Sh1.3 bilioni kupunguza upotevu wa maji Kilimanjaro

Moshi. Wakati asilimia 69 ya upotevu wa maji katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, ukichangiwa na ubovu wa miundombinu ya maji, Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) limepanga kutumia zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa ajili ya kurekebisha miundombinu hiyo.

Wilaya nyingine zitakazonufaika na mradi huo ni Siha, Longido na Arumeru, pamoja na Loitoktok iliyopo nchini Kenya mpakani na Tanzania kwa upande wa Wilaya ya Rombo.

Akizungumzia mradi huo leo Aprili 19, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo na kwamba zaidi ya wananchi 200,000 watanufaika na mradi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala akizungumzia changamoto ya maji wilayani humo na mpango wa kutatua changamoto hiyo.

“Moja ya changamoto kubwa Rombo ni maji, sasa kwa kushirikiana na WWF na Coka cola tunakwenda kutatua tatizo la maji Wilaya ya Rombo hususani katika vyanzo vya   Rongai. Tunaamini tukirekebisha vile vyanzo vya maji vinaweza kutusaidia sana katika maeneo yetu ya Wilaya ya Rombo, maana changamoto yetu kubwa sisi ni maji,” amesema Mwangwala

Amesema baadhi ya miundombinu ya maji ya zamani imekuwa ikipoteza maji mengi na hivyo maji yanayofika kwa wananchi yanakuwa ni asilimia ndogo kulingana na mahitaji ya wananchi.

“Vile vidakio vya maji (intake) ambavyo vilikuwa vinavuja kutokana na miundombinu yake kuwa ni ya zamani, ikifanyiwa maboresho maana yake zaidi ya asilimia 69 ya upotevu wa maji ambao upo kwa sasa utakuwa umekwisha. Upatikanaji wa maji utakuwa ni mzuri kwa sababu maeneo mengi yatakuwa yamezibwa,” amesema DC Mwangwala.

Aidha, amesema maboresho hayo yakifanyika wataondokana na changamoto hiyo ya maji na kwamba hata mabadiliko ya tabianchi yanapojitokeza hawataathirika zaidi.

Pamoja na mambo mengine, amesema kipindi cha kiangazi wananchi hupata maji kwa asilimia 42 na masika kwa asilimia 69 jambo ambalo amesema hali hiyo bado hairidhishi.

Kipindi cha masika tuna maji, lakini kiangazi tunapata changamoto ya maji. Tunaenda kuweka miundo mbinu ambayo inaweza kutusaidia tupate maji kipindi cha kiangazi, na kipindi cha masika hivyo kimsingi warsha hii imekuwa ni nzuri na kimsingi tumekubali kupokea mradi huu ambao utakuwa na faida kubwa kwa wananchi wetu.

Meneja wa mradi huo unaotambulika kama ‘Waterways for Resilience’, Novat Kessy, amesema mradi huo utatumia mifumo ya maji kuongeza ustahimilivu wa maji katika wilaya hizo na kwamba utatumia dola za Marekani 519,000 sawa na Sh1.3 bilioni za Kitanzania kwa ajili ya maboresho.

Meneja Mradi unaotambulika kama ‘Waterways for Resilience’ kutoka shirika la uhifadhi wa mazingira (WWF)Novat Kessy, akizungumzia mradi huo na namna ambavyo utapunguza changamoto ya upotevu wa maji.

“Tumechagua wilaya hizi kwa sababu katika ukanda wa Kaskazini ndio umeathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo mradi huu ambao unatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2025 hadi 2027 utawafikia wananchi 10,000,” amesema Kessy na kuongeza;

“Mradi huu utasaidia kurekebisha miundombinu ya maji ambayo ipo eneo la Rongai ambao unafaidisha vijiji vya Kikelelwa, Nalemuru lakini na wananchi wa Loitoktok katika nchi ya Kenya.”

Jenista Kawau, mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Rombo, amesema endapo mradi huo ukikamilika kwa wakati utapunguza kero ya maji kwa asilimia kubwa, kwa kuwa kipindi cha kiangazi yanakuwa ya mgao na wakati mwingine kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Mwananchi mwingine, Agatha Temu, amesema upatikanaji wa maji toshelevu katika Wilaya ya Rombo ni changamoto kutokana na   kuwa machache hususani katika kipindi cha kiangazi.