BAADA ya mapumziko ya mwezi mmoja, raundi ya 22 ya Ligi ya Championship, inaendelea tena leo Jumamosi kwa mechi mbili na nyingine tano kupigwa kesho Jumapili na moja kuhitimishwa keshokutwa Jumatatu, ikiwa ni tiketi ya lala salama msimu huu.
Songea United iliyotoka kuichapa TMA FC ya Arusha bao 1-0, mechi ya mwisho kabla ya kupisha mapumziko, itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji, mkoani Ruvuma, kucheza dhidi ya Bigman, iliyochapwa nyumbani na maafande wa Transit Camp mabao 2-1.
Timu hiyo ya Songea iko nafasi ya tisa na pointi 26, baada ya kushinda mechi sita, sare nane na kupoteza saba, huku kwa upande wa Bigman, imeshinda saba, sare sita na kupoteza nane na kikosi hicho kinashika nafasi ya saba na pointi 27.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, mjini, Tanga na African Sports, iliyo nafasi ya 15 na pointi 11, itaikaribisha Barberian FC, zamani Kiluvya United, inayoburuza mkiani ikiwa nafasi ya 16 na pointi 10.
Timu hizo zinakutana zikiwa na matokeo mabaya na Sports, imeshinda mechi tatu tu, sare mbili na kupoteza 16, huku kwa upande wa Barberian FC, ikishinda moja, sare saba na kuchapwa 13, zikipambana kujinasua na janga la kushuka daraja.
Kesho Jumapili, itashuhudiwa zikipigwa mechi tano na vinara wa Ligi ya Championship, Geita Gold yenye pointi zake 52, itakuwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita, kucheza dhidi ya Hausung FC ya Njombe, iliyo nafasi ya 14 na pointi 11.
Geita Gold ni vinara wa Ligi ya Championship kwa sasa ikiwa na pointi 52, baada ya kushinda mechi 16, ikitoka sare nne na kuchapwa moja, ikifunga mabao 38 na kuruhusu 12, ikipambana kurejea Ligi Kuu, baada ya kushuka msimu wa 2023-2024.
Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Geita ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera Sugar iliyo nafasi ya pili na pointi zake 49, baada ya kushinda mechi 15, sare nne na kupoteza mbili, itacheza dhidi ya B19, inayoshika nafasi ya 12 na pointi 21, ikishinda tano, sare sita na kupoteza 10.
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu iliposhiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, kikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23. KenGold, inayoshika nafasi ya nane na pointi 26, itakuwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya jijini, Mbeya, kucheza dhidi ya kikosi cha Mbeya Kwanza kutoka Tabora na timu hiyo inashika nafasi ya tatu hadi sasa na pointi 45.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu, baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Hata hivyo, KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu Bara na kushuka daraja msimu wa 2024-2025, ikimaliza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar, iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, TMA FC iliyo nafasi ya 11 na pointi 21, baada ya kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Songea United, itaikaribisha, Stand United, inayoshika nafasi ya 13 na pointi 20, iliyochapwa pia mabao, 2-0 na B19 FC. Mechi ya mwisho leo, itapigwa kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani na Transit Camp, iliyo nafasi ya nne na pointi 43, itaikaribisha Polisi Tanzania, inayoshika nafasi ya tano na pointi 42, ikiwa ni vita ya maafande hao.
Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Raundi ya 22, itahitimishwa keshokutwa Jumatatu kwa mechi moja kupigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini, Morogoro na Gunners FC, iliyoichapa Hausung FC ya Njombe, mabao 3-0, itacheza dhidi ya Mbuni FC, iliyoichapa KenGold ya Mbeya 3-0. Gunners FC, inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu huu, iko nafasi ya 10 na pointi 23, baada ya timu hiyo ambayo ni mabingwa wa First League msimu wa 2024-2025, kushinda mechi sita, sare tano na kupoteza 10, kati ya 21.
Kwa upande wa Mbuni FC, imekuwa na mwenendo wa kusuasua msimu huu na katika mechi 21, ilizocheza imeshinda 12, sare mbili na kupoteza saba, ikiwa nafasi ya sita na pointi 38, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 31 na kuruhusu 16.
Kocha wa B19 FC, Twaha Beimbaya, amesema mapumziko ya mwezi mmoja yamekuwa na manufaa kwa ajili ya kutengeneza balansi ya kikosi hicho, kuanzia eneo la kujilinda na ushambuliaji, hivyo, kwa sasa wako tayari ili kuendeleza ushindani zaidi.
“Kiujumla sisi kama benchi la ufundi tumekuwa na mwezi mmoja mzuri kwa sababu wakati ligi imesimama tulicheza pia mechi nyingi za kirafiki na timu zenye uzoefu, lengo kubwa ni kufanyia kazi changamoto zilizokuwepo mwanzo,” amesema Beimbaya