI) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imefanya upasuaji rekebishi wa  viungo uliorejesha uwezo wa kujongea na kuboresha maisha ya wagonjwa hao ambao ni wanawake na watoto waliokuwa na majeraha ya kuungua, ajali, na ukatili wa kijinsia.

Katika kambi hiyo iliyoanza Aprili 13 hadi 17, 2026, timu ya wataalamu wa kimataifa wa upasuaji wa kurekebisha viungo kutoka RWI, Marekani, Kanada, na Ulaya kwa kushirikiana na madaktari wa upasuaji kutoka Aga Khan na MNH jumla ya wanawake na watoto 24 walichaguliwa kwa uchunguzi wa kina ili kubaini ustahiki wao kwa upasuaji na hatimaye 16 kati yao waliokidhi vigezo wamepata matibabu bila gharama yoyote.

Akizungumza na waandishi waliofika hospitalini hapo kushuhudia wagonjwa hao leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Junior Jamal (13), aliyeungua moto akiwa bwenini shuleni kwao amesema anashukuru Mungu anaendelea vizuri.

“Bweni lilikuwa linaungua moto usiku yeye akainuka kuwasaidia wenzie bahati mbaya akaungua mikono na sasa amefanyiwa upasuaji anaendelea vizuri anaweza kukunja mikono,” amesema kaka yake aitwaye Abdul Mohamed.

Akitaja umuhimu wa kambi hiyo kwa maisha ya Watanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya Dk Hamad Nyembea amesema inaokoa watu hivyo amepongeza hospital ya Aga Khan kutokana na kuwa wadau wakubwa wa huduma za afya.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya Dk Hamad Nyembea akizungumza leo kuhusu kambi ya upasuaji kwa Watanzania wenye majeraha.

“Hatukua na wataalamu hawa wa upasuaji rekebishi miaka kumi iliyopita lakini sasa tunavyozungumza tunao na wengine wanasoma hii ni hatua muhimu katika sekta yetu,” amesema Dk Nyembea.

Kutokanaa na manufaa ya kambi hiyo, Dk Nyembea amesema atapendekeza Wizarani ianze kufanyika mara mbili kwa mwaka.

Amesema kuhusu upasuaji rekebishi zaidi ya watu 300 wameshapata huduma hiyo tangu kuanza nchini.

“Wageni hawa wanaokuja kufanya upasuaji wamesababisha kuwe na idara pale MNH na tunao mabingwa 13 hii ni hatua katika kuimarisha huduma za kibobezi nchini.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Aga Khan imefanikiwa kuanzisha huduma hiyo inayoanzia Muhimbili na kusambaa hospitali nyingine.

Amesema changamoto hiyo ni kubwa na wanaonufaika wengi ni watu wa Dar es Salaam kwahiyo kuanzia kambi zinazokuja watahamasisha watu wengi ili kuongeza idadi kutoka 300 kwenda juu zaidi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa jumla katika Hospitali ya Aga Khan, Aidan Njau amesema programu ya kuwasaidia Watanzania wanawake ambao afya zao zimeteteleka kutokana na majanga kama ajali, moto, kuharibika kwa vioungo kutokana na saratani inasaidia kwa kiasi kikubwa.

Amesema pia wanatumia zoezi hili kubadilishana ujuzi na wenzao kutoka Marekani na Ulaya. Wanafunzi wanaosomea udaktari pia wanajifunza ikiwemo teknolojia mpya.

“Zoezi hili ni bure na tunapata msaada kutoka Marekani na Ulaya na washirika wa hapahapa ndani ya nchi kufanikisha zoezi hili. Huu ni mwaka wa 10 tangu tuanze zoezi hili na tunajivunia sana.

Kupitia mpango huu wa kila mwaka katika Hospitali ya Aga Khan, unaotolewa bila malipo wagonjwa hupata fursa ya pili ya maisha wa kudumu.

Mkuu wa Kitengo cha upasuaji na Urekebishaji na plastiki Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Edwin Mrema amesema zaidi ya wagonjwa 264 wenye ulemavu mbalimbali uliosababishwa na ajali za barabarani, majeraha ya moto, na ukatili wa majumbani wamenufaika na ushirikiano huu.

“Pia, Chuo chetu cha Sayansi shirikishi (MUHAS), kimeanzisha hii kozi hii ya upasuaji tangu mwaka 2019 kwaajili ya kifundisha ili kuwazalisha watalaamu hawa hapahapa nchini wakafanye kazi maeneo mbalimbali,” amesema.

Naye, Dk Murtaza Mukhtar mkuu wa Operesheni ya Kliniki Aga Khan amesema kambi hiyo ya upasuaji ni gharama na ndio maana wanashirikiana na wadau kama Benki ya Stanbic kuwashika mkono ambayo imetoa zaidi ya Sh45 milion kwenye kambi hiyo kama alivyosema Mkuu wa biashara, Kai Mollel kutoka Stanbic Tanzania.

Kwa upande wake, Sisawo Konteh, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Health Service, Tanzania, ameishukuru Wizara ya Afya pamoja na wafadhili kwa mchango wao mkubwa wa kifedha ulioendelea kusaidia upasuaji huu kwa miaka mingi.