Chadema kusaka mrithi wa Wenje Kanda ya Victoria

Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Victoria kimeanza mchakato wa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa kanda iliyokuwa ikishikiliwa na Ezekiel Wenje kabla ya kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2025.

Mbali na nafasi hiyo, chama hicho pia kinatarajia kujaza nafasi nyingine za uongozi ikiwamo ya Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Katibu wa Baraza la Vijana (Bavicha) na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mwanza, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Peter Machoko kabla ya kuondoka na wanachama 170 Mei 2, 2025 na kujiunga na CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Aprili 18, 2026 katika ofisi za kanda hiyo jijini Mwanza, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi amesema mchakato huo utaanza rasmi kwa kutangazwa kwa uchaguzi wa nafasi hizo.

Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi akizungumza na wanachama wa chama hicho leo Aprili 18, 2026 wakati wa mkutano wa kanda hiyo uliofanyika katika ofisi za Kanda ya Victoria, mkoani Mwanza.

“Uchaguzi huu utasimamiwa na kamati tendaji ya kanda, na muda wowote tutatangaza ratiba rasmi itakayotoa mwongozo kuanzia ngazi ya mkoa, jimbo, wilaya, kata hadi matawi ya chama,” amesema Obadi.

Amesema kamati ya kanda itakutana Aprili 28 na 29, 2026 na itatoa maelekezo na maazimio ya utekelezaji wa mchakato huo kwa wanachama.

Katika hatua nyingine, Obadi amesema chama hicho kitaendelea kuweka nguvu katika juhudi za kuhakikisha Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, anaachiwa huru.

Ameongeza kuwa kipaumbele kingine ni kufungua ofisi za chama katika mikoa ya Kanda ya Victoria, inayojumuisha Mwanza, Geita na Kagera, huku ofisi ya kanda hiyo jijini Mwanza ikifunguliwa rasmi leo.

Kuhusu uendeshaji wa chama, Obadi amesema kwa sasa Chadema itategemea mchango wa wanachama kupitia mfumo wa “tone tone” kutokana na kukosa ruzuku ya Serikali.

“Kwa sasa tunajiendesha kwa nguvu ya wanachama. Huu ni wakati wa kila mwanachama kushiriki kuchangia maendeleo ya chama,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa kutoka Mkoa wa Mwanza, Salma Kasanzu ametangaza nia ya kuachia nafasi ya Katibu wa Bawacha Mkoa na kuwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi hiyo.

“Nawaomba wanawake mjitokeze kwa wingi kugombea nafasi hii na kushiriki kukijenga chama,” amesema Kasanzu.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kanda hiyo, Upendo Mwamsoja amesema kurejea kwa shughuli za kisiasa kumeongeza ari kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho.

“Wananchi wanatupenda kwa misimamo yetu, na sasa tunapata matokeo ya kile tulichokisimamia,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Charles Chichibela amesema chama hicho kiko tayari kutumia fursa ya kurejea kwa shughuli za kisiasa kuimarisha uhai wake katika ngazi zote.

“Tutatumia fursa hii kuamsha chama upya na kuimarisha shughuli zake kuanzia ngazi ya chini hadi juu,” amesema.

Chadema ilikuwa imezuiwa kufanya shughuli za kisiasa kuanzia Juni 10, 2025 kwa siku 310, kabla ya kuruhusiwa tena Aprili 15, 2026.