Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewaachia huru waendesha bodaboda wawili waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa na uzito wa kilo 150.11.
Walioachiwa huru ni Isihaka Ramadhani na Mikidadi Shabani ambao walidaiwa kukutwa na dawa hizo za kulevya zilizokuwa kwenye mifuko saba katika kituo cha mabasi cha Mlandizi, Novemba 6, 2024, katika eneo la Mlandizi, wilayani Kibaha, mkoa wa Pwani.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 101/2026 ilikuwa ikisikilizwa na Jaji Sedekia Kisanya, aliyetoa hukumu hiyo Aprili 16, 2026, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Jaji Kisanya amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imeridhika kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi yao bila kuacha shaka, na kuwa kulikuwepo na mapungufu makubwa katika ushahidi yaliyoifanya Mahakama ishindwe kuunganisha moja kwa moja washtakiwa na kosa hilo.
Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo kadhaa, ikiwemo ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyothibitisha kuwa dawa hizo zilikuwa bangi.
Pia uliwasilisha pikipiki mbili zilizodaiwa kutumika kusafirisha dawa hizo pamoja na cheti cha ukamataji.
Shahidi wa pili, ambaye ni ofisa wa polisi, alidai kuwa wakiwa katika doria ya kawaida walipokea taarifa za siri kuwa kuna watu walikuwa wakipakia mizigo katika kituo hicho cha mabasi ambayo ilitiliwa shaka.
Baada ya taarifa hizo, akiwa na polisi wenzake, waliongozana hadi kituoni hapo ambapo walikuta wanaume hao wawili wakiwa na mifuko saba iliyokuwa na majani makavu yaliyoshukiwa kuwa ni bangi, kisha wakawakamata na kuwapeleka kituo cha polisi.
Hata hivyo, katika uchambuzi wake, Mahakama ilibaini kuwa ingawa ni kweli bangi hiyo ilikamatwa na kuthibitishwa kitaalamu, bado kulikuwa na shaka juu ya uhusiano wa moja kwa moja kati ya washtakiwa na dawa hizo.
Mahakama ilieleza kuwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hasa ule wa askari aliyefanya ukamataji (shahidi wa pili), ulikuwa na mapungufu na kutofautiana katika maelezo muhimu.
Jaji amesema katika hatua moja shahidi huyo alidai washtakiwa walikiri kuwa mizigo ilikuwa yao, huku katika taarifa yake ya awali akieleza kuwa walidai mizigo hiyo ilikuwa ya mwanamke aliyewaita kuwasaidia kusafirisha.
Tofauti hiyo ilitafsiriwa na Mahakama kama dosari inayogusa kiini cha kesi, hasa ikizingatiwa kuwa washtakiwa walikuwa bodaboda ambao kazi yao ni kubeba abiria na mizigo bila lazima kujua kilichomo ndani.
Jaji amesema Mahakama ilibaini kuwa kulikuwa na ushahidi unaoashiria mizigo hiyo ilishushwa kutoka basi la abiria, jambo lililohitaji uchunguzi wa ziada kubaini mmiliki halisi wa mizigo hiyo, lakini hatua hiyo haikufanyika.
Katika utetezi wao, washtakiwa walidai kuwa walikuwa wameitwa na mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mama Richie ili wamchukue pamoja na mizigo yake kutoka stendi ya mabasi.
Walieleza kuwa walikamatwa kabla hata hawajaanza kubeba mizigo hiyo, na kwamba mwanamke huyo alitoweka ghafla.
Mahakama iliona maelezo hayo hayawezi kupuuzwa kirahisi, hasa kutokana na ukosefu wa ushahidi unaoonyesha kuwa washtakiwa walikuwa na ufahamu kuwa mizigo hiyo ilikuwa na dawa za kulevya.
Jaji Kisanya amesema upande wa mashtaka ulishindwa kuonyesha mnyororo madhubuti wa ulinzi wa vielelezo (chain of custody), kuanzia vilipokamatwa hadi vilipofikishwa maabara na baadaye mahakamani.
Alibainisha kuwa kulikuwa na mkanganyiko kuhusu namna mifuko hiyo ilivyofungwa na kuhifadhiwa, pamoja na nani hasa aliyekuwa na jukumu la kuitunza katika vipindi tofauti.
Aidha, kutokuwapo kwa ushahidi kutoka kwa mhifadhi mkuu wa vielelezo kulizidisha mashaka juu ya usalama na uhalisia wa vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani.
“Katika kesi za jinai, mzigo wa uthibitisho upo kwa upande wa mashtaka na lazima uthibitishwe bila kuacha shaka yoyote. Pale ambapo kuna shaka, ni lazima imuendee mshtakiwa,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.
Kutokana na dosari hizo, Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha bila shaka kuwa washtakiwa walihusika na usafirishaji wa dawa hizo.
Kutokana na dosari hizo, Mahakama iliwakuta washtakiwa wote wawili hawana hatia na kuwaachia huru.
