Maisha utotoni yanavyoathiri mapenzi ukubwani

Dar es Salaam. Watu wengi huamini kuwa uchaguzi wa mwenza wa maisha ni matokeo ya mvuto wa kimwili, bahati au mazingira ya sasa ya kijamii.

Hata hivyo, ukweli unaoibuliwa na wataalamu wa saikolojia ya uhusiano unaonyesha kuwa chaguo hilo huanza kuumbwa mapema sana, katika miaka ya utotoni.

Makala kuangazia vyanzo mbalimbali vya kimtandao na vitabu vya wataalamu, inaweza namna maisha anayopitia mtu utotoni yanavyoweza kuathiri sio tu uchaguzi wa mwenza lakini namna ya kuishi ndani ya uhusiano.

Utoto si tu kipindi cha kucheza na kukua kimwili, bali ni hatua ya kwanza ambapo binadamu hujifunza maana ya kupendwa, kuachwa, kusikilizwa au kupuuzwa.

Ndani ya uzoefu huu wa awali, mtoto hujenga msingi wa namna atakavyopenda na kuchagua mwenza ukubwani.

Mwanasaikolojia wa Uingereza, John Bowlby, alisisitiza kuwa uhusiano wa awali kati ya mtoto na mlezi wake una athari ya kudumu katika maisha ya kihisia ya mtu.

Akisema mtoto hujifunza kujielewa kupitia uhusiano wake na mlezi. Katika maandiko yake, anaeleza kwa kauli yenye uzito mkubwa: “Kile ambacho mtoto hawezi kumwambia mama yake, hawezi pia kukisema ndani ya nafsi yake.”

 Kauli hii inaonyesha kuwa mtoto anayekosa mazingira salama ya kueleza hofu, huzuni au mahitaji yake hukua akiwa na ugumu wa kujitambua na kujieleza katika uhusiano wa utu uzima.

Mtoto anayelelewa katika mazingira ya upendo thabiti, uthabiti wa kihisia na uangalizi hujifunza kuwa dunia ni mahali salama na uhusiano unaweza kuaminika.

Kinyume chake, mtoto anayekulia katika mazingira ya vurugu, kutelekezwa au kutotabirika hujenga mtazamo kuwa upendo ni kitu cha kuogopa au kupigania kwa maumivu.

 Mtazamo huu huendelea hadi utu uzima na mara nyingi hujitokeza katika aina ya mwenza anayemvutia mtu.

 Mara nyingi si kwa sababu mwenza huyo ni bora, bali kwa sababu anafanana na uzoefu wa kihisia ambao moyo tayari unaufahamu.

Nadharia ya ‘ mshikamano kimapenzi’

Katika kitabu Attached, waandishi Amir Levine na Rachel Heller wanaendeleza nadharia ya ‘attachment’ (mshikamano) kwa kuielekeza moja kwa moja katika uhusiano wa kimapenzi kwa watu wazima.

Wanaeleza kuwa binadamu hujenga mitindo ya kushikamana tangu utotoni, na mitindo hiyo huathiri namna wanavyopenda, wanavyogombana, na muhimu zaidi, wanavyowachagua wenza wao.

Wanaonyesha kuwa mitindo hii si nadharia za kufikirika, bali ni nguvu halisi zinazoendesha mahusiano. Wanaandika: “Mitindo ya attachment si dhana za kinadharia tu; inaathiri jinsi tunavyopenda, jinsi tunavyogombana, na jinsi tunavyowachagua wenza wetu.”

Kauli hii inaweka wazi kuwa uchaguzi wa mwenza si tukio la bahati nasibu, bali ni matokeo ya historia ya kihisia iliyojengwa tangu utotoni.

Kwa mfano, mtu aliyekulia katika mazingira yenye upendo usiotabirika anaweza kukua akiwa na hofu ya kutelekezwa.

Akiwa mtu mzima, anaweza kuvutiwa na mwenza asiyejitolea kihisia, kwa sababu uhusiano huo unachochea hisia alizozizoea, kusubiri, kuomba upendo, na kuishi katika hofu ya kuachwa.

Ingawa uhusiano wa aina hii huleta maumivu, mara nyingi huonekana kuwa wa kawaida kwa sababu unafanana na uzoefu wa awali wa maisha.

Hii inaeleza kwa nini baadhi ya watu hujikuta wakirudia uhusiano wenye mifumo ile ile ya maumivu, licha ya kuapa kubadilika.

Bila ufahamu wa ndani, mtu anaweza kudhani tatizo ni bahati mbaya au laana ya mapenzi. Lakini kwa mtazamo wa nadharia hii, tatizo mara nyingi ni ramani ya kihisia iliyojengwa utotoni ambayo bado inaongoza uamuzi wa sasa.

Kubadilisha mwelekeo wa uchaguzi

Harville Hendrix, mwandishi wa Kitabu kiitwacho: Getting the Love You Want, anaeleza kuwa mara nyingi binadamu huwachagua wenza wanaoamsha majeraha yao ya utotoni kwa matumaini ya ndani kwamba safari hii wataweza kuyaponya.

Kwa mujibu wa nadharia yake, mvuto wa kimapenzi mara nyingi hutokana na kufanana kwa mwenza na walezi wa awali, hasa katika maeneo ya maumivu.

Hendrix anaandika kwa maneno yenye kutafakari kwa kina: “Tunazaliwa katika uhusiano, tunaumizwa katika uhusiano, na tunaweza kupona kupitia uhusiano.” Tafsiri hii inaonyesha kuwa uhusiano si tu chanzo cha majeraha, bali pia yana uwezo wa kuwa tiba.

Changamoto hutokea pale ambapo watu hawatambui kwa nini wanavutiwa na aina fulani ya watu, na hivyo kuendelea kurudia maumivu yale yale bila mabadiliko.

Kwa mtazamo huu, tatizo si kuchagua mwenza mbaya pekee, bali ni kukosa ufahamu wa kile kinachoendesha uchaguzi huo.

Ufahamu wa historia ya utotoni humsaidia mtu kujiuliza maswali ya msingi: Kwa nini ninahisi upweke hata nikiwa kwenye uhusiano? Kwa nini ninavutiwa na watu wasionipa usalama wa kihisia? Maswali haya huanza safari ya kuvunja mzunguko wa maumivu.

Dk Sue Johnson, mtaalamu wa tiba za kihisia anasisitiza kuwa hitaji la msingi katika uhusiano wa watu wazima ni usalama wa kihisia.

Katika kitabu chake Hold Me Tight, anaandika: “Tumeumbwa kimaumbile kuungana; upendo si anasa, ni hitaji la msingi.” Tafsiri hii inaondoa dhana kuwa kuhitaji ukaribu ni udhaifu. Badala yake, inaonyesha kuwa tamaa ya kupendwa na kuhakikishiwa ni sehemu ya asili ya binadamu.

Kwa mujibu wa DK Johnson, matatizo mengi ya uhusiano hayatokani na ukosefu wa mapenzi, bali na hofu ya kupoteza uhusiano au kukataliwa, hofu ambazo mara nyingi zina mizizi yake utotoni.

Pale mtu anapojifunza kuelewa na kudhibiti hofu hizi, anaanza kuchagua wenza kwa msingi wa usalama na heshima, si kwa msingi wa majeraha ya zamani.

Kwa jumla, mawazo ya waandishi hawa yanaonyesha kuwa kubadilisha uchaguzi wa mwenza kunahitaji safari ya ndani ya kujitambua.

Haiishii kwenye kuamua kubadilika, bali inahitaji kuelewa historia binafsi, kuomboleza kile ambacho hakikupatikana utotoni, na kujifunza njia mpya za kuwasiliana na kuunganika kihisia.

Habari njema ni kuwa mambo yanaweza kubadilika kupitia uhusiano salama, ushauri nasaha, na ufahamu wa ndani.

Katika ngazi ya jamii, mjadala huu unatukumbusha umuhimu wa malezi bora ya watoto.

Mtoto anayelelewa katika mazingira ya upendo, usalama na uthibitisho, hukua akiwa na uwezo wa kuchagua mwenza kwa uhuru na busara. Na kwa wale ambao hawakupata malezi hayo, ufahamu ni hatua ya kwanza ya kuandika upya hadithi ya uhusiano wao na kuvunja mizunguko ya maumivu ya kizazi hadi kizazi.