Iringa. Jumla ya makada 18 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamechukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea Jimbo la Isimani, mkoani Iringa, wakilenga kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.
Imeelezwa kuwa idadi hiyo inajumuisha wanamume 16 na wanawake wawili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa, Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Sure Mwasanguti amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulianza jana na kuhitimishwa leo kwa mafanikio.
Mwasanguti amesisitiza kuwa hatua inayofuata ni kesho kufanyika kwa uchaguzi wa kura za maoni katika kata zote za jimbo hilo, ambapo wanachama watapata nafasi ya kuwachagua wagombea wanaowakubali kabla ya mchakato wa uteuzi wa mwisho kufanyika.
Mwasanguti ametaja majina ya wanachama 18 waliochukua na kurejesha fomu hizo kuwa ni Fred Ngajilo (Vunjabei), Festo Kiswaga, Asakwe Widambe, Arif Abri, Sebastian Kiyoyo, Tumaini Msowoya, Watende Kiyagi, Lazaro Ngwira, David Komba, Thobias Mwilapwa, Titho Cholobi, Emmanuela Mtatifikolo, Claudio Nzwaga, Josephat Msambwa, Elias Kazikuboma, Egidy Mkolwe, Abdallah Lusasi na Tedson Ngwale.
