Dar es Salaam. Ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT) katika njia ya Gongo la Mboto umefikia asilimia 99, huku mipango ikiendelea ya kujenga kituo kingine cha mabasi ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Akizungumza na Mwananchi juzi kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa ujenzi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Frank Mbilinyi, amesema kazi iliyobaki ni asilimia moja tu inayohusisha ufungaji wa mifumo ya umeme katika vituo pamoja na taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara.
Mradi huo wa kimkakati wa Serikali unatekelezwa kwa awamu sita, huku Tanroads ikisimamia ujenzi wa miundombinu.
Awamu ya tatu, ikiwamo Barabara ya Nyerere (Gongo la Mboto) inatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa DUTIP, kwa gharama ya Dola 148.2 milioni za Marekani katika mradi huo wenye urefu wa kilometa 23.3 na vituo 32 vya abiria.
Aidha, kuna eneo maalumu la kuegesha magari madogo 200 katika kituo kikuu cha Gongo la Mboto Mwisho.
Awamu hiyo inaanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mitaa ya Azikiwe na Maktaba, barabara za Bibi Titi na Nyerere, hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuendelea hadi Gongo la Mboto.
Tawi jingine linaanzia kituo cha Kariakoo Gerezani kupitia Lindi, Shaurimoyo na Uhuru hadi Buguruni, kisha kuungana na Barabara ya Nelson Mandela na Nyerere katika makutano ya Tazara.
Akielezea hatua ya ujenzi, Mbilinyi amesema: “Tunatarajia kukamilisha kazi zilizobaki za mifumo ya umeme ifikapo mwisho wa Aprili.”
Kutokana na hatua hiyo, amewataka wananchi kujiandaa kuanza kutumia huduma hiyo hivi karibuni, akibainisha kuwa hata sasa baadhi ya magari ya kawaida yameanza kutumia barabara hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Said Tunda, amesema huduma zitaanza baada ya kukabidhiwa rasmi barabara hiyo.
Ameongeza kuwa bado kunahitajika kukamilika kwa mageti janja ya kukatia tiketi, karakana ya mabasi, pamoja na kituo kinachotarajiwa kujengwa ndani ya uwanja wa ndege.
Mbilinyi amesema ujenzi wa karakana katika eneo la zamani la kiwanda cha nguo cha Kili, Gongo la Mboto Mwisho, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
Vilevile, ujenzi wa kituo cha mabasi ndani ya uwanja wa ndege utaenda sambamba na karakana hiyo, tayari
“Ujenzi wa karakana na kituo cha uwanja wa ndege hauzuii kuanza kwa huduma kwenye barabara kuu mara itakapokamilika.”
Kwa mujibu wa Dart, mabasi 200 yanatarajiwa kutoa huduma katika njia hiyo.
Kampuni ya Uendeshaji Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) tayari imeteuliwa kutoa huduma na imeshaingiza nchini mabasi 100 mapya yanayotumia gesi.
Msemaji wa Udart, Gabriel Kapinga amesema wana mpango wa kuongeza mabasi zaidi kadri mahitaji yatakavyoongezeka.
Baadhi ya wakazi wa Gongo la Mboto na maeneo jirani wamesema wana hamu ya kuona huduma zikianza haraka ili kupunguza changamoto za usafiri.
Mkazi wa Gongo la Mboto Mwisho, Ruta Kabigi amesema usafiri wa kwenda katikati ya jiji umekuwa mgumu hasa asubuhi, hali inayowalazimu kutumia bajaji au bodaboda kwa gharama kubwa.
Naye Zena Kassim wa Kisarawe amesema kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza gharama za mafuta kwa wanaotumia magari binafsi.
“Watu wengi wataacha magari yao na kutumia mwendokasi hadi mjini,”amesema.
Leonard Tarimo, amesisitiza umuhimu wa ubora wa huduma:“Tunatarajia huduma bora ili kuepuka malalamiko kama yaliyowahi kujitokeza awamu ya kwanza.”
