Mradi wa kusafisha majichumvi kuwa majisafi wazinduliwa Kinondoni

Dar es Salaam. Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kisima cha maji pamoja na mitambo ya kusafisha majichumvi kuwa majisafi katika Kituo cha Afya Kinondoni, mradi unaolenga kuboresha upatikanaji wa maji salama kwa wananchi na wagonjwa.

Mradi huo umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam kwa gharama ya Sh191.7 milioni, na unatarajiwa kunufaisha takribani wakazi 3,360 wa eneo hilo pamoja na watumiaji wa huduma za afya katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Wazo Mwang’onda, amesema ameridhishwa na ubora wa utekelezaji wake, akisisitiza kuwa unadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo  Mwang’onda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mhandisi Mkama Bwire wakiangalia maji katika  mradi wa kisima cha Maji Kituo cha Afya Kinondoni.

Amesema uwepo wa maji safi na salama katika vituo vya afya ni jambo muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu, kuzuia maambukizi ya magonjwa, na kuongeza ufanisi kwa wahudumu wa afya.

“Mradi huu ni kielelezo cha jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji, hasa katika maeneo nyeti kama vituo vya afya. Niwapongeze Dawasa (Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam) kwa kazi hii nzuri,” amesema Mwang’onda.

Kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa sekta ya maji, maeneo mengi ya ukanda wa pwani wa Dar es Salaam hukumbwa na changamoto ya maji yenye chumvi, hali inayofanya kuwa vigumu kuyatumia moja kwa moja kwa matumizi ya binadamu bila kuyasafisha.

Hivyo, uwekezaji katika teknolojia ya kusafisha majichumvi (desalination) unatajwa kuwa suluhisho muhimu kwa maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Amesema mradi huo utaondoa adha ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi katika kituo hicho cha afya, hali iliyokuwa ikiathiri utoaji wa huduma kwa wagonjwa na hata usafi wa mazingira ya hospitali.

“Upatikanaji wa maji safi na salama katika kituo hiki utarahisisha utoaji wa huduma za afya na kuboresha mazingira ya tiba kwa wagonjwa. Tunathamini juhudi hizi za Serikali na Dawasa,” amesema Mtambule.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo pia wameeleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema utawapunguzia gharama na muda waliokuwa wakitumia kutafuta maji safi kutoka maeneo ya mbali.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi pana za Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za maji mijini na vijijini, sambamba na kuimarisha miundombinu ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama.