Lindi. Ubovu wa barabara umeendelea kuwa kilio kikubwa kwa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, huku wakimtaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wilayani humo kufika katika maeneo yaliyoathirika ili kujionea hali halisi wanayopitia wananchi.
Akitoa kero ya ubovu wa barabara kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani robo ya tatu (Januari hadi Machi) leo Ijumaa, Aprili 18, 2026, diwani wa Kata ya Kitumbikwera, Abdallah Mtalika, amewaambia Tarura kuwa barabara ya kutoka Kivukoni hadi Zahanati ya Kitumbikwera ni mbaya na ni barabara ambayo inatumika kusafirishia mazao ya biashara kama ufuta na korosho.
Ameendelea kusema kuwa wakiacha hali hiyo iendelee, wakulima wa ufuta watalazimika kupeleka mazao yao Halmashauri ya Mtama kwa kuwa halmashauri hiyo imeboresha barabara zao.
“Mvua zinazoendelea kunyesha zimezidisha ubovu wa barabara hizo, hali iliyosababisha baadhi ya maeneo kushindwa kupitika kabisa na kuwaweka wananchi katika wakati mgumu wa usafiri na mawasiliano,” amesema Mtalika.
Diwani wa Kata ya Ng’apa, Issa Ngasha, akiwasilisha kero ya ubovu wa barabara kutoka Mtutu–Cheleweni hadi Mkanga iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Lindi, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani. Picha na Bahati Mwatesa.
Diwani wa Kata ya Mipingo, Hamza Msagula, amesema kuwa changamoto ya miundombinu imeathiri shughuli za kiuchumi, hususan kwa wakulima wanaotegemea barabara hizo kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.
“Barabara nyingi hazipitiki kabisa, wakulima wanashindwa kusafirisha mazao yao, hali inayopunguza kipato chao na kudumaza maendeleo ya wananchi,” amesema Msagula.
Madiwani hao wameonya kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, hali hiyo itaendelea kuathiri ustawi wa wananchi na kudhoofisha juhudi za maendeleo katika manispaa hiyo.
Mbali na wakulima, wananchi wengine wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wanafunzi pia wameathirika na hali hiyo, ambapo baadhi yao hulazimika kutumia muda mrefu kufika katika maeneo yao kutokana na ubovu wa barabara hizo.
Mariamu Juma, mkazi wa Nangaru, ameiomba Serikali kuwasaidia kutengeneza barabara hizo kwani kuna wakati wanashindwa kufanya shughuli za kijamii kutokana na ubovu wa miundombinu.
“Tunaomba mtusaidie kutukarabatia barabara zetu za Nangaru. Barabara ni mbovu sana, kuna wakati hata kuja mjini tunashindwa kwani baadhi ya maeneo hayapitiki,” amesema Juma.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Lindi, Magreth Ajabu, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo, akieleza kuwa baadhi ya miradi ya mwaka wa bajeti 2025/2026 bado haijaanza kutokana na vikwazo mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa wakandarasi na taratibu za zabuni.
“Nawahakikishia madiwani kuwa tayari tumeanza maandalizi ya bajeti ya dharura itakayowasilishwa makao makuu ili kuhakikisha barabara zilizoathiriwa na mvua zinapatiwa matengenezo haraka iwezekanavyo,” amesema Ajabu.
Hata hivyo, Tarura inaendelea kufanya tathmini ya kina ya barabara zote zilizoathirika ili kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa wa matengenezo ya haraka.