MZUNGUKO wa 23 wa Ligi Kuu Zanzibar umeanza kuchezwa Aprili 18, 2026 kwa michezo miwili kati ya Mlandege na Muembe Makumbi wakati Fufuni ikisaka alama tatu kwa Junguni kisiwani Pemba.
Ukiachana na mechi hizo ambazo timu zote zinapambana kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo huku Junguni ikikaribia kushuka, leo kuna vita ya timu za vikosi kati ya KVZ na Polisi.
Mechi hiyo sio kinyonge kwa timu hizo kwani KVZ inahesabu za kushinda ili kulinda utawala wake kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ifikishe pointi 46.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa KVZ, upande wa Polisi mambo ni tofauti, timu hiyo inahitaji kushinda kujiondoa kwenye mstari wa hatari wa kushuka daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa KVZ, Abduljalil Mohamed, alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Malale Hamsini ameitengeneza KVZ ambayo kila timu inahofia kucheza nayo.
Alisema kutokana na ubora wa timu hiyo, ipo tayari kwa mchezo huo na inaahidi ushindi na sio vinginevyo.
“Timu hazitaki kukiri kwamba zinahofia kukutana na KVZ ambayo Kocha Malale kaifanya kuwa bora zaidi ya ilivyokuwa awali,” alisema.
Ofisa Habari huyo, alisisitiza kuwa uwekezaji unaofanywa na KVZ ni kubeba mataji matatu ikiwemo Ligi Kuu Zanzibar, FA Cup na Muungano inayotarajiwa kuanza Aprili 21, 2026.
Kwenye mzunguko wa kwanza, KVZ iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi. Katika hatua nyingine, Mafunzo imeingia kambini kujiandaa na mchezo wao dhidi ya New King utakaochezwa Jumapili hii ambapo timu zote zina presha ya kushuka daraja msimu huu.