WAZIRI MKUU APONGEZA MCHANGO WA WANAWAKE UKUAJI WA UCHUMI

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewapongeza wanawake nchini kutokana na mchango mkubwa wanaoutoa katika kukuza uchumi uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati zinamilikiwa na wanawake hivyo inaonesha wazi kuwa injini ya uchumi wa Taifa inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na wanawake. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Aprili 18, 2026) katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano wa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (SMEs) na Maonesho ya Uwekezaji na Biashara yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Four Season jijini Arusha.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa uchumi jumuishi huchochea amani na mshikamano katika jamii kwa sababu kitendo cha ushirikiano wa pamoja kinawezesha kubadilisha hali ya uchumi na kufikia maendeleo jumuishi kwa wote.

“Tunapaswa kujenga uchumi jumuishi unaohusisha makundi yote ya jamii, kwa upande wetu  Serikali tutahakikisha ajenda hii inatekelezwa kwa vitendo”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali, huku akiahidi kuwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta binafsi itaendelea kuwa mhimili muhimu katika ajenda kuu ya uchumi. 

Amesema Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalumu wa kuwawezesha wahitimu wa vyuo vikuu kifedha ili kukuza mawazo yao ya kibiashara, pamoja na kuboresha sera zitakazoruhusu matumizi ya mali zinazohamishika kama dhamana, ikiwemo vyeti vya taaluma. 

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wajasiriamali kutumia kikamilifu fursa za miundombinu iliyoboreshwa, hususan reli ya kisasa (SGR) na reli ya TAZARA inayofanyiwa maboresho, ili kufikia masoko ya kimataifa kupitia kanda za Northern Corridor na Central Corridor, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Tanzania hadi maeneo kama Kapiri Mposhi nchini Zambia.

Kwa upande wake,  Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Pius Chaya ametumia furha hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri na msaada mkubwa anaoutoa katika ofisi yao na hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

Dkt. Chaya amesema kuwa wizara yao itahakikisha inaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wafanyabiasha Wadogo na wa Kati (SMEs) pamoja na wawekezaji ili waweze kukua na kutoa mchango wenye tija katika kufikia uchumi wa dola trilioni moja.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amesema Serikali imeweka mkazo katika kukuza Sekta ya Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) ili ziweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi, ajira na mapato kwa Taifa yatokanayo na kodi.  

Amesisitiza umuhimu wa urasimishaji wa biashara, uzalishaji wenye kuongeza thamani, kuzingatia viwango vya ubora pamoja na matumizi ya teknolojia za kidigitali umewezesha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

 Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kurahisisha taratibu, kuimarisha mifumo ya usajili na kulinda ubunifu ili kuwafanya wajasiriamali waaminike na kuvutia mitaji, kutoka kwa wawekezaji wa nje.