Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imezitaka taasisi na mashirika ya umma kubadilika na kuanza kuchangamkia fursa zinazotolewa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya miaka mitatu kati ya DSE na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, yenye lengo la kujengeana uwezo, hususan kuongeza mitaji ya mashirika hayo.
Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Sanya, amesema moja ya jambo muhimu na lenye tija ni makubaliano hayo na DSE, na mchakato wake umeanza tangu Machi hadi kufikia hatua hiyo.
Amesema wamekubaliana mambo mengi, na kwamba ofisi hiyo ina majukumu mengi ya kusimamia mali zote za umma na taasisi za uwekezaji, na watahakikisha makubaliano hayo hayaishii kwenye makabati, bali utekelezaji wake unaanza mara moja.
“Tumekabidhiwa jukumu hili, na ni muda sahihi kutumia fursa ambazo DSE wanazo. Jambo kubwa ni elimu ya uelewa juu ya DSE na kutumia fursa zilizopo,” amesema Sanya.
Amesema Zanzibar, chini ya utawala wa Rais Hussein Mwinyi, mambo mengi yamefanyika, na kwa maana hiyo mashirika yanapaswa kubadilika ili kuendana na wakati na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo DSE.
“Hatuwezi kujifungia wenyewe Zanzibar. Taasisi nyingi za umma zinakopa sana kwenye benki, miradi inakuja, sehemu ya kwenda ni benki. Itafikia benki zitaishiwa, lakini kumbe kuna DSE,” amesema.
Msajili huyo wa Hazina amesema kati ya mashirika 17 ya umma Zanzibar, mashirika mawili pekee ndiyo yamejisajili DSE, na baada ya makubaliano hayo na utoaji wa elimu, wana imani yatabadilika na kuchangamkia fursa zaidi.
“Tuko tayari kushirikiana, na makubaliano haya hayataishia mezani. Baada ya kusaini, tutaanza utekelezaji haraka,” amesema.
Naye Mkuu wa Idara ya Mitaji Zanzibar, Mustafa Omary Abdallah, amesema makubaliano hayo yanakwenda kutoa fursa kwa taasisi wanazozisimamia kwa kujenga uelewa kwa taasisi hizo za umma juu ya DSE.
Abdallah, ambaye pia ni Wakili Mwandamizi wa Serikali ya Zanzibar, amesema makubaliano hayo yatawezesha kuangalia mitaji wanayoweza kuwekeza, huku DSE na Ofisi ya Msajili wa Hazina nao wataelewa vizuri nafasi ya DSE katika mitaji, kwani Serikali imewekeza fedha nyingi na lazima sasa zisimamiwe kwa tija.
Ili kuhakikisha makubaliano hayo ya miaka mitatu yanafanyika, amesema: “Tuna imani kabla ya kuja huku tumezungumza kuhusu nini tunakifanya ili utekelezaji uanze mara moja.”
Abdallah amesema: “Wananchi na wakuu wa mashirika ya umma watarajie mabadiliko makubwa, na wenyewe wawe tayari kubadilika, wasipokuwa tayari, watabadilishwa.”
Awali, Ofisa Mkuu wa Biashara wa DSE, Emmanuel Nyalali, amesema makubaliano hayo yatawezesha ushiriki wa taasisi na wananchi kutoka Zanzibar kuwa mkubwa: “Na sisi tuna kazi kubwa kuhamasisha ushiriki kwenye DSE, kwani wana haki ya kupata huduma na uwekezaji.”
Amesema kupitia makubaliano hayo, Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar itakuwa daraja kati ya DSE na wananchi, mashirika na taasisi zake, na wamejipanga kuhakikisha wanatoa ujuzi na uelewa mpana juu ya Soko la Hisa la Dar es Salaam na fursa zilizopo.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inavyopiga hatua kuimarisha uchumi wake, ushirikiano huu tulioingia tunaamini ni hatua kubwa kwa mashirika kujiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam,” amesema Nyalali.
