SERIKALI NA TNCC KUIMARISHA USHIRIKIANO KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI NA MASOKO YA KIMATAIFA

*****

Dar es Salaam 

 Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), Bw. Vicent Minja, kwa lengo la kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kurahisisha biashara na kukuza diplomasia ya uchumi.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Ulanga alisema Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na TNCC ili kuhakikisha taarifa sahihi na zilizopangwa kutoka sekta binafsi zinatumika kikamilifu katika kufungua masoko ya kimataifa.

“Tunataka kuona TNCC inakuwa kitovu cha taarifa za wafanyabiashara kwa kuandaa kanzidata yenye angalau makampuni yenye sifa na kuaminika, pamoja na utambuzi wa makampuni hayo yaliyo tayari kwa mauzo ya nje katika masoko ya EAC, SADC na AfCFTA,” alisema Balozi Ulanga.

Kwa upande wake, Bw. Minja alisema TNCC iko tayari kutekeleza majukumu hayo kwa kuandaa mifumo madhubuti itakayorahisisha ushiriki wa wafanyabiashara katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.

“Tutahakikisha tunatambua na kuandaa makampuni hayo pamoja na kuwaunganisha na Wakurugenzi Wakuu kutoka ndani na nje ya nchi kupitia majukwaa ya biashara, jambo litakaloongeza ushindani na fursa za uwekezaji,” alisema Minja.

Majadiliano hayo pia yaligusia umuhimu wa majukwaa ya kimkakati, ikiwemo Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Afrika Mashariki (EAC CEO Forum), linalotarajiwa kufanyika mapema Mei likiwakutanisha viongozi wa biashara kutoka sekta mbalimbali, ambapo TNCC imepangiwa jukumu la kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi.

Aidha, pande hizo mbili zilikubaliana kuharakisha maandalizi ya Hati ya Makubaliano (MoU), kuanzisha mfumo wa pamoja wa uratibu, na kuimarisha ushirikiano na balozi za Tanzania nje ya nchi ili kusaidia upatikanaji wa masoko, taarifa za biashara na uwekezaji.

Mkutano huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuiweka sekta binafsi mstari wa mbele katika utekelezaji wa ajenda ya diplomasia ya uchumi ya Tanzania, hususan katika kuongeza mauzo ya nje na kuvutia uwekezaji.

*Mwisho*