MABOSI wa Singida Black Stars, wameanza mchakato wa kumfuatilia beki wa kati wa Police FC ya Rwanda, Mghana Issah Yakubu ‘Varane’, ili kuipata saini yake mapema, baada ya menejimenti ya nyota huyo kudaiwa kufanya mazungumzo na timu kadhaa.
Beki huyo aliyezaliwa Oktoba 22, 1997, alijiunga na Police FC, Julai 1, 2024, akitokea Stade Malien ya Mali, ambapo kwa sasa inaelezwa huenda akaachana na kikosi hicho mwisho wa msimu huu wa 2025-2026, kwa ajili ya kupata changamoto mpya.
Chanzo kutoka ndani ya Singida, kimeliambia Mwanaspoti beki huyo ni miongoni mwa nyota wanaopigiwa hesabu za kusajiliwa ili kuongeza nguvu eneo hilo, baada ya Januari 2026, kuondoka kwa beki wa kati raia wa Ivory Coast, Anthony Tra Bi Tra.
“Miongoni mwa mapendekezo ya benchi la ufundi chini ya Meneja Mkuu, Papy Kimoto ni kuanza mchakato mapema wa usajili, ili kuepuka usumbufu, suala la Yakubu ni kweli lipo, ingawa, hakuna makubaliano yaliyofikiwa,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa taarifa huyo, alisema hadi sasa wapo wachezaji wanne ambao walitaka kuwasajili katika dirisha dogo la Januari 2026, ingawa, hawakufanikisha sajili zao kutokana na changamoto mbalimbali, hivyo, watarudi upya kuanza mazungumzo nao mapema.
Licha ya kucheza Stade Malien na sasa Police FC, ila beki huyo amewahi pia kuzicheza ES Bafing ya Ivory Coast na Dreams FC ya kwao Ghana, akitajwa ni miongoni mwa mabeki wazuri, wanaowaniwa na timu mbalimbali kubwa hapa nchini msimu ujao.