CAG Zanzibar kutumia AI kuimarisha ukaguzi wa fedha za umma

Unguja. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Zanzibar imeingia makubaliano na taasisi za ukaguzi kutoka India kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wake katika matumizi ya akili unde (AI), sayansi ya data na usalama wa mitandao, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa fedha na mali za umma.

Makubaliano hayo yanahusisha Taasisi za Juu za Ukaguzi (SAI) za Zanzibar na India na mafunzo yatatolewa kwa awamu mbili kwa ufadhili wa India.

Awamu ya kwanza inatarajiwa kuanza Juni 2026 katika IIT Madras Zanzibar, ikiwahusisha watumishi 45, huku awamu ya pili ikifanyika India kwa watumishi 30 watakaofanya vizuri zaidi.

Kwa mujibu wa mpango huo, ndani ya kipindi cha miaka miwili jumla ya watumishi 185 wanatarajiwa kuwa wamepatiwa mafunzo hayo ya kisasa.

Akizungumza leo Jumamosi, Aprili 18, 2026 baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dk Othman Abas Ali, amesema hatua hiyo itaiwezesha taasisi hiyo kuendesha ukaguzi kwa kutumia mifumo ya kidijitali yenye ufanisi zaidi.

Amesema pamoja na Zanzibar kuanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika utoaji wa huduma za Serikali, bado baadhi ya shughuli zinafanyika kwa njia za kawaida, hali inayopunguza ufanisi.

“Tunatambua India imepiga hatua kubwa katika teknolojia. Sisi tumeshafikia hatua ya pili ya matumizi ya mifumo, lakini bado tunakabiliwa na changamoto za akili bandia (unde), usalama wa mtandao na uchambuzi wa data,” amesema Dk Abas.

Amesema baada ya kupata mafunzo hayo, ofisi hiyo inalenga kupata vyeti vya viwango vya kimataifa (ISO), hatua itakayoiwezesha kufanya ukaguzi katika taasisi za kimataifa zikiwamo zile za Umoja wa Mataifa, tofauti na ilivyo sasa ambapo inajikita zaidi katika taasisi za ndani na baadhi ya balozi.

Ofisa Mkaguzi Mwandamizi kutoka ofisi ya CAG India, Sadhashiv Ranade, amesema mafunzo ya awali ya wiki mbili yatatolewa Zanzibar na kuhitimishwa kwa utoaji wa vyeti, kabla ya washiriki bora kuendelea na mafunzo ya juu India katika taasisi za IIT Madras Chennai na iCISA Noida.

Amesema kupitia mafunzo hayo, CAG Zanzibar itakuwa na uwezo wa kutumia akili unde katika ukaguzi, kufanya uchambuzi mpana wa data na kubaini upungufu uliopo katika mifumo ya Tehama ya Serikali.

“Lengo ni kuongeza thamani ya ukaguzi unaofanyika tayari na kuboresha zaidi kwa kutumia teknolojia za kisasa, pamoja na kuimarisha usalama wa mifumo dhidi ya udukuzi,” amesema Ranade.

Amesema mafunzo hayo pia yatawajengea uwezo maofisa kutambua vihatarishi vya kiusalama katika mifumo ya Serikali na kusaidia kuzuia ubadhirifu wa mali za umma.

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mifumo ya Tehama ofisi ya CAG Zanzibar, Juma Mohamed Juma amesema kasi ya maendeleo ya teknolojia imeongeza changamoto mpya, hususan mashambulizi ya mtandao yanayoweza kuhatarisha rasilimali za umma.

“Tutatumia ujuzi huu kufanya ukaguzi wa mifumo, kubaini hatari zilizopo na kuhakikisha mifumo ya Serikali inakuwa salama na yenye ufanisi zaidi,” amesema.

Kwa mujibu wa wataalamu, matumizi ya akili unde na sayansi ya data katika ukaguzi yanatarajiwa kuongeza uwazi, kupunguza makosa ya kibinadamu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma, hatua inayokwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali duniani.