KUNA mstari mwembamba sana umetenganisha furaha ya ubingwa, si Ligi Kuu Bara wala Ligi Kuu England. Hivi sasa kuna mbio za wakubwa huko zikienda kwa kasi ya treni ya SGR.
Tukiwa miezi hii ya mwishomwisho kumalizia msimu wa 2025-2026, kuna maswali yamebaki ya nani atakuwa bingwa, huku timu mbili zikionekana kuwa karibu zaidi na mafanikio hayo.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Yanga inakimbizwa na Simba, tofauti yao ya pointi ni saba, huku nazo zikiwa na mechi moja ya kuwakutanisha na kuamua jambo fulani.
Yanga hesabu zao hivi sasa zipo katika mechi 11 zilizobaki kukamilisha kile walichokianza msimu huu katika kubeba ubingwa wa ligi mara ya tano mfululizo.
Katika hesabu hizo za mechi 11, zipo nane za karibuni ambazo zinaisogeza karibu zaidi na ubingwa kabla ya kukutana na Azam katika mechi ya tisa.
Mechi hizo nane ambazo Yanga inakabiliana nazo kuanzia sasa inaanza na Simba, Mei 3 mwaka huu ikiwa ugenini baada ya awali kuwa mwenyeji na matokeo kuwa 0-0.
Nafuu ya Yanga inakuja kutokana na kuwa na muda mwingi wa kujiandaa na mechi hii kulinganisha na wapinzani wao Simba ambao Jumamosi wakimalizana na Namungo ugenini, ndipo wataisubiri Yanga.
Lakini hapo katikati, timu zote hizo zitakuwa Zanzibar kushiriki Kombe la Muungano kuanzia Aprili 21 hadi 29 mwaka huu.
Michuano hiyo pengine wataitumia kama sehemu ya maandalizi kuelekea Kariakoo Dabi.
Katika mechi nane zijazo ambazo Yanga ikishinda zote itakusanya pointi 24 na kufanya jumla kuwa 71, zitaisogeza karibu zaidi kwani itazifanya timu zingine kushindwa kufika hapo hata zikishinda mechi zote zilizobaki, ukiiondoa Simba ambayo yenyewe inaweza kufika 72.
Kwa mechi 12 ambazo Simba imebakiwa nazo, ikishinda zote itamaliza msimu na pointi 75, hivyo inachopaswa ni kutodondosha pointi kuanzia sasa huku pia kuiombea mabaya Yanga iteleze.
Yanga mechi 11 zilizobaki, ikishinda zote itamaliza msimu na pointi 80, lakini hata ikitokea imepoteza moja, bado itatetea ubingwa kwa kukusanya pointi 77.
Ratiba inaonesha Yanga katika mechi hizo nane zijazo itacheza dhidi ya Simba (ugenini), KMC (ugenini), Coastal (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani), Namungo (nyumbani), Mashujaa (ugenini) na Fountain Gate (ugenini).
Katika ratiba ya mechi hizo nane, ni dhidi ya Simba pekee ambayo Yanga ilitoka sare zilipokutana duru la kwanza, huku zingine hizo ikizichapa, hivyo kuna uwezekano pia ikaendeleza ubabe wake marudiano.
Simba yenyewe ili kuichelewesha Yanga isiwe bingwa mapema, mechi nane zijazo itacheza dhidi ya Namungo (ugenini), Yanga (nyumbani), JKT Tanzania (nyumbani), Tanzania Prisons (nyumbani), Mashujaa (ugenini), Coastal Union (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani) na Pamba Jiji (nyumbani).
Katika duru la kwanza, Simba ilitoka sare tatu dhidi ya Yanga, Pamba Jiji, Dodoma Jiji, ikishinda tano mbele ya Namungo, JKT Tanzania, Tanzania Prisons, Mashujaa na Coastal Union.
Katika kipindi kama hiki, timu zinapokwenda ugenini zinachukua tahadhari kubwa sana kwani zinapitia wakati mgumu kuliko inapokuwa nyumbani.
Hilo linazifanya Yanga na Simba zinapokuwa nje ya Dar, kuwa makini sana kwani zikiwa jijini Dar zinakuwa na mipango mingi ya ndani ya uwanja kutokana na viwanja kuruhusu kucheza soka lao pendwa.
Kwa maana hiyo, katika mechi zilizobaki, Yanga itakwenda nje ya Dar kucheza mechi tatu wakati Simba ni mechi tano.
Mechi tano za nje ya Dar kwa Simba ni dhidi ya Namungo (Lindi), Mashujaa (Kigoma), Coastal Union (Tanga), Mbeya City (Mbeya) na Mtibwa Sugar (Dodoma).
Yanga nje ya Dar itacheza dhidi ya Dodoma Jiji (Dodoma), Mashujaa (Kigoma) na Fountain Gate (Arusha).
Rekodi zinaonesha msimu huu Yanga imecheza mechi nane nje ya Dar ikitoka sare tatu dhidi ya TRA United, Mtibwa Sugar na Mbeya City, ikizifunga Pamba Jiji, Singida Black Stars, Tanzania Prisons, Coastal Union na Namungo.
Simba nje ya Dar msimu huu imecheza mechi saba ikishinda tatu dhidi ya Singida Black Stars, Fountain Gate na Tanzania Prisons, haijapoteza huku ikitoka sare nne dhidi ya Pamba Jiji, TRA United, Dodoma Jiji na Yanga.
Yanga na Simba katika mechi zilizobaki, zinakutana na wapinzani saba wanaofanana, kwa maana ya zile timu itakazokutana nazo Yanga, pia itacheza dhidi ya Simba. Pia ndani yake kuna mechi yao wenyewe wakubwa. Wapinzani hao ni Namungo, JKT Tanzania, Mashujaa, Coastal Union, Dodoma Jiji, Singida Black Stars na KMC.
Ratiba ya Simba itakuwa hivi; Namungo vs Simba, Simba vs Yanga, Simba vs JKT Tanzania, Mashujaa vs Simba, Coastal vs Simba, Simba vs Dodoma Jiji, Simba vs Singida na Simba vs KMC.
Yanga itakuwa hivi; Simba vs Yanga, KMC vs Yanga, Yanga vs Coastal, Dodoma Jiji vs Yanga, Yanga vs Singida, Yanga vs Namungo, Mashujaa vs Yanga na JKT vs Yanga.
Pale England ndani ya Ligi Kuu, Arsenal inakimbizwa kwa ukaribu na Manchester City, hivi sasa tofauti ya pointi baina yao ni sita, huku wikiendi hii zinapokwenda kukutana, kuna jambo hapo la uamuzi huenda likatokea ingawa safari haitaishia hapo.
Kwa sasa Arsenal ikiwa imeiacha Man City kwa pointi sita, pia City ina mchezo mmoja mkononi.
Mbio za ubingwa hazitaisha bila kujali kitakachotokea wakati Manchester City watakapowakaribisha Arsenal Jumapili hii. Lakini matokeo ya mechi hiyo yatakuwa na mchango mkubwa sana kuamua nani atatwaa taji.
Pep Guardiola ameita mchezo huo fainali. Arsenal, ambao kwa sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi sita, wanajua ushindi utakuwa kama kumaliza kazi kabisa. Sare pia inaweza kuwatosha. Lakini wakipoteza, basi City watakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushinda ubingwa.
Kuna mechi kubwa, halafu kuna mechi kubwa zaidi. Ingawa City bado wanashiriki FA Cup na Arsenal wapo kwenye Champions League, hakuna shaka hii ndiyo mechi kubwa iliyobaki kwa pande zote msimu huu.
Ingawa dhana ya ‘big six’ (Arsenal, Chelsea, Liverpool, Man City, Manchester United na Tottenham) inaweza kuwa imepitwa na wakati, bado hutumika kupima nguvu. Arsenal wamepoteza mechi mbili tu kati ya tisa dhidi ya timu hizo (ushindi 4, sare 3). City wana rekodi sawa kabisa (ushindi 4, sare 3, kupoteza 2), hata mabao waliyofunga (15) na kufungwa (9) yanafanana. Hivyo ni bora kuangalia rekodi zao dhidi ya kila mmoja.
Arsenal wanaweza kufarijika na rekodi yao ya hivi karibuni dhidi ya City. Baada ya kupoteza mechi 12 mfululizo, walishinda 1-0 Oktoba 2023, na sasa hawajapoteza katika mechi tano za mwisho za ligi dhidi ya City (ushindi 2, sare 3).
Katika mechi ya kwanza msimu huu, City walionekana kushinda baada ya bao la mapema la Haaland, lakini Martinelli alisawazisha dakika za mwisho na kufanya sare ya 1-1. City wameshinda mechi moja tu kati ya saba za mwisho dhidi ya Arsenal mashindano yote, ingawa ushindi huo ulikuwa fainali ya Kombe la Ligi mwezi uliopita. Arsenal wanaonekana kupoteza nguvu mwishoni mwa msimu.
Wameshinda mechi moja tu kati ya tano zilizopita, wamepoteza tatu, na wametolewa kwenye mashindano mawili ya vikombe. Kuna dalili za uchovu na presha ya mbio za ubingwa.
Kwa upande mwingine, City wako kwenye kiwango bora, wameshinda Liverpool, Chelsea na Arsenal kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi tatu.
Historia pia haiko upande wa Arsenal mwezi Aprili, ambapo mara nyingi wamekuwa wakidorora.
City wamekuwa imara sana Etihad. Hawajapoteza mechi ya nyumbani tangu mwanzo wa msimu. Wamefunga angalau mabao mawili katika mechi 12 kati ya 14 za nyumbani.
Kwa upande wa Guardiola, ameifunga Arsenal mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine yoyote.
