‘Ajira kwa watu wenye ulemavu bado hairidhishi’

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jacob Mwinula, amesema licha ya uwepo wa sheria inayotaka uajiri wa watu wenye ulemavu, utekelezaji wake bado ni mdogo.

Ikumbukwe, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inataka taasisi zenye wafanyakazi kuanzia 20 kuajiri angalau asilimia tatu ya watu wenye ulemavu na kuwawekea mazingira rafiki ya kazi.

Hayo yamebainishwa na Mwinula kwenye majadiliano yaliyoandaliwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, yaliyoandaliwa na Jukwaa la Watendaji Wakuu Tanzania (CEOrt) kupitia programu ya Think Equal, Lead Smart (TELS) inayotekelezwa kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation.

Akizungumza, Mwinula amesema: “Sheria inataka taasisi zenye wafanyakazi 20 na kuendelea kuajiri angalau asilimia tatu ya watu wenye ulemavu, lakini utekelezaji wake bado uko chini ya asilimia moja, jambo ambalo linahitaji hatua za haraka.”

Amesema katika utekelezaji wa takwa hilo la kisheria, kwa upande wa sekta ya umma umefikia asilimia 0.37 pekee, huku sekta binafsi ikiwa asilimia 0.2, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza juhudi za kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa.

Mwinula amezitaka taasisi kuwekeza katika mazingira rafiki ya kazi, ikiwemo vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu wa kuona na kusikia, miundombinu inayowezesha utembeaji, pamoja na maeneo rafiki ya kujisitiri.

Katika kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo, “Ni hatua gani zinazochochea ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika maeneo ya kazi,” wadau, wakiwemo viongozi wa Serikali, watunga sera, waajiri kutoka sekta binafsi na umma pamoja na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu kwa ujumla, wamejadili changamoto zinazowakwamisha kupata ajira katika maeneo ya kazi, ambapo wametoa wito kusimamiwa kikamilifu kwa sheria hiyo.

Mshauri wa Kisheria wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata), Novath Rukwago, amesema Tanzania imeridhia mikataba ya kimataifa, ikiwemo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na lile la Umoja wa Mataifa.

Mratibu wa Miradi kutoka Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEOrt), Warda Shege akiwasilisha mada wakati wa kongamano lililoandaliwa kwa pamoja na CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kupitia programu ya Think Equal, Lead Smart (TELS) kujadili changamoto zinazowakwamisha watu wenye ulemavu kupata fursa za ajira.

“Matakwa haya ni sehemu ya ajenda ya Taifa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika maendeleo ya nchi,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema baadhi ya waajiri bado wanaogopa gharama za kuboresha mazingira ya kazi kwa watu wenye ulemavu, jambo linalochangia kuwanyima fursa za ajira.

Akitoa ushuhuda wake, Meneja wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu kutoka CCBRT, Frederick Anigallah, amesema wenye ulemavu bado wanakumbana na unyanyapaa mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Niliwahi kuzuiwa kushiriki usaili kwa kudhaniwa kuwa ni ombaomba, licha ya kuwa na sifa zote stahiki,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa CEOrt, Hawa Urungu, amesema mjadala huo ni sehemu ya juhudi za pamoja na Vodacom Tanzania Foundation kupitia programu ya TELS tangu mwaka 2024, za kuimarisha usawa na ujumuishaji wa makundi maalum, hususan wanawake na watu wenye ulemavu, katika shughuli za kiuchumi.

Naye Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema kongamano hilo lina mchango mkubwa katika kuhamasisha ushiriki wa wadau wote kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

“Kupitia programu ya TELS, tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha makundi maalumu yanawezeshwa na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa,” amesema.

Kwa ujumla, wadau walikubaliana kuwa kuna haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa sera na sheria, pamoja na kubadilisha mitazamo ya jamii ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa katika ajira na maendeleo ya kiuchumi.