Arusha. Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, imewatia hatiani ndugu wa damu watatu kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya ndugu yao, yaliyotokea katika kijiji cha Ifundwa, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa.
Aidha, mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wengine wawili baada ya kuwakuta hawana kesi ya kujibu, ambapo iliridhika kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuwahusisha na tukio hilo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 3764/2025, waliotiwa hatiani ni James Kulwa, Samson Kulwa na Lugendo Mihangwa, huku ikiwaachia huru Lujegi Musa na Jibunge George, ambao kwa pamoja walishtakiwa kwa kosa la kumuua ndugu yao, Nambo Golani.
Hukumu ya Jaji Abubakar Mrisha iliyowekwa katika tovuti ya mahakama Aprili 17, 2026 haikuonyesha adhabu baada ya kutiwa hatiani, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code), adhabu pekee ya kosa hilo ni kunyongwa hadi kufa.
Katika kesi hiyo, ndugu hao watano walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Jaji Mrisha amesema upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha bila shaka yoyote kuwa washtakiwa watatu walihusika moja kwa moja katika mauaji hayo ya kikatili. Alieleza kuwa ushahidi wa utambuzi uliotolewa na mashahidi ulikuwa wa kuaminika na uliungwa mkono na mazingira ya tukio pamoja na ushahidi wa kitabibu.
Ili kuthibitisha shtaka hilo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba, huku utetezi ukiwa na mashahidi watatu (washtakiwa waliotiwa hatiani).
Shahidi wa kwanza, Holo Magilali (mke wa marehemu), alidai kuwa siku ya tukio, usiku wa manane, alisikia mlango ukifunguliwa kwa nguvu. Alipoamka, aliwaona watu wawili ndani ya chumba chao cha kulala, ambao walimfunga marehemu kwa kamba na kumlazimisha kutoka kitandani, wakimuuliza kuhusu madeni yake.
Alidai kumsikia mumewe (sasa marehemu) akijibu kuwa hakuwa na deni lolote, na baadaye washambuliaji hao walianza kumshambulia kwa kumjeruhi kwa panga kabla ya kumburuza na kumtoa nje ya nyumba.
Alidai kuwatambua washambuliaji hao kuwa ni Samson, maarufu kwa jina la Shinje (shemeji yake), na Lugendo, lakini hakuweza kumtambua mtu wa tatu aliyekuwa pamoja nao.
Alieleza kuwa mumewe alipiga kelele kuomba msaada nje. Alifanikiwa kufungua mlango uliokuwa umefungwa kwa nje na kukimbilia kwa shemeji yake, Mwandu Jibunge, lakini hakupata msaada. Baadaye alikwenda kwa jirani, na waliporejea walikuta mwili wa mumewe ukiwa uchi na wenye majeraha kichwani, shingoni na kifuani.
Shahidi wa tatu, ambaye ni ofisa wa polisi aliyechunguza kesi hiyo, alidai kuwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji, aliongozana na wenzake hadi eneo la tukio ambapo walikuta mwili ukiwa na majeraha ya kukatwa kichwani, shingoni na kifuani, huku damu ikiwa imetapakaa eneo hilo.
Alidai kuwa maelezo ya shahidi wa kwanza na wa pili yaliwezesha kukamatwa kwa washtakiwa wawili, akiwemo James, ambaye alikutwa amejificha chini ya uvungu wa kitanda na kupelekwa Kituo cha Polisi Namanyere kwa mahojiano zaidi.
Shahidi wa nne, ambaye ni daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo, alihitimisha kuwa chanzo cha kifo ni kupoteza damu nyingi kufuatia majeraha makubwa aliyoyapata kichwani, kifuani na mgongoni.
Katika utetezi wao, washtakiwa walikana kuhusika na mauaji hayo na kudai kuwa walikamatwa bila sababu za msingi.
James alidai kuwa akiwa nyumbani kwake Juni 5, 2022, watu kadhaa waliingia nyumbani kwake na kumtaka atoke nje, kisha walimpeleka kwa pikipiki hadi Kituo cha Polisi Namanyere kwa mahojiano kuhusu mauaji hayo.
Alidai kuwa akiwa kizuizini alivuliwa nguo, kufungwa pingu na kuteswa kwa kipindi cha mwezi mmoja, jambo lililosababisha majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo miguu kuvimba.
Aidha, alikana kuwepo kwa mgogoro wowote wa ardhi na marehemu. Alidai kuwa alifahamu mgogoro uliokuwepo kati ya marehemu na baba yake mdogo, George Jibunge, uliotokana na kutokukubaliana kuhusu kumsaidia kulipa mahari.
Alieleza kuwa marehemu alikuwa akiishi Ifundwa tangu 1996 na tangu wakati huo hawakuwa na mawasiliano yoyote, hivyo akakana kuhusika na mauaji hayo.
Kwa upande wake, Samson alidai kukamatwa Juni 28, 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete, Tabora. Alisema kuwa alipofikishwa kituo cha polisi alivuliwa nguo, kufungwa pingu na kuteswa, huku akishtakiwa kwa kosa la mauaji ambalo alikanusha kuhusika nalo.
Alikana kufahamu mgogoro wa ardhi unaodaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo na kuiomba mahakama imwachie huru.
Kwa upande wake, Lugendo alidai kuwa Julai 4, 2022, akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Kidema, aliamshwa usiku na watu waliojitambulisha kama maofisa wa polisi. Alidai kuwa aliamriwa kuvua nguo zote, kufungwa pingu na kuteswa, ikiwemo kuchomwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa pasi ya moto.
Alidai kuwa kati ya Mei 29 hadi Juni 5, 2022 alikuwa nyumbani kwake kutokana na kuumwa mguu na hakuwahi kutoka. Hata hivyo, alikiri kukutana na marehemu katika mazishi ya baba wa marehemu huko Maswa, na kusisitiza kuwa hakukuwa na mgogoro kati yao.
Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kueleza kuwa haukuweza kuibua shaka juu ya ushahidi thabiti uliotolewa na upande wa mashtaka.
Jaji Mrisha alisisitiza kuwa, ingawa sheria inaonya juu ya hatari ya kutegemea ushahidi wa utambuzi, katika kesi hiyo mashahidi waliwafahamu vyema washambuliaji na waliwataja majina yao mapema, jambo lililoondoa uwezekano wa kukosea utambulisho.
Mahakama pia ilibaini kuwa kitendo cha washambuliaji kumfunga marehemu, kumuhoji na kisha kumshambulia kwa mapanga kilionyesha wazi kuwepo kwa nia ovu ya kuua.
“Kwa kuzingatia ukubwa wa majeraha yaliyosababisha kifo na namna shambulio lilivyotekelezwa, mahakama inaridhika kuwa kulikuwa na nia ya kusababisha kifo,” amesema Jaji Mrisha katika hukumu yake.
Kutokana na hoja hizo, mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka umetimiza wajibu wake wa kuthibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote na kuwatia hatiani washtakiwa watatu kwa kosa la mauaji kama walivyokuwa wameshtakiwa.
