Pura: Tanzania ina kiwango cha gesi mara mbili zaidi ya malengo

Dodoma. Tanzania huenda ikawa mzalishaji mkubwa wa gesi kutokana na matokeo kuonyesha uwezo wa zaidi ya mara mbili kuliko ilivyotarajiwa.

Mkuu wa Kitengo cha ushirikishwaji wazawa na Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa mkondo wa juu wa Bahari (Pura), Charles Nyangi amesema uwezo wa kuzalisha gesi umekuwa zaidi ya mara mbili kwa ilivyotarajiwa.

Nyangi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 21, 2026 wakati akizungumza kwenye Banda la Pura katika maonyesho ya Wiki ya Nishati 2026 yanayoendelea viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema takwimu katika kisima kilichokamilika cha Mnazibay mkoani Mtwara zimeonyesha uzalishaji uko juu ya matarajio ya awali.

“Tumekamilisha uchimbaji wa kisima kimoja kule Mnazi bay, matarajio yalikuwa tupate futi za ujazo 20 Milioni lakini kisima kinatoa futi za ujazo 45 milioni, kwa hakika tupo mahali salama zaidi,” amesema Nyangi.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kwa sasa wanakamilisha uchimbaji wa kisima cha pili huku utafutaji zaidi ukiendelea akisema uhakika wa kupata gesi nyingi zaidi kutokana na dalili zinazojitokeza.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau, inaendelea kuwekeza zaidi katika utafutaji na uchimbaji wa geni na mwelekeo ni mzuri kwa siku za usoni.

Ameeleza namna Watanzania watakavyonufaika katika matumizi ya vifaa vinavyotumia gesi ikiwemo hata kwenye matumizi ya kupikia kwani kiwango kilichopo kinaonyesha kutosheleza.