Pwani. Bagamoyo Mwenge wa Uhuru 2026 leo Jumamosi Aprili 18, 2026 umekabidhiwa rasmi kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Pwani katika hafla iliyofanyika Bagamoyo, huku viongozi wakisisitiza uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Mwenge huo umekabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ambapo katika mbio zake mkoani Pwani utakimbizwa umbali wa zaidi ya kilomita 1,000 ukipitia wilaya saba na halmashauri tisa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kunenge amesema Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi 68 yenye thamani ya zaidi ya Sh200 bilioni, ambapo miradi 23 itawekewa mawe ya msingi, 21 itazinduliwa na miradi 24 itakaguliwa.
Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha miradi yote inayopitiwa na Mwenge inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
“Miradi yetu iko vizuri, lakini pia tumejipanga kuhakikisha taarifa zote zinazohitajika zinapatikana kwa urahisi,” amesema Kunenge.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onde amesema halmashauri zote zinapaswa kuweka wazi taarifa za miradi ili kurahisisha ukaguzi na kubaini changamoto pindi Mwenge unapofika kwenye vituo vya miradi.
“Na safari hii mwenge utakimbizwa na wananchi wenyewe walioko maeneo husika hivyo naomba Mkuu wa Mkoa wa Pwani tuandalie watu watakaokuwa wanaushika mwenge na kuukimbiza huku viongozi tukiwa tunawasimamia,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa Bagamoyo akiwemo Amiry Juma na Abeda Shabani, wametaka hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watu watakaobainika kudhoofisha miradi ya maendeleo kwa ubadhirifu, ubora hafifu au matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.
Wananchi hao wamesema ukaguzi wa Mwenge uwe chachu ya kubaini dosari na kuwawajibisha wahusika, badala ya kuwa shughuli ya kawaida isiyoleta matokeo kwa waliokiuka taratibu.
Naye Joshua Samuel amesema kuwa seriikali inapaswa kuweka utaratibu wa kuwaajibisha watendaji wanaobainika kudhoofisha miradi ya maendeleo kwa makusudi kwakuwa wanasababisha jamii kukosa huduma zinazostahili.
“Ukaguzi wa miradi ya maendeleo ulete matokeo chanya hasa inapobainika mtu amefuja pesa za miradi inayogharimiwa na pesa za umma ili kuwezesha watendaji kutekeleza majukumu yao kikamilifu,” amesema.
