SMZ yatoa neno ushirikishwaji wananchi utafiti wa mafuta, gesi

Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikijiandaa kuanza shughuli za ukusanyaji wa takwimu za mafuta na gesi asilia kwa teknolojia ya 3D seismic survey, wananchi wa maeneo husika wameanza kupewa elimu ili waweze kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo.

Maeneo yatakayohusishwa na utafiti huo yanajumuisha ukanda wa kilomita za mraba 66 katika maeneo ya Paje, Bwejuu, Mtule na Jozani, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Hatua hiyo inafuatia kutiwa saini kwa mkataba wa mwaka mmoja Januari mwaka huu kati ya SMZ, kupitia Shirika la Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) na kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS) yenye makao makuu Oman, kwa ajili ya ukusanyaji wa data za kijiolojia za mfumo wa 3D.

Akizungumza jana Aprili 18, 2026 katika mkutano wa utoaji elimu kwa wananchi na wanafunzi wa Kijiji cha Paje uliofanyika Shule ya Paje, Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Othman Ali Maulid alisema ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha hilo.

“Ni lazima tutoe ushirikiano wa hali na mali ili Zanzibar yetu iweze kunufaika na rasilimali hizi kwa uhakika,” alisema.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kukusanya takwimu sahihi za kijiolojia kwa wakati, hatua itakayochangia kubaini uwepo wa mafuta na gesi asilia katika eneo hilo.

Maulid alibainisha kuwa endapo rasilimali hizo zitapatikana, wananchi wa Zanzibar watakuwa wanufaika wakubwa kupitia ongezeko la kipato na kuboreshwa kwa maisha yao.

Alisema mafanikio ya mradi huo ni mafanikio ya wananchi wote, akiwataka kuendelea kuiamini Serikali na kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha manufaa yanapatikana kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunashuhudia mabadiliko ya bei za mafuta duniani, hasa kutokana na migogoro ya kimataifa. Kama tutakuwa na rasilimali zetu, hali ya maisha itakuwa nafuu zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPDC, Mikidad Ali Rashid alisema utoaji wa elimu hiyo unalenga kuwafahamisha wananchi juu ya dhamira ya serikali ya kuendeleza utafutaji wa mafuta na gesi asilia visiwani humo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia (ZPDC), Mikidad Ali Rashid akizungumza na wananchi wakati wa kutoa elimu ya ukusanyaji wa taatifa za mafuta na gesi asilia katika sekondari ya Paje Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Alisema utafiti wa awali uliofanyika kwa kushirikiana na kampuni ya RakGas ulikuwa wa ukusanyaji wa data za 2D na sasa hatua inayofuata ni ukusanyaji wa data za 3D kabla ya kuanza uchimbaji.

“Hii ni hatua muhimu katika mchakato wa utafutaji wa mafuta. Baada ya 3D, hatua inayofuata ni uchimbaji,” alisema.

Aliongeza kuwa uchambuzi wa data za awali umeonesha uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta au gesi katika maeneo ya kusini mwa kisiwa cha Unguja, hususan Paje na maeneo yanayolizunguka.

Kuhusu utekelezaji wa mradi, amesema shughuli zitahusisha kusafisha njia na zinaweza kuathiri baadhi ya mali za wananchi, ikiwemo mazao, hivyo tathimini itafanyika na fidia kulipwa kwa wahusika wote.

Alisema kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa Mei mwaka huu na magari maalumu yatatumika kutoa mitetemo ardhini ili kukusanya taarifa za kijiolojia.

“Wananchi wasishtuke watakapoona magari hayo au vifaa vinavyotumika ardhini, bali watoe ushirikiano,” alisema.

Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuwaelimisha watoto wao ili wasivurugwe na shughuli hizo.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA), Mohammed Salum Said alisema Serikali imeamua kusimamia moja kwa moja mchakato huo badala ya kutegemea wawekezaji pekee.

 Baadhi ya wananchi wameipongeza Serikali kwa kuwashirikisha mapema katika mradi huo.

Mkazi wa Paje, Mjaka Haji Issa amesema utoaji wa elimu hiyo umeongeza uelewa na kuimarisha utayari wa wananchi kushiriki.

“Mara nyingi miradi mikubwa huja bila wananchi kushirikishwa, lakini safari hii tumepata elimu na tupo tayari kutoa ushirikiano,” amesema.

Naye Mustafa Fatawi Mussa amesema mradi huo una manufaa kwa jamii na ameahidi kushirikiana ili kuhakikisha unafanikiwa na Zanzibar inanufaika na rasilimali ya mafuta na gesi asilia.